The House of Favourite Newspapers

Simba, NMB Walivyozindua Kadi za Aina Tatu za Mashabiki

0

 

KLABU ya Simba jana Jumamosi kwa kushirikiana na Benki ya NMB katika kuwafikia mashabiki wa timu hiyo walizindua akaunti, Simba Account ambazo zitakuwa maalum kwa ajili ya mashabiki wa timu hiyo.

Wawili hao walizindua akaunti hizo ambazo zitawahusisha mashabiki wa timu hiyo, mashabiki platnums na akaunti za watoto.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula alisema: “Mashabiki wanatakiwa kupata faida kutokana na ushabiki wao, ndiyo maana tumekuja na akaunti na kadi hizi.

“Akaunti hizi za mashabiki zitakuwa tatu, kadi za mashabiki, kadi za mashabiki platnums na kadi za watoto.

 

“Kwa Mwanasimba atafungua akaunti kwa shilingi elfu 5,000, lakini pia kutakuwa na akaunti za kina mama zitajulikana kama Malkia Akaunti na akaunti za watoto. Akaunti zote zitaambatana na bima za maisha.

“Tumeingia nao mkataba, NMB kwa kuwa wana mawakala na matawi mengi nchini, wana zaidi ya mawakala elfu 20 nchini,” alisema Kajula.

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu Benki ya NMB, Filbert Mponzi alisema: “Benki ya NMB inajulikana kama benki bora nchini na kwa kuwa Simba ni klabu bora kwa hapa nchini, tunaamini tutaenda kufika mbali kwa kuwa sisi wote tupo sehemu kubwa ya nchi.

“Tunazindua NMB Simba akaunti, NMB Queen account, hizi akaunti zitakuwa na faida kubwa sana, kwa kuwa kadi hizo utaweza kufanya miamala, kupata mkopo wa Mshiko Fasta ambao unaanzia shilingi elfu 1000 hadi laki tano.

“Pia kuna faida nyingine ambazo shabiki atazipata ikiwemo kupata punguzo kubwa katika manunuzi ya vitu, bima ya afya, kufanya miamala na vitu vingine.

“Lakini pia kutakua na kadi za watoto na hapa tunawasihi wazazi wawafungulie watoto wao kadi hizi kwani zina faida sana kwa watoto wao.

 

“Kama tayari una akaunti ya NMB tutakupa kadi nyingine ambayo itakufanya uweze kufanya miamala tofauti na kadi yako ya kawaida.

“Kuelekea kwenye Simba Day, tutafanya usajili wa mashabiki wote wa Simba na tunaamini tutasajili mashabiki wengi katika muda huo.

“Mahusiano haya yatakuwa na faida kubwa sana kati yetu na Simba na tunawaambia mashabiki waje kwa wingi kwa kuwa watapata faida nyingi kama ambavyo nimezitaja,” alimaliza Mponzi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu alisema: “Tumeingia mkataba wa ushirikiano na NMB ambapo ushirikiano huu kwa kiasi kikubwa ndiyo unatusaidia kuendesha timu, kusajili wachezaji wazuri na mengineyo.

“Kwa mashabiki wetu ambao walikuwa na kadi na taasisi nyingine ambazo tulikuwa tunashirikiana nazo huko nyuma tunawaomba wahamie NMB sasa.”

Ikumbukwe kuwa Simba inakuwa klabu ya pili NMB kuingia nayo mkataba wa kutoa kadi za mashabiki baada ya hivi karibuni kuingia mkataba kama huo na Yanga.

Katika shughuli hiyo, Simba walimtambulisha winga wao mpya Mcameroon, Willy Essomba Onana ambaye amesajiliwa na klabu hiyo akitokea Rayon Sports ya Rwanda.

Leave A Reply