The House of Favourite Newspapers

Simba Yaweka Rekodi ya Ubingwa Kibabe

0

TUPENI Kombe letu! Ndiyo kauli ambayo Wanasimba wanatamba nayo sasa ikiwa ni baada ya timu yao kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMC na kufikisha pointi 76.

 

Mabao ya Chris Mugalu dakika ya 2 na 44 ndiyo yaliyofanikisha ushindi huo muhimu kwao na kupunguza machungu ya kuchapwa bao 1-0 na watani zao wa jadi, Yanga, huku ikishuhudiwa KMC ikimaliza mechi pungufu ya mvhezaji mmoja baada ya beki wake, Vincent Andrew ‘Dante’ kutolewa kwa kadi nyekundu.

 

Ushindi huo ilioupata Simba kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, umeifanya kihesabu kuwa bingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo.

 

Pointi zao zinaweza kufikiwa na Yanga, lakini idadi ya mabao inawabeba Simba hata kama itapoteza mechi zake tatu zilizosalia.Simba hivi sasa imefikisha mabao 71 ya kufunga, huku ikiruhusu kufungwa mabao 13 na kuifanya tofauti ya mabao kuwa 58.

Idadi kubwa zaidi ya mabao kuliko timu zote ndani ya Ligi Kuu Bara msimu huu.Wakati Simba ikiwa na tofauti hiyo ya mabao, Yanga imefunga mabao 50, imeruhusu kufungwa mabao 21 na kufanya tofauti kuwa 29.

 

Yanga kuja kuwa sawa na Simba kwa mabao, mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara kwenye mechi zao mbili zilizobaki dhidi ya Ihefu na Dodoma Jiji, watatakiwa kufunga si chini ya mabao 29 ambayo kwa wastani kila mechi ni mabao 15, huku Simba ipoteze mechi zote tatu zilizobaki.

 

Hivi sasa Yanga ina pointi 70, ikishinda mechi zote mbili, inafikisha pointi 76 ambazo Simba inazo kwa sasa. Kumbuka Simba imesaliwa na mechi tatu dhidi ya Coastal Union, Azam na Namungo ambazo zote itachezea Dar.

 

Yanga yenyewe imesaliwa na mechi mbili, dhidi ya Ihefu itakayochezwa nyumbani na Dodoma Jiji ugenini.

 

Kwa hesabu hizo, ni wazi Simba imetangaza ubingwa kwa kuifunga KMC jana ambapo ubingwa huo wanne mfululizo kwao, unaifanya timu hiyo kuifukuzia rekodi waliyoiweka wenyewe kuanzia mwaka 1976 hadi 1980 walipobeba mara tano mfululizo.Kabla ya Simba kufanya hivyo, Yanga nao waliwahi kuchukua taji hilo mara tano mfululizo kuanzia mwaka 1968 hadi 1972.

 

Msimu huu Simba imekuwa na wastani mzuri wa kufunga mabao kupita misimu yote mitatu nyuma ambayo wamewahi kubeba ubingwa wa ligi hiyo.Msimu wa 2017/18 ambao walianza safari ya kubeba ubingwa mfululizo, Simba walicheza mechi 30 msimu mzima na kufunga mabao 62.

 

2018/19 katika mechi 38, ilifunga mabao 77, huku 2019/20 ikifunga mabao 78 kwenye mechi 38.

Mpaka sasa ikiwa imecheza mechi 31 na kufunga mabao 71, inahitaji kufunga mabao nane tu kwenye mechi tatu zilizobaki ili kuvunja rekodi ya msimu uliopita ambapo itakuwa imecheza mechi chache, lakini imefunga mabao mengi.

 

Kuanzia 2011, ndani ya Ligi Kuu Bara, imeshuhudiwa Simba pekee ndiyo imewahi kubeba ubingwa wa ligi hiyo kwa kufunga mabao zaidi ya 70, huku Yanga ikipambana msimu wa 2015/16 ilipofikisha mabao 70 na kubeba ubingwa kwa kukusanya pointi 73.

 

Ubingwa huu ni furaha kubwa kwa nyota raia wa Ghana, Bernard Morrison ambaye kwa mara ya kwanza anakwenda kubeba Kombe la Ligi Kuu Bara tangu atue hapa nchini kucheza soka ambapo alianzia Yanga, kisha akajiunga na Simba mwanzoni mwa msimu huu.

 

Morrison anaungana na nyota wengine wapya wa Simba kubeba ubingwa huo akiwemo Mugalu, Taddeo Lwanga na Rally Bwalya.

Leave A Reply