The House of Favourite Newspapers

SIMULIZI YA KUSISIMUA: THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 11

0


MTUNZI: Hashim Aziz (Hashpower)
0719401968
ILIPOISHIA:

Ilionesha ni kama wanafahamiana kwa jinsi walivyokuwa wanachangamkiana. Muda mfupi baadaye, meza ilikuwa imejaa vinywaji, kuanzia pombe kali, bia za kawaida na pakti mbili za sigara.

 

Kwa fujo hizo ilionesha kwamba walikuwa na fedha za kutosha, nikawa nashangaashangaa tu.
SASA ENDELEA…

“Unakunywa pombe gani?” aliniuliza yule mwanaume ambaye alikuwa amekaa pembeni yangu. Kwangu mimi alikuwa ndiyo mwenyeji wangu kwani angalau alinionesha roho nzuri tangu aliponikuta katikati ya timbwili na yule konda.

“Fanta orange!” nilisema, wote wakacheka na kugongesheana mikono.

“Unakunywa Fanta kwani wewe mgonjwa? Utatujazia nzi bure hapa! Kunywa hii,” alisema huku akifungua chupa ndogo ya bia yenye rangi ya kijani. Aliifungua kwa kutumia chupa nyingine na kuiweka mbele yangu.

Niseme ukweli kwamba katika maisha yangu sikuwa nimewahi kunywa pombe hata mara moja, kwa hiyo huo ulikuwa mtihani mkubwa kwangu.

“Hiyo wala siyo chungu na haieleweshi, kunywa uchangamke,” alisema huku wenzake wakiendelea kucheka. Nikajikaza kisabuni na kuishika, nikapeleka mdomoni na kupiga funda moja.

 

Ni kweli haikuwa chungu sana kama nilivyokuwa nasikia lakini sikuipenda ladha yake, nikaendelea kujikaza na kumeza.

Ndani ya dakika zisizozidi kumi, walikuwa wameshamaliza pombe zote pale mezani kwani staili yao ya kunywa ilikuwa ni fujo tupu, mtu akishika chupa ya bia haishushi mpaka iishe, wakachangamka sana huku moshi mwingi wa sigara ukinipa wakati mgumu sana.

Mpaka wanamaliza, mimi ya kwangu hata nusu haikuwa imefika, wakainuka na kuniambia niwasubiri hapohapo wanakuja, aliitwa mhudumu mmoja na kukabidhiwa eti anilinde.

“Akimaliza muongezee na akitaka chakula mhudumie, tunakuja sasa hivi,” alisema yule mwenyeji wangu huku akinipigapiga begani, nikawa natingisha kichwa kukubaliana naye.

 

Walipotoka, nilimuomba yule mhudumu anihamishie kule nje kulikokuwa na hewa maana chumba chote kilikuwa kimejaa moshi wa sigara.

Alinisaidia kubeba chupa yangu ya bia, akaenda kuniwekea kwenye meza ambayo haikuwa na mtu, basi watu wakawa wananitazama kwa macho ya wiziwizi huku wakiwa ni kama wananong’onezana jambo.

 

Sikuwajali sana, nilihisi wananitazama jinsi ninavyoinywa ile bia kwani kiumri bado nilikuwa mdogo.

 

Niliendelea kunywa taratibu huku safari hii nikijitahidi kutoonesha ushamba.

Dakika kama tano hivi baadaye, wote tuliokuwa ndani ya baa hiyo tulishtuka baada ya kusikia milio ya risasi, watu wote wakaacha kila walichokuwa wanakifanya, wengine wakainuka harakaharaka na kuanza kuangalia uwezekano wa kukimbia.

Sikuwa nimewahi kusikia milio ya risasi zaidi ya kusikia tu kwa watu wakihadithiana lakini iliposikika tu, nilijua lazima ndiyo risasi hizo nilizokuwa nikisikia tu kwa watu.

 

Ilivyoonesha, milio hiyo haikutoka mbali sana na pale tulipokuwepo.

Muda mfupi baadaye, ukimya ulitawala, kwa mbali likaanza kusikika gari likija kwa kasi kubwa huku muungurumo wake ukiwa mkubwa kama yale magari ya mashindano, kila mtu akawa anatazama barabarani kutaka kutazama ni gari gani lililokuwa linapita kwani ilionesha kuna uhusiano wa gari hilo na milio ya risasi iliyosikika.

Katika hali ambayo iliniacha mdomo wazi, nilishuhudia lile gari tulilokuja nalo likiingiakwa kasi kwenye maegesho ya pale baa tulipokuwa tumekaa. Akashuka yule mwenyeji wangu na kupanda ngazi harakaharaka, akaelekea moja kwa moja kule kwenye kile chumba walichoniacha.

Niligundua kwamba kwa vyovyote atakuwa ananitafuta mimi, basi nikasimama harakaharaka na kumfuata.
“Tuondoke!” alisema huku kijasho chembamba kikiwa kinamtoka. Sikupata hata nafasi ya kumuuliza chochote, nikawa namfuata nyumanyuma akielekea kwa haraka pale kwenye gari, watu wote wakawa kimya kabisa. Alifungua mlango na mimi harakaharaka nikaingia.

Ndani ya sekunde chache tu, alilitoa lile gari kinyumenyume, akafunga breki kali na kuzungusha usukani kwa nguvu, akakanyaga mafuta na kuganya gari liondoke kwa kasi mithili ya yale magari ya mashindano. Wenzake kule nyuma walikuwa kimya kabisa, mara kwa mara wakigeuka kutazama walikotoka.

Mbele kidogo kulikuwa na taa za kuongozea magari na licha ya taa nyekundu kuwaka kuonesha magari yaliyokuwa yakitokea kule tulipokuwepo yanatakiwa kusimama, dereva alicheza ‘faulo’ moja ya hatari ambayo nusura isababishe ajali, akakata kona na kuingia upande wa kulia kwenye barabara ambayo hata sikuwa najua inaelekea wapi, akakanyaga mafuta kwa nguvu na kufanya watu wote walioshuhudia jinsi alivyopita pale kwenye mataa akiwa haamini kilichotokea.

Mwendo aliokuwa akienda nao ulikuwa unatisha kwelikweli, nikajishikilia vizuri kwenye kiti kwa sababu sikuwahi kupanda kwenye gari linaloendeshwa vibaya kama hilo. Ndani ya dakika chache tu, tulikuwa tayari tumefika mbali sana, nje kabisa ya mji.

Mbele kidogo alipunguza mwendo na kukata kuingia kwenye barabara nyembamba upande wa kushoto, safari ikaendelea kwa kasi kubwa na kuishia mbele ya geti kubwa la chuma ambapo alipiga honi mara mbili, likafunguliwa na gari kuingizwa ndani kisha geti likafungwa.

Hakusimama, aliendelea kukanyaga mafuta mpaka kwenye geti la pili ambalo lilifunguliwa, akaingiza gari na kupaki ndani ya kama ‘godauni’ kubwa, tukateremka huku mimi nikigeuka huku na kule kushangaa mandhari ya eneo hilo.
Lilikuwa ni godauni kubwa ambalo ndani yake kulikuwa na watu kadhaa wakifanya kazi za ufundi wa kuchomelea vyuma huku wengine wakiwa bize kutengeneza magari mengi yaliyokuwa ndani ya godauni hilo.

“Twende huku,” alisema yule mwanaume, tukawa tunatembea kwa kasi kuelekea ndani zaidi ya lile godauni. Ni hapo ndipo nilipogundua kwamba wale wanaume walikuwa na begi ambalo hata sikujua ndani yake lina nini lakini katika kumbukumbu za awali, sikuwaona mahali popote wakiwa na begi.

Ndani ya kichwa changu, nilishahisi kwamba begi lile lina uhusiano mkubwa na tukio la kusikika kwa milio ya risasi na ule mwendo tuliokuja nao mpaka ndani ya eneo hilo lililokuwa limezungushiwa ukuta mrefu kwa nje.
“Huyu ni nani na ameingiaje humu ndani?”

“Huyu ni mgeni wa bosi.”

“Mbona sina taarifa zake,” alisema mlinzi aliyekuwa kwenye geti la kutokea kwenye lile godauni upande wa ndani kabisa.

“Hili lipo kwenye mikono yangu, nimeshakwambia ni mgeni wa bosi,” alisema yule mwenyeji wangu kwa sauti ya kibabe, mlinzi ambaye alishaonesha dalili za kutaka kunizuia nisipite, alishusha bunduki yake na kusogea pembeni kutupisha, tukaingia.

Kwa kule ndani, kulikuwa na nyumba kama tatu hivi, zilizojengwa kisasa kama makazi ya watu wenye fedha zao.

 

Yaani usingeweza kuamini kama hapo ni wapi kwa sababu mazingira ya kule nje kabisa ya geti, ndani ya geti, ndani ya godauni na kwenye nyumba hizo, yalikuwa tofauti kabisa.

“Utamweleza bosi kama ulivyonieleza mimi.”

“Kuhusu nini?”
“Kuhusu kazi! Mweleze moja kwa moja, usipindishe maneno,” aliniambia kwa sauti ya kunong’ona wakati tukikaribia kwenye mlango wa vioo wa kuingilia kwenye moja kati ya nyumba zile.

 

Pale nje ya mlango palikuwa na ile mashine maalum inayotumika kukagua watu wanaoingia maeneo yenye ulinzi, kama uwanja wa ndege.

Kulikuwa na wanaume watatu wenye miili mikubwa waliovalia sare maalum ambapo walikuja na vikapu maalum vya plastiki, wakawa wanamsogezea kila mmoja. Kilichotokea kilinishtua mno, kumbe kati ya wale watu tuliotoka nao Gongo la Mboto, ni mimi pekee ndiyo sikuwa na silaha, kila mtu alikuwa na bunduki.

Mwenyeji wangu ndiye aliyekuwa wa kwanza kutoa ya kwake, tena siyo bastola bali bunduki kubwa iliyokuwa imekatwa mtutu na kitako na kuwa fupi. Alinitazama kisha akawa ni kama ananikonyeza hivi, nilishindwa kuelewa anamaanisha nini.

Basi wote walikabidhi silaha zao kisha wakakaguliwa kwa kile kifaa maalum chenye uwezo wa kugundua kama una chuma chochote mwilini, mmoja kati ya wale wanaume akabonyeza namba fulani ukutani na mlango ukafunguka.

Tuliingia ndani ambako kulikuwa na watu wengine kadhaa wakiendelea na kazi zao, huyu yuko bize na kompyuta, mwingine anapekuapekua mafaili, yaani ilikuwa ni ofisi kabisa.

 

Tulipita kwenye ofisi kadhaa, tukatokea kwenye ofisi kubwa yenye vioo kila upande, mlango mkubwa ukafunguka wenyewe na tukaingia mpaka ndani.

Wote waliinama kwa heshima na kusimama kwa kujipanga, yule aliyekuwa amebeba begi akasogea mbele hatua kadhaa na kuliweka juu ya meza kisha akarudi kujipanga kama wenzake, nikawa natetemeka kuliko kawaida.

Kwa muda wote huo, yule mwanaume ambaye bila hata kuuliza nilijua ndiye bosi mwenyewe, alikuwa akihangaika kuwasha sigara kubwa au maarufu kama ciger huku mkononi akiwa anabofyabofya simu yake ya bei mbaya.

Ilipowaka, alivuta na kutoa moshi mwingi kisha akawatazama mmoja baada ya mwingine bila kuzungumza chochote na macho yake yakatua kwangu, akayagandisha huku akiwa ni kama ananishangaa.

Nilimuona yule mwenyeji wangu akimsogelea bosi kwa unyenyekevu, akainama pembeni yake kisha akawa ni kama anamnong’oneza kitu fulani. Nilijua kabisa lazima atakuwa anampa taarifa zangu, naye akawa ananitazama kwa kunikazia macho.

Hakutingishika wala kujibu chochote, baada ya kumalizia kuzungumza naye, alirudi pale alipokuwa amesimama na kujipanga na wenzake, nikaona yule bosi akininyooshea kidole kisha akanipa ishara kama anayeniita.

“Huku nikitetemeka, nilisogea huku nikiwa makini kumtazama. Aliwapa ishara wale wengine wote kutoka, mle ndani tukabaki mimi na yeye tu, akanionesha kwa ishara sehemu ya kukaa, jirani na pale alipokuwa amekaa na ‘kukunja nne’ huku akiendelea kuvuta ‘ciger’.

Kwa zaidi ya dakika tano nzima hakuzungumza chochote zaidi ya kuendelea kuvuta sigara huku akitoa moshi mwingi angani, akawa anabofyabofya simu yake na wakati mwingine akiandikaandika vitu kwenye laptop yake ya kisasa, zile zenye kama alama ya ‘epo’ kwa nyuma, wenyewe wanaziita ‘Mac Book’.

“Unaitwa nani!” aliniuliza kwa sauti nzito ya kukwaruzakwaruza.

“Naitwa Kenny!”
“Bonta ameniambia taarifa zako, unahitaji nikusaidie nini?”

“Naomba kazi bosi, kazi yoyote tu hata ya kufagiafagia bosi, baba yangu anaumwa sana, dawa zake zimemuishia na yeye ndiye pekee tuliyekuwa tunamtegemea, nisaidie bosi nipo tayari kufanya chochote,” nilisema huku machozi yakianza kunitoka.

“Unalia nini sasa? Wewe ni mwanaume unatakiwa kuwa na roho ngumu,” alisema huku akikaa vizuri pale kwenye sofa alilokuwa amekalia, akaendelea kuchezea simu yake huku akinitazama mara mojamoja.

“Baba yako anaumwa nini?”
“Anaumwa sana, madaktari wamesema hawaoni ugonjwa na hivi tunavyoongea amekata kauli, yaani wa leo wa kesho!” nilisema huku nikijisikia uchungu mkali sana ndani ya moyo wangu.

 

Kiukweli nilikuwa nahitaji bosi huyo anionee huruma na kunisaidia.

Je, nini kitafuatia? Usikose kesho hapahapa! Unaweza pia kusoma au kusikiliza hadithi nyingine kwa kuingia:

 

www.simulizizamajonzi7113.blogspot.com , Facebook: Simulizi za Majonzi au Youtube: Hashpower Online.

 

Usisahau kulike, share na ku-subscribe.

Leave A Reply