The House of Favourite Newspapers

Video: Tamasha la Simba Day Kufanyika Mwezi Septemba

0

KAIMU Afisa Habari wa Simba Ezekiel Kamwaga leo Agosti 20, 2021 amefunguka kuwa Tamasha la Simba Day ambalo awali lilitangazwa kufanyika Agosti 28, 2021 na sasa tamasha hilo linatarajiwa kufanyika mwezi Septemba mwaka huu ambapo uongozi utatangaza tarehe rasmi muda wowote.

 

Kamwaga amefafanua ishu hiyo kwenye mahojiano maalum katika kipindi cha Krosi Dongo kinachoruka kupitia +255 Global Radio ambapo alisema kuwa uongozi wa Simba haukutoa  taarifa rasmi kuhusu tamasha la Simba Day ambalo awali kuna taarifa ziliibuka kuwa huenda lingefanyika Agosti 28.

“Klabu haijatoa taarifa rasmi kuhusu kufanyika tamasha la Simba Day Agosti 28 na hii ni kutokana na sababu tofauti, kwanza kocha mkuu bado anaendelea kutengeneza kikosi kwenye maandalizi kwani tukio la Simba Day linakwenda sambamba na timu kucheza mechi.

 

“Ratiba yetu ya kwanza ilikuwa timu irudi kesho Jumamosi lakini kutokana na sababu alizotupa mwalimu kambi imesogezwa mbele na kikosi kitarejea nchini mwisho wa mwezi huu hivyo tamasha la Simba Day litafanyika mwezi Septemba na muda wowote klabu itatoa taarifa kuhusu tamasha letu.”

 

Aidha Kamwaga aligusia kuwa mchakato wa uzinduzi wa jezi mpya za Simba kuelekea msimu ujao umekamilika na tukio la uzinduzi litafanyika kwenye wiki ya Simba ambayo inatarajiwa kufanyika mwezi Septemba.

 

“Kuhusu kuchelewa kwa uzinduzi wa jezi mpya za msimu huu ni muingiliano wa ratiba na ushiriki wa Simba kwenye michuano ya kimataifa, uzinduzi rasmi wa jezi utafanyika kwenye wiki ya Simba na utakuwa uzinduzi wa aina yake ambao haujawahi kutokea na baada ya uzinduzi jezi zitakuwa zinapatikana nchi nzima.” Aliongeza Kamwaga.

 

Kesho Jumamosi kikosi cha Simba kinatarajiwa kushuka dimbani kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya FAR Rabat inayonolewa na Sven Vandebroeck kabla ya kurudi nchini kwa ajili ya tamasha la Simba Day.

STORI NA HUSSEIN  MSOLEKA | GPL

Leave A Reply