Simba yaanza kazi Zanzibar, Waarabu wajipange

Kikosi cha timu ya Simba

KIKOSI cha Simba kipo mjini Unguja kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mapinduzi na leo kitashuka uwanjani kupambana na Chipukizi katika mechi yake ya kwanza ya michuano hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Amaan.

Hata hivyo, wachezaji wa Simba watashuka katika mechi hiyo akili zao zote zikiwa kwenye mechi ya kimataifa ya Mabingwa Afrika ambayo watacheza Januari 12, mwaka huu dhidi ya JS Saoura ya Algeria kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam mechi hiyo, wachezaji wa Simba watakuwa na kazi moja tu ya kuhakikisha wanaitandika JS Saoura ili waweze kujitengenezea mazingira mazuri ya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

 

Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems, ameliambia Championi Ijumaa kuwa wamejipanga vilivyo kwa ajili ya mechi hiyo na anaendelea kuufanyia kazi baadhi ya upungufu aliouona katika mechi za kwanza za mtoano za michuano hiyo ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi mnono dhidi ya Waarabu hao.

 

Alisema katika mechi hizo, kuna mambo aliyaona ya kiufundi, hivyo ameshaanza kuyafanyia kazi na leo katika mechi dhidi ya Chipukizi anataka kuona ni jinsi gani wachezaji wake wameyapokea maelekezo yake hayo.

 

“Tumejipanga vizuri kwa ajili ya mechi hiyo ni matumaini yangu kuwa tutaibuka na ushindi japokuwa naamini kabisa mechi itakuwa ni ngumu.

 

“Kuna makosa ya kiufundi ambayo niliyaona katika mechi zetu za kwanza za hatua ya mtoano tulizocheza dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland pamoja na Nkana FC ya Zambia. “Kwa hiyo katika mechi ya kesho (leo) dhidi ya Chipukizi nitaitumia kuangalia ni jinsi gani maelekezo yangu niliyowapa wameyapokea na kuyafanyia kazi kikamilifu,” alisema Aussems.

Loading...

Toa comment