The House of Favourite Newspapers

Simba Wapiga Chini Ofa Ya Milioni 300 Kwa Salamba

Adam Salamba.

 

IMEBANIKA kuwa uongozi wa Simba umepiga chini ofa ya dola 150,000 ambazo ni sawa na shilingi milioni mia tatu (milioni 300) kwa ajili ya kumu­uza mshambuliaji wake, Adam Salamba.

 

Licha ya mshambuliaji huyo kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Simba, lakini uongozi wa timu hiyo umeamua kupiga chini ofa hiyo kutoka kwa wakala wa beki wa Rayon Sport ya Rwanda, Abdul Rwatubaye, Enzo Mupenzi mwenye uraia wa Rwanda na Ubelgiji.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Mupenzi ambaye anafanya kazi hiyo kupitia mawakala wakubwa duniani, alisema kuwa lengo la kumtaka mchezaji huyo ni kumpeleka Ulaya kwenda kufanya majaribio katika klabu ya Anderlecht ya Ubelgiji.

“Naona Simba hawataki kutupa Salamba kwa sababu sasa ni miezi mitatu tangu tuwatumie mkataba lakini CEO wa Simba (Crescentius Magori) amekuwa akizungusha tu, tumempa mkataba wa dola laki moja (milioni 229,305,000) ukiwa na bonasi ya dola 50,000 (milioni 114,663,000) lakini kagoma.

 

“Unajua sisi lengo letu ni kumuuza nje, sasa hatuwezi kumuuza kama hatuna mkataba na Simba juu ya mchezaji, na ukiangalia mchezaji mwenyewe hapati nafasi kwa nini hawataki kumuachia,” alisema Mupenzi.

 

Championi lilimtafuta Magori ambaye alisema kuwa: “Tatizo siyo kwamba sisi tumekataa kumuachia lakini unawezaje kumuchia mchezaji kwenye kipindi cha mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika aende nje kufanya majaribio?

 

“Sasa lazima ieleweke huu ni wakati mgumu kufanya hivyo labda ikifika Mei kwa kuwa mashindano yatakuwa yamekwisha tunaweza kufanya hivyo, lakini sasa hapana,” alisema Magori.

Stori Ibrahim Mussa, Championi jumatano

Comments are closed.