The House of Favourite Newspapers

Simba Yatua Rasmi Kwa Makusu

0

LILE dili la Simba na mshambuliaji Jean Marc Makusu Mundele, limeibuka upya na sasa klabu hiyo imerudi tena kwa nguvu kuhakikisha wanamsajili straika huyo ambaye kwa sasa anakipiga katika Klabu ya Orlando Pirates ya Sauzi kwa mkopo akitokea AS Vita ya DR Congo.

 

Simba chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya timu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’, walipitisha bajeti ya Sh bilioni 3 katika kikao cha mwisho kufanywa na bodi hiyo kwa ajili ya usajili wa wachezaji wapya wa maana jambo ambalo linaonyesha kuanza kufanya kazi kwa Simba kuanzia kwa Makusu Mundele.

 

Mundele ni mmoja wa washambuliaji waliofanya vizuri katika Klabu ya AS Vita msimu wa 2018-19, lakini kwa sasa amekuwa na maisha magumu tangu ajiunge na Orlando kwa mkopo akitokea AS Vita, jambo ambalo linamfanya mshambuliaji huyo kufikiria kuhama ndani ya timu hiyo.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, moja kwa moja kutoka nchini DR Congo, Kocha Msaidizi wa AS Vita, Raoul Shungu, amesema kuwa amesikia taarifa za Simba zikienea nchini humo kuwa wanamhitaji straika huyo japo bado hawajapokea ofa yao rasmi kutoka kwa Simba.

 

“Makusu ni mchezaji wa AS Vita bado ana mktaba na AS Vita, sisi kama makocha tunatamani kumuona akirejea tena ndani ya AS Vita, ni mchezaji mzuri mwenye uwezo mkubwa na alifanya vizuri sana wakati anacheza hapa, tunamkaribisha kwa mikono yote kama atarejea.

 

Kuhusu Simba nimesikia taarifa kuwa wanamhitaji japo bado hawajaleta ofa mezani ndani ya Vita, japo mkataba wake na sisi haumzuii yeye kwenda Simba, hayo yatakuwa ni maamuzi yake yeye mwenyewe kuchagua sehemu atakayohitaji kwenda kucheza,” alisema kocha huyo.

 

Naye alipotafutwa Makusu Mundele kuhusu kujiunga na Simba alisema kuwa yupo katika mazungumzo na klabu kadhaa ambazo zinamhitaji lakini hayupo tayari kuzitaja kwa kuwa hajafikia makubaliano na klabu yoyote kwa sasa.

 

“Bado sijakamilisha mazungumzo na timu yoyote, japo timu nyingi zinanihitaji na zipo katika mazungumzo na uongozi wangu ambao ndio wasimamizi wangu katika masuala ya usajili,” alisema mshambuliaji huyo.

 

Championi Ijumaa lilipomtafuta Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, kuzungumzia juu ya usajili wa mshambuliaji huyo simu yake iliita bila majibu.

Leave A Reply