The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya Kweli ya Gamboshi – 2

0

 

NILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA…

Watu wengi wamekuwa wakisikia habari nyingi kuhusu Gamboshi. Hiki ni kijiji kilichopo wilayani Bariadi katika Mkoa wa Simiyu.

Kijiji hiki kimekuwa kikihusishwa na uchawi na ushirikina huku ikisemekana kuwa kina maajabu mengi sana. Je, ni kweli? ENDELEA…

 

VYOMBO vya habari vimekuwa vikitoa simulizi mbalimbali hasa redio. Mwandishi nguli wa hadithi nchini Tanzania, Eric Shigongo aliwahi kuandika hadithi akitumia jina la kijiji hicho.

 

Kuna wale ambao walikuwa wakihisi kuwa jina hilo ni la kubuni na hakuna kijiji kama hicho.

Lakini mfululizo wa makala hizi utakupa ukweli kuhusu kijiji hiki.

Mwanzoni ilielezwa kuwa kijiji hiki ni nadra mno kutembelewa na viongozi wa Serikali tangu tupate uhuru Desemba 9, 1961.

 

Kama nilivyodokeza wiki iliyopita, kijiji hiki kimepata umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi kikielezwa kuwa ni kitovu cha uchawi na wachawi wanaoweza kufanya miujiza.

Mmoja wa wanakijiji hiki anasema; “Sisi ni wakulima wakarimu wa pamba, mahindi na mpunga. Yote mnayoyasikia kwamba sisi ni magwiji wa uchawi, ni uvumi uliotiwa chumvi nyingi.”

 

Wanakijiji wanadai kuwa, hofu iliyoenezwa ndani na nje ya nchi kuhusu uchawi uliovuka mipaka wa Kijiji cha Gamboshi umesababisha madhara makubwa kwa kijiji chao kiasi cha kutengwa na jamii yote ya Watanzania.

“Hakuna aliyetembelea kijiji hiki kwa miaka mingi sana. Hata sisi tunapotoka nje ya kijiji, wengi hawataki kutusogelea wakiamini tutawadhuru,” anasema mwanakijiji mwingine.

 

Kuhusu viongozi wa Serikali kutofika Gamboshi tangu uhuru mwaka 1961, wanakijiji hao wanasema si kweli kwani Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge aliwahi kufika kijijini hapo.

Kikiwa mafichoni kabisa, kiasi cha kilometa 44 kutoka mjini Bariadi, Kijiji cha Gamboshi si rafiki wa watu wa Kanda ya Ziwa.

 

Mijini na vijijini, kumekuwa na ubishani mkali kuhusu ni mkoa gani unaokimiliki kijiji hicho ambacho baadhi ya wakazi wake wanadai kuwa miongoni mwa vioja vyake ni mauzauza yanayoweza kuifanya Gamboshi iyonekane kama Jiji la New York, Marekani au London, Uingereza wakati wa usiku.

 

Pamoja na umaarufu wake, bado uwepo wa Gamboshi umekuwa ni kitendawili kikubwa.

Mbali na ubishani mkali kuhusu mahali hasa kilipo kijiji hicho cha miujiza, wengi wamekuwa wakidai wakazi wake siyo jamii ya Kisukuma.

 

Wakazi wa Shinyanga wanadai kuwa Gamboshi iko wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza, wakati wale wa Mwanza wakidai kuwa iko mkoani Shinyanga au Simiyu.

Lakini kwa mujibu wa Serikali, Gamboshi ipo wilayani Bariadi, karibu na mpaka unaotenganisha na Wilaya ya Magu.

 

Wanakijiji wa Gamboshi wanasema sifa mbaya ya kijiji hicho imewafanya kutengwa na jamii zingine. Wanakijiji wa Gamboshi ni masikini kwa sababu mkondo wa maendeleo na mageuzi umepita mbali sana nao.

 

Chanzo cha hayo yote ni simulizi ya zamani sana ambapo wenyeji wanasema zamani ilitokea kijana mmoja kutoka kijiji jirani cha Ngasamwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na msichana mzaliwa wa Gamboshi.

 

Siku moja kijana huyo alifika kijijini hapo akimsindikiza mpenzi wake kisha kushindwa kurudi kwao kwa maelezo kwamba alinasa kijijini hapo kichawi.

Juhudi za kumsaka kijana huyo hazikuweza kuzaa matunda, hadi alipoonekana kichakani baada ya siku saba, huku ngozi yake ikiwa imebadilika na kuwa nyeupe.

 

Alipoulizwa alifikaje kichakani hapo, kijana huyo alijibu kuwa ameteremshwa na ndege kutoka Ulaya na baada ya hapo kijana huyo alirukwa na akili na kushindwa kuongea.

Ilibidi achukuliwe na kupelekwa kutibiwa na waganga wa jadi na akapona baada ya matibabu ya zaidi ya mwezi mmoja.

 

Tangu siku hiyo, Gamboshi ikatangaziwa uadui na vijiji vingine kiasi cha kukifanya kuogopwa na kuchukiwa.

Uvumi kama Gamboshi inaweza kuonekana kama Ulaya au Marekani ulianzia hapo na umeendelea na kukifanya kijiji hiki kiitwe jiji la maajabu.

 

Kwa mujibu wa wanakijiji, wangeweza kuitangazia dunia kuwa wao ni wasafi lakini, kwa miaka mingi wamekosa jinsi ya kuifanya sauti yao isikike.

Wapo wanaokiri kuwa Gamboshi ni jiji la manguli wa uchawi na ukifika huko kuna sehemu hawatakuachia ufike au upaone.

 

Itaendelea wiki ijayo.

Msimuliaji: Sifael Paul | 0713 750 910

Leave A Reply