The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya Msamaha wa Mama – 06

0

global-insta

MWANDISHI/MTUNZI SEID BIN SULTAN
NILIONGEA kwa huruma na sauti ya chini kwani tayari nilishahisi kuna kitu nimemkosea mUme wangu na mimi nIlikuwa sipendi nimkosee kwa lolote.

Nilipomuuliza hivyo aliniangalia sana kwa jicho la husuda mpaka niliogopa, alionekana kuwa mtu aliyejawa hasira, aligeuka akanipa mgongo kisha akanambia, “Sihitaji kuzaa kwa sasa…”

Ni jibu ambalo lilinifanya jasho lianze kunitoka kabla hata ya kumuuliza kwa nini, nilihisi tumbo linauma, mwili wote uliishiwa nguvu, nilitoa macho na kumuuliza kwa sauti ya upole.
“Kwa nini hutaki kuzaa?”
“Sihitaji maswali, bali nimekwambia sitaki kuzaa, nielewe mwanamke!” alinijibu hivyo baada ya kumuuliza.

Alitoka akaingia chumbani, nilijaribu kumuita mme wangu lakini hakuitika, nilijua labda ananitania ilibidi nimfuate chumbani, nilimkuta amelala chali miguu chini akiwa hajavua viatu.

Ilikuwa kawaida yangu kila siku kumvua viatu kwa sababu tayari nilishakubali kuwa mjinga kwake ili kulinda ndoa yangu. Niliteremka chini nikiwa katika hali ya unyonge, nikamvua viatu vyake pamoja na soksi, nilisogea na kumuuliza tena, machozi yakiwa yananilengalenga.

“Mume wangu, uko serious kwa ulichoniambia au unanitania?”
“Sihitaji kuongea chochote, niache nipumzike,” alisema kwa mkato.
“Mume wangu hali yangu si nzuri niambie ukweli basi; please ongea chochote kile kingine kizuri, nionee huruma mwenzio. Nilisema kwa sauti iliyokuwa imejaa upole.
“Mwanamke nielewe, sihitaji kuzaa kwa sasa,” alisema.

Niliumia sana kusikia hivyo, kwa mara ya pili machozi yalianza kunitoka kama mtoto, aligeuka na kulalia tumbo nikasikia akisema maneno yaliyonifanya nitake kulia.

“Tena hiyo mimba nataka uitoe haraka iwezekanavyo!”
“Unasemaje Masoud!!?” nilimuuliza kwa mshangao.

“Si matangazo ya vifo!  Umepewa masikio ili kusikia,” alijibu kwa kunikejeli.
“Masoud unanijibu hivyo mimi leo!  Kwa kipi kibaya hasa nilichokufanyia?”

Kuanzia siku hiyo alianza kubadilika, nyumbani alikuwa akirudi muda  anaotaka, ilifika kipindi akawa analala chumba chingine nikimuuliza kwa nini anasema, “Toa mimba!”

“Toa mimba” ndiyo ukawa wimbo uliobakia nyumbani, hakukuwa na salama tena kisa mimba, nikafika sehemu nikachoka maneno yake. Nakumbuka alikuwa anajiandaa kwenda kazini, nikamwambia naomba niende kliniki kuandikisha.

Aligeuka na kuniangalia, akaniuliza nasemaje? Nikarudia tena nilichomwambia, aliniangalia bila kupepesa macho zaid ya sekunde nne kisha akasema.
“Nimesema, toa, hiyo, mimba!”
“Hivi Masoud kwa nini unakuwa hivi mume wangu ee?  Kuna familia inahitaji watoto, kuna wanawake hawajapewa kizazi wanalilia kila siku mtoto, leo mimi nimejaaliwa kupata mimba unasema nitoe kwa nini lakini?  Tena ni ya halali mume wangu hatujazini sisi au ulinioa kwa ajili ya starehe zako binafsi?”
“Yyees nilikuoa kwa ajili ya starehe,” alisema Masoud kwa hasira… na bora ningeoa mgumba kwa sababu sihitaji kuzaa, kwa nini ung’ang’anie wakati staki lakini.?  Sihitaji kuzaa mwanamke, kwani lazima? Usipoitoa hiyo mimba mtafute baba yake mimi sio.”
“Masoud naomba usinifanyie hivyo, kwa nini lakini unanifanyia hivyo mimi, kwani  kitu gani hasa kikubwa kinakufanya hivyo ee?”

Nilianguka chini nikamshika miguu.

Sikuamini kama Masoud anaweza kunipiga siku moja, lakini siku hiyo kudhihirisha kuwa hayuko tayari kuzaa na anaichukia mimba yangu, alinigeukia akanisukuma kitandani na kuanza kunipiga ngumi za tumbo huku akilalamika.

“Kwa nini hunielewi wewe mwanamke, au mpaka nikuue ndo uamini?  Sitaki, sitaki, sitaki, sitaki mpumbavu wewe, sasa kwa kuwa hutaki kutoa ngoja niitoe mimi, alaaaa unanletea upuuzi hapa!”

Kila aliposema  hivyo, alikuwa akinikandika ngumi za tumbo zilizopelekea kuzimia.  Jasho lilikuwa likimtoka, aliniacha bila kujali akaenda kazini, nilipozinduka nilishangaa kuona tumbo linaniuma sana, nilitoka nikaenda hospitalini, daktari alinipima akanipatia dawa na kunishauri nipumzike.
Nilirudi nyumbani nikiwa natokwa na machozi, kibaya zaidi nilikuwa sijui kwa nini Masoud alibadilika kiasi hicho.  Kiukweli niliumia sana, nilihisi dunia ni chungu ndani ya muda mfupi, nilitamani kufa kwa hali niliyokuwa nayo. Bado sikuacha kumjali mume wangu, niliamini ipo siku Mungu atanisaidia na kama mali ndiyo zimemfanya awe hivyo basi atamkumbusha kuwa anakosea, atajirekebisha.

Ulikuwa ni usiku wa tarehe mbili siku ambayo sitoisahau katika maisha yangu, alikuwa ameingia bafuni kuoga, simu yake iliita nikasogea karibu kuiangalia nikakutana na jina Yulaina kwenye skrini.

Nilishtuka kidogo baada ya kuangalia saa nikakuta ni saa tano usiku, nikajiuliza ni nani huyu anayempigia mume wangu usiku wote huu! Nilinyanyua simu nikapokea, nikaweka sikioni kisha nikakaa kimya kusikia ataongea nini.
Moyo wangu ulianza kuuma na kujuta kwa nini nimepokea niliposikia akisema,  “Hello Darling,  how are you?”  Sikuongea chochote nikijua huenda ataongea kitu zaid ya hicho, na kweli baada ya kuona nimekaa kimya akasema.
“Sweet, mbona kimya?  Au uko na hicho kijimwanamke chako?  Kama nlivyokuambia naomba usifanye nacho mapenzi, ikifika asubuhi kabla ya kuingia kazini njoo upate vitu vitamu huku ambavyo hakajawaki kukupatia, si unanijua shughuli yangu?  Habari nzuri ambayo nadhani ni kiunganishi kizuri cha mapenzi yetu ni kwamba nimeenda kupima leo nimeambiwa nina kabebi tumboni natamani uwepo ukashikeshike katumbo kangu!”

Sikuweza kuvumilia, miguu ilishika ganzi nikaishiwa nguvu, nilifanikiwa kuiweka simu kwenye meza nikaanguka chini.

Alipotoka bafuni aliniita huku akinimwagia maji ya baridi, nilishtuka nikalala kitandani, aliniuliza kulikoni nikamwambia hakuna ni mshituko tu, kabla sijamaliza kuongea simu iliingia tena, aliichukua na kutoka nayo sebuleni, ikabidi nami nisogee nisikie atachokiongea.

“Hello beibi!” alisema Masoud.
“Mbona simu yangu ulikata?”
“Acha jokes bhana, mi nilikuwa naoga beibi, nambie!”
“Sina la kukuambia zaidi ya kukuambia tena kesho asubuhi pita uje ukaage katoto kako tumboni nimeenda kupima nina pregnancy!”

“Weeeee!  Sema, hakya-Mungu!.
“Hakya-Mmungu sweet nina mimba yako!”
“Heheheeee!  We mtoto mbona unataka kunifanya nimkimbie huyu mwanamke?  Si kesho, nakuja sasa hivi kukaangalia kabebi kangu, sasa hivi nakuja, sawa mamaa?”
“Haya njoo sweet, nitakuwa na amani zaidi.”
“Niko kwa ajili yako mmmwwaaaa!”

Alikata simu na kuja haraka chumbani, mimi nilimuwahi nikakaa kitandani, alianza kuvaa nikamuuliza andkwenda wapi, akajibu, “Haikuhusu.”
Nilishindwa kuvumilia, nilitoka hadi mlangoni na kumwambia Masoud haendi kokote, alinangalia na kuniambia mara tatu akiomba nimpishe, akaanza kunipiga makofi ya masikio, akanisukuma nikaangukia chini naye akapita na kuondoka zake.

Nilianza kulia kama mtoto, siku hiyo sikujua nililala saa ngapi, aliporudi siku ya pili tayari nilishaandaa chai, nilimkaribisha vizuri kama mtu asiyejua chochote, nikamuuliza kwa kujiamini nikiwa katika hali ya kawaida.
“Mke mwenzangu hajambo?”
“Nini?”  alishangaa sana kumuuliza hivyo.
“Marudio Jumamosi, kama hujasikia limepita karibu unywe chai,” nilimjibu.
Ilibidi nimjibu vibaya siku hiyo kutokana na hasira nilizokuwa nazo kwa sababu nilishaona tayari ninakoelekea ni kubaya, nilijuta kwa nini Masoud alipata mali, kwa kuwa tayari nilishajua kuwa kuna mwanamke mwenzangu ambaye sikujua kama amemwoa au laa, ilibidi nipunguze wivu.  Kibaya zaidi nikajua hayuko tayari kuzaa na mimi ila yupo mwanamke mwengine ambaye yuko tayari kuzaa naye.
Nlipomjibu hivyo aliniuliza.
“Naona una hamu ya kupigwa,  siyo?”
“Nishazoea kupigwa kwa sababu umenigeuza ngoma, kila ukijisikia unapiga tu.”
Aliniangalia kwa jicho baya, aliachia msonyo na kuingia ndani.
“Utasonya sana mwaka huu, nishaujua ukweli wala hunibabaishi, japo naumia lakini nitafanyaje.”
Niliongea kwa kujipa moyo lakini maumivu bado yalikuwa yakinisumbua, machozi yalianza kunitoka upya, nilimimina chai nikajaribu kunywa lakini haikunyweka nikasukumia kikombe mbali kwa hasira.

Kila siku alizidi kunifanya matukio mapya mabaya.  Alizidi kunifanyia mapya, nilikuwa nikienda kupima hospitali kila kukicha, madaktari walinipa ushauri mzuri namshukuru Mungu, kwa kuwa ndiyo ilikuwa mimba yangu ya kwanza nilifatilia ushauri wao mwanzo-mwisho, nilienda kwa wataalam wa ushauri ili kurudisha amani ndani ya ndoa yangu lakini haikuwezekana.  Nilipoenda kwa wazee wake kumbe tayari alishawambia wote  kuwa anataka kuoa mke mwengine ambaye ndiyo mwema kwake na mjanja, walinishambulia kwa maneno tofauti mabaya, nikawa mtu wa kulia kila siku kila kukicha.

Ilikuwa ni siku nyingine tena mbayo sitoisahau katika maisha yangu, nilipokuwa jikoni,  napika jamaa aliniita nami nikaitika, nikaenda sebuleni na kukutana na sura ya mwanamke wa Kiarabu.
Nilimuangalia mwanamke huyo, huku mme wangu akiwa amekaa kwenye kiti anatingisha miguu, nilimsalimia mume wangu na kumkaribisha huyo dada. Kilichonishangaza baada ya kumwambia hivyo alinisonya ‘akanishusha na kunipandisha’, mume wangu alicheka sana,  moja kwa moja nikajua uenda huyo ndiye Yulaina.

“Najma!” aliniita Masoud nami nikaitika.
“Abee,” niliitikia kwa upole.
“Huyu anaitwa Yulaina, mtoto mzuri kuliko wote duniani , mtoto wa Kiarabu, mtoto mwenye hadhi ya kukaa kwenye nyumba nzuri kama hii. Yaani alivyoingia tu na nyumba imecheka kwa sababu ameendana nayo, kama unavyomuona akikaa kwenye sofa anajaa kama jini vile. Heheheee, vipi tumependeza ee!!!” alisema.

Sikuweza kuvumilia, hasira ziliniingia nikamwambia basi inatosha, nilitoka pale na kuingia ndani chumbani,  nikapakia nguo zangu kwenye begi machozi yakiwa yakinitoka, hapo tayari nilikuwa na mimba ya miezi mitano na nusu. Nilitoka ndani hadi sebuleni mwili wangu ukiwa hauna nguvu>  Nilijaribu kufuta machozi yaliyokuwa yanatoka lakini ilishindikana, nikiwa na begi nilimuangalia Masoud nikamwambia,

“Asante sana, nashukuru Masoud, Mungu akuongoze, inshallah atanilipia kwa yote niliyokufanyia kama mke, na hiki kiumbe kilichoko tumboni ipo siku moja utakifuata tu hali ya kuwa hakikutambui, na hicho kiungo kilichoko mwilini mwako kitakutafuna tu.”

Aliniangalia akiwa anacheka, kabla sijatoka nje aliniita na kuniambia.
“Cha kukusaidia tu ngoja nikuandikie talaka zako zote tatu na usahau kuhusu mimi kwa sababu hatuendani, jingine kama hutojali, najua pakuishi patakuwa tabu kidogo kwa sababu huyo mama yako ana kanyumba kana chumba kimoja tu, tena si kanyumba nimekuheshimu, ni  kijibanda,  nakuachia shamba la huko kijijini uishi humo na ni lako hilo nimekupa.

“Ninavyokupenda nakupa na mkataba wake huu hapa, nakupatia bure si langu mimi hilo silitambui ila tu nitakuja kuvuna kila kilichomo ili upande vya kwako, wasalimie uendako siwezi kuwa na mwanamke wa Kiswahili mimi, nahitaji mwanamke anayejua kutumia bhana.

“Mtoto mzuri huyu hapa kwanza kimahaba humshiki, akiwa kitandani anashugulika kweli, si wewe dakika mbili eti mume wangu nimechoka, mashine hii hapa toto kuanzia mwili hadi ladha ni sweet, si wewe unaniita sweet huku hujui kitu.”

“Nashkuru sana Masoud,” nilimjibu.

Hilo ndiyo jibu nililompa baada ya kuniambia aliyoniambia, nilitoka nje na kukutana na kundi la ndugu zake wote, waliniangalia na kuachia kicheko nikapishana nao wakiingia ndani, nilisikia kauli tofauti wakizisema, moja ambayo niliishika mpaka kesho.
“Yamekushinda, ondoka usiwabane wanaoweza kuyahimili.”

Nilitoka na maumivu makubwa  ambayo sitoyasahau hadi kufa kwangu, na hakuna siku nitakayoumia kama siku hiyo katika maisha yangu yote.
Machozi yalizidi kunitiririka wakati wote, nilipofika getini nilikutana na mlinzi wa geti,  tayari naye alikuwa analia kutokana na huruma aliyokuwa ananionea, kwani niliishi naye vizuri na kumchukulia kama ndugu yangu.  Alinikumbatia na kuomba nimpatie namba yangu ya simu, nilimpatia, naye akatoa kiasi cha shilingi laki moja akanipatia, nilishukuru sana.

“Sitoweza kupata bosi aliyekuwa na huruma kama wewe, nitakukumbuka daima, ila konga moyo wanaume ndo tulivyo hasa tukishapata pesa. Nilikuchukulia kama dada’angu wakati ni bosi wangu, nimeshuhudia mengi ukifanyiwa ndani lakini ulivumilia, muda wote nilikuwa nikikuonea huruma bosi unavyoteswa na mumeo, ila ya Waswahili hatimaye yametimia.

Kiukweli nami nahisi sitoweza kuendelea na kazi hapa, bora nikose kibarua kwa ajili yako madam, naomba unisubiri hapo nje niende nimwambie nimeacha kazi ili japo tuongozane nipajue utapoishi kwa sasa, tuendeleze udugu wetu kwa sababu umenisaidia mengi sana ambayo yalinifanya nikuone wewe ni miongoni mwa watu wachache ambao bado wapo katika dunia hii ya sasa.

TUKUTANE SEHEMU YA 07 LEO SAA 2:00 USIKU

Leave A Reply