The House of Favourite Newspapers

Simba SC Yawekewa Ukuta wa Berlin

STORI| MUSA MATEJA | CHAMPIONI JUMAMOSI | DAR ES SALAAM

UKUTA wa Berlin ulijengwa na Wajerumani mwaka 1961 na kuigawa nchi yao katika sehemu mbili, yaani Ujerumani Mashariki na Ujerumani Magharibi, lakini mwaka 1989 ukafunguliwa na ilipofika mwaka 1992 ukawa ushavunjwa.

Ilikuwa ngumu kwa mtu kuvuka ukuta huo, sasa Simba imewekewa ngumu katika mechi zake tatu za Kanda ya Ziwa zinazoweza kuamua majaliwa yake ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Hadi sasa Simba iliyoanzishwa mwaka 1936, ipo kileleni mwa ligi kuu ikiwa na pointi 55 katika mechi 24 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 53 katika idadi kama hiyo ya mechi.

Mechi tatu za Simba katika Kanda ya Ziwa, ni dhidi ya Kagera Sugar Aprili 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, halafu Aprili 8 dhidi ya Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na itamalizia na Toto African uwanj1961ni hapo Aprili 12, mwaka huu.

Kagera Sugar ina mchezaji mkongwe ambaye amewahi kucheza Simba, huyu ni kipa Juma Kaseja ambaye amepanga kuionyesha timu hiyo kuwa yeye bado wamo kwa kuizuia kupata ushindi.

Kaseja aliliambia Championi Jumamosi: “Tunajifua siku zote, si kwa sababu ya Simba pekee, bali timu zote na sasa walio mbele yetu ni Simba, tutapambana nao kuweka heshima yetu.

“Wao wanataka ubingwa lakini sisi tunataka kumaliza tukiwa katika nafasi za juu, hatuwezi kukubali kuwa njia ya wengine japokuwa wapinzani wetu si wabaya sana.”

Naye Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime, alisema atahakikisha anakiandaa vizuri kikosi chake ili kiweze kupata matokeo mazuri mbele ya Simba.

MBAO NAO HAWATAKI

Katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya Simba Oktoba 23, mwaka jana, Mbao ilifungwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam mfungaji akiwa Mzamiru Yassin.

Kocha wa Mbao, Etienne Ndairagije, alisema: “Simba ni timu nzuri na ni timu kubwa, hilo silikatai, nilishacheza nao, sitarajii tena kutoa nafasi ya kupoteza hapa nyumbani.”

Ndairagije, raia wa Burundi, ni kocha aliyewahi kumfundisha mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe na Laudit Mavugo wa Simba kwa nyakati tofauti walipokuwa wakiichezea Vital’O ya kwao Burundi.

TOTO HAWATAKI KUSHUKA DARAJA

Toto sasa inafundishwa na Novatus Frugence ikiwa katika nafasi ya 14 na pointi 25 katika timu 16 za ligi kuu, imepanga kushinda mechi za nyumbani ili isishuke daraja.

Frugence aliliambia gazeti hili kwamba: “Tuna wakati mgumu sana wa kufanya kila namna ili tubaki ligi kuu, hivyo kwa kutambua hilo kila mchezo ulio mbele yetu sasa ni fainali.

“Simba inataka ubingwa lakini sisi tunataka kubaki ligi kuu, hatuwezi kukubali kirahisi kushuka eti ili Simba iwe bingwa, hakuna kitu kama hicho.”

Hata hivyo, Simba inayonolewa na Kocha Joseph Omog imetamba kufanya vizuri katika mechi hizo tatu za Kanda ya Ziwa ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa.

Comments are closed.