The House of Favourite Newspapers

Fahamu Ukweli Kuhusu Chanjo ya Ukimwi Iliyozinduliwa

0

-Matumaini mapya ya kutokomeza gonjwa hilo hatari yaamsha furaha kwa wengi

-Teknolojia inayotumika ni ya kisasa na tofauti na nyingine zote zilizowahi kutumika

-Mafanikio ya chanjo za Corona ndiyo yaliyochochea kupatikana kwa chanjo ya Ukimwi

 

Taarifa za Kampuni ya Moderna ya nchini Marekani, kuanza majaribio ya chanjo ya Ukimwi kwa binadamu, zimepokelewa kwa shauku kubwa kutoka maeneo mbalimbali duniani! Shauku hiyo inatokana na ukweli kwamba kwa zaidi ya miaka 38 sasa, maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), limekuwa ni janga kubwa hususan kwa nchi za Kiafrika, Kusini mwa Bara la Asia.

 

Takwimu za Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa la kutokomeza UKIMWI, (UN-AIDS), zinaeleza kwamba tangu kuibuka kwa janga hilo mwaka 1981, takribani watu milioni 79.3 wamepata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na kati yao, watu milioni 36.3 wamefariki dunia.

 

Idadi hiyo ya watu inatosha kukuonesha ni kwa kiasi gani Ugonjwa wa Virusi vya Ukimwi umekuwa tishio duniani kote, hususan katika nchi maskini.

 

Hatua kubwa iliyopigwa na Kampuni ya Moderna yenye makao makuu yake Cambridge, Massachusetts nchini Marekani, imepokelewa kwa furaha kubwa na wengi wanaamini kwamba hiyo ni hatua muhimu sana ya kwenda kuutokomeza ugonjwa huo hatari.

 

Shauku ya wengi ni kutaka kujua zaidi kuhusu chanjo hiyo na jinsi inavyofanya kazi. Taarifa kutoka Moderna, zinaeleza kuwa majaribio ya kwanza ya chanjo hiyo kwenye mwili wa binadamu, yanaanza Agosti 19, 2021 na yanatarajiwa kuendelea hadi mwaka 2023 na kwa kuanzia, watu 56 wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 50, watafanyiwa majaribio hayo.

 

Kampuni ya Moderna, hawako peke yao katika utafiti huo kwani wanashirikiana na wadau wengine kadhaa, vikiwemo Chuo Kikuu cha Texas kilichopo San Antonio nchini Marekani, Chuo Kikuu cha George Washington, Kituo cha Utafiti wa Saratani cha Fred Hutchinson Cancer Research Center na Chuo Kikuu cha Emory, vyote ikiwa ni kutoka nchini Marekani.

 

Chanjo zinazoanza kufanyiwa majaribio, zipo za aina mbili, mRNA-1644 na mRNA-1644v2-Core ambazo zote tayari zimeshakidhi vigezo vya kufanyiwa majaribio kwenye mwili wa binadamu, baada ya kufanyiwa majaribio ya awali kwa wanyama wakiwemo panya wa maabara na kuonesha mafanikio makubwa.

 

Hizi siyo chanjo za kwanza kufanyiwa majaribio, zipo nyingine kadhaa ambazo zimewahi kujaribiwa lakini hazikuweza kufikia hatua ya kufanyiwa majaribio kwenye mwili wa binadamu.

Inaelezwa kwamba, safari hii Kampuni ya Moderna imeweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa, ikitumia uzoefu uliotumika kutengeneza chanjo ya Virusi vya Corona, Covid 19.

 

Moderna ina matumaini ya kufanikiwa kwa chanjo hiyo kutokana na teknolojia mpya ra mRNA iliyotumika, ambayo ndiyo hiyo pia iliyotumika kutengeneza chanjo ya Moderna ya Virusi vya Corona, ambayo imeonesha ufanisi wa zaidi ya asilimia 90 na kuidhinishwa kutumika duniani kote.

 

Chanjo za Corona za Moderna na Pfizer zimetajwa kupata mafanikio zaidi, kutokana na kutumia teknolojia ya mRNA (Messenger RNA).

 

Teknolojia ya mRNA, inatajwa kuwa na ufanisi mkubwa zaidi wa kupambana na virusi wa aina mbalimbali kwa sababu, virusi vina kawaida ya kuwa vinabadilikabadilika mara kwa mara kwa hiyo njia pekee inayoweza kutumika kupambana navyo, ni mRNA ambayo nayo hubadilika kadiri kirusi kinavyobadilika.

 

Virusi vya Ukimwi viligunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1981 ambapo tangu miaka hiyo mamilioni ya watu wamepoteza maisha yao kutokana na janga hilo lisilo na kinga wala tiba.

JINSI CHANJO INAVYOFANYA KAZI

Kwa kawaida, katika utengenezaji wa chanjo, kinachofanyika huwa ni kuifundisha kinga asili ya mwili, namna ya kuvitambua kwa haraka vimelea vya aina fulani na kuvishambulia kabla havijaleta madhara katika mwili.

 

Kinachofanyika inakuwa ni kuchukua chembechembe za kirusi husika (antigens) kisha kuzidhoofisha kwa kutumia mbinu ya ‘genetic engineering’ na kutumia chembechembe hizo, kuingizwa kwenye mwili wa binadamu kwa kiasi kidogo, kwa lengo la kwenda kuishtua kinga ya mwili kuweza kutambua uwepo wa vimelea hivyo, na kupambana navyo mpaka kuvishinda kisha kujenga kinga ya mwili endapo virusi vya aina hiyo vitaushambulia tena mwili.

 

Kitendo hiki kitaalamu huitwa Live Attenuated Vaccines (L.A.V) ambapo magonjwa mengi yaliyokuwa yakitisha kwa kusababisha vifo kama Polio, Surua, Ndui na kadhalika, yameweza kudhibitiwa kabisa kwa watoto wadogo kupewa chanjo ambayo huwalinda katika kipindi chote cha maisha yao.

 

Hata hivyo, hali imekuwa tofauti kwa virusi vya Ukimwi ndiyo maana chanjo ya uhakika haijapatikana kwa takribani miaka 38. Hii ni kwa sababu, Virusi vya Ukimwi (HIV), vimekuwa na kawaida ya kujibadilishabadilisha.

 

Kivipi? Vinapoingia ndani ya mwili, ndani ya muda mfupi tu huingia kwenye seli na kujibadilisha kufanana na seli za mwili, kitendo ambacho kitaalamu huitwa camouflage! Kitendo hiki huzichanganya seli za kinga ya mwili na kushindwa kuelewa adui ni yupi na rafiki ni yupi, hivyo kushindwa kuelewa wapi pa kushambulia.

 

Mbaya zaidi, licha ya kujibadilisha na kufanana na seli za mwili, virusi vya Ukimwi huanza kubadilisha DNA (vinasaba) vya seli za mwili, kwenda kwenye RNA na kudhoofisha zaidi seli za mwili wakati vyenyewe vikiendelea kuzaliana kwa wingi.

 

Ni hapo ndipo wanasayansi walipokuja na mbinu mpya, mRNA!

Katika chanjo zinazotumia teknolojia hii, kinachofanyika siyo kuingiza mwilini chembechembe za virusi kwa ajili ya kutengeneza kinga, bali ni kuingiza mwilini Messenger RNA ambayo huenda kufanya kazi kama virusi viingiapo ndani ya mwili, kisha kujenga kinga kuanzia ndani kabisa ya seli, kiasi kwamba ikitokea virusi halisi wakiingia mwilini, wanakuta tayari kuna mazingira ambayo hayaviwezeshi kuendelea kuishi na hivyo kufa vyenyewe.

 

Hiki ndicho kinachofanyika kwenye chanjo mpya na tayari matumaini yamekuwa ni makubwa kutokana na jinsi mbinu hiyo, ilivyoonesha ufanisi katika kupambana na Virusi vya Corona kama ilivyoelezwa.

 

Majaribio haya yanayofanywa katika chanjo ya Moderna, ni hatua ya tatu katika utengenezaji wa chanjo hiyo. Hatua za awali, zilikuwa ni kufanyika kwa utafiti wa kimaabara kisha kutengenezwa kwa chanjo.

 

Hatua ya pili ilikuwa ni kuanza kufanya majaribio ya chanjo hizo kwa kuwatumia wanyama ambao wanafanana kwa kiasi kikubwa na binadamu katika jinsi mifumo ya miili yao inavyofanya kazi na hapa, panya wa maabara huonekana kuwa ndiyo chaguo sahihi zaidi.

Hatua ya tatu ndiyo hii inayokwenda kufanyika sasa, ya majaribio kwa mwili wa binadamu, ambapo awamu ya kwanza itahusisha watu wachache, awamu zinazofuatia zitahusisha watu wengi zaidi na baada ya majaribio ya awamu tatu, hapo ndipo chanjo hiyo itakapokuwa imekamilika.

 

Matokeo yatakayotolewa katika majaribio hayo, ndiyo yatakayotumika kuthibitisha kwamba chanjo hiyo ina uwezo wa kupambana na Virusi vya Ukimwi au laah!

 

Kama ilivyoelezwa, hii si mara ya kwanza kwa chanjo ya Virusi vya Ukimwi kufanyiwa majaribio.

 

Tangu mwaka 1987, zaidi ya chanjo 30 za Virusi vya Ukimwi zimefanyiwa majaribio zikihusisha zaidi ya watu 10,000 na matokeo ya majaribio hayo, yamekuwa yakiendelea kufanyiwa utafiti wa kina zaidi kuelekea kwenye upatikanaji wa chanjo ya kudumu ambayo inaweza kuwa msaada mkubwa katika kupambana na Maambukizi ya Virusi vya Corona.

Leave A Reply