Simba: Tunaandika historia Taifa

KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems, ameweka kando kipigo walichokipata mbele ya JS Saoura kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na kutamka kwamba wataweka historia katika mechi yao ya mwisho dhidi ya AS Vita.

 

Simba ikiwa ugenini nchini Algeria juzi Jumamosi ilipokea kichapo cha mabao 2-0 mbele ya wenyeji wao JS Saoura anayoichezea Mtanzania, Thomas Ulimwengu.

 

Kikosi hicho kwa sasa kinakamata nafasi ya mwisho kikiwa na pointi sita huku Saoura wakiwa vinara na pointi nane.

 

Lakini jinsi msimamo wa kundi hilo la D ulivyo, kila timu ina nafasi ya kutinga robo fainali, na timu yoyote pia ina nafasi ya kuaga mashindano.

Simba, kama ilivyo kwa timu nyingine, wamebakiwa na mechi moja ambayo watacheza dhidi ya AS Vita katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Machi 16, mwaka huu, kama Simba wakishinda mechi hii watasonga hatua ya robo fainali na kuandika historia mpya.

 

Katika kundi hili, hadi sasa hakuna timu iliyofungwa nyumbani, kila timu imeshinda nyumbani, isipokuwa AS Vita akiwa nyumbani alitoka sare ya 2-2 na Saoura, na Saoura wakiwa home walitoka sare ya 1-1 na Al Alhy.

 

Hii inamaanisha kwamba Simba wana nafasi kubwa ya kuutumia uwanja wa nyumbani kupata ushindi wowote na kusonga mbele.

 

Mbelgiji huyo amesema kwake hajihangaishi sana na kipigo ambacho wamekipokea kutoka kwa Saoura, kwa kuwa anajua wanachotakiwa kufanya ni nini.

 

Amesisitiza wanaelekeza nguvu na akili katika mechi yao ya mwisho ambayo anataka kuandika historia kwenye mechi hiyo watakayocheza nyumbani.

 

“Hatukuwa na utendaji mzuri kwa kiuchezaji jana (juzi) na ndiyo maana ikawa vile. Wala sikuwa natarajia sana matokeo mazuri.

 

“Tutacheza Jumamosi ijayo katika mechi yetu ya mwisho ya kundi hili, najua tutapambana na wapinzani wa namna gani kwenye ligi hii.

 

“Lakini ninawaomba Mashabiki waje uwanjani kwa ajili ya kutuhimiza kuandika historia kwenye mechi hiyo,” alisema kocha huyo.

 

Said Ally, Dar es Salaam.

Toa comment