Siri ushindi wa Lowassa hizi hapa!

lowassaa

Mgombea urais wa Chadema anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.

Neophitius Kyaruzi

MGOMBEA urais wa Chadema anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa ana nafasi ya kuibuka na ushindi wa kiti cha urais iwapo chama hicho kitaongeza juhudi katika mkakati wa kuwafikia wananchi wengi zaidi maeneo ya vijijini katika siku zilizobaki, Uwazi Mizengwe limefahamishwa.

Wachambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, waliliambia gazeti hili kuwa Lowassa ni mwanasiasa mwenye mvuto na ushawishi mkubwa kwa wananchi, hivyo iwapo atatumia vyema siku zilizobaki kuwafikia wananchi wengi zaidi, ana uwezo wa kuibuka mshindi katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Hata hivyo, wanazuoni hao walitoa angalizo kuwa mkakati huo hauwezi kufanikiwa iwapo Chadema itaendelea na mkakati wake wa kutumia usafiri wa helikopta kwa kuwa mgombea wao hatakuwa na fursa pana ya kukutana na wapiga kura.

“Lowassa amekuwa akitumia helikopta katika kampeni lakini ikumbukwe kwamba kwa kutumia usafiri huo, hawezi kuwafikia wananchi wengi kama mgombea anayetumia barabara kwa kuwa Anakutana na wapiga kura wengi zaidi ambao anaweza kuwabadili fikra na mtazamo hatimaye kumuunga mkono,” alisema Mhadhiri wa Kitivo cha Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini.

Pia alisema kuwa Lowassa amekuwa akitumia mkakati wa kuteka saikolojia ya watu kwa ahadi ya kuwaondolea umaskini wananchi hasa akina mama na vijana, mkakati ambao ni muhimu kwa kuwa hilo ndilo kundi kubwa la wapiga kura, hali inayompa taswira ya ushindi kutokana na kuungwa mkono na makundi hayo.

Walisema kwamba iwapo CCM isipowafikia wananchi wengi zaidi na kunadi sera zake na kuwapiga propaganda ili kuwashawishi kuondokana na itikadi za mabadiliko zinazonadiwa na Chadema, inaweza kusababisha chama hicho kikakosa ushindi.

Hata hivyo, walisema kuwa chama hicho kina uwezekano mkubwa wa kushindwa katika uchaguzi huo iwapo mgombea wake (Lowassa), ataendelea na tabia yake ya kutojinadi kwa muda mrefu, kwa kuwa wapiga kura wanamhusisha na magonjwa, jambo ambalo limekuwa likishusha morali ya kumpigia kura katika uchaguzi ujao Wakati huohuo, walisema mkakati wa Chadema wa kueneza propaganda kupitia mitandao ya kijamii unampa Lowassa nafasi kubwa ya kuungwa mkono hasa katika maeneo ya mijini, hivyo anaweza kujikuta akipata kura nyingi katika maeneo hayo ikiwa CCM isipokuwa makini kujibu mashambulizi ya propaganda hizo.

Hata hivyo, wataalam hao walifafanua kuwa CCM ndiyo chama kinachofanya kampeni za uhakika zaidi kutokana na mkakati wake wa kuzunguka nchi nzima kwa kutumia barabara hivyo kitawafikia wapiga kura wengi zaidi kuliko chama chochote cha siasa nchini kinachowania nafasi hiyo.

Walisema kuwa kutokana na mkakati huo, Magufuli ndiye mgombea anayeungwa mkono na watu wengi zaidi nchini na kuongeza kuwa CCM inajiimarisha zaidi siku zilizobaki kuhakikisha kwamba inapata ushindi mnono dhidi ya Chadema.

Waliongeza kwamba CCM imeelekeza zaidi kampeni zake katika maeneo ya vijijini ambako kuna zaidi ya asilimia 70 ya wapiga kura ambao wengi wao si watumiaji wa mitandao ya kijamii. Waliongeza kuwa mtaji mkubwa wa CCM wa wanachama zaidi ya milioni 6, unakipa chama hicho uhakika zaidi wa kuibuka mshindi kutokana na uhamasishaji unaofanyika kuanzia katika kaya hadi ngazi ya taifa.

alifafanua kuwa pamoja na mtaji huo, Magufuli kupitia mikutano yake ya kampeni amekuwa akitumia muda mrefu zaidi kunadi sera za chama chake na kueleweka zaidi kwa wapiga kura kuliko Lowassa ambaye amekuwa akitumia muda mfupi kuzungumza katika mikutano yake.


Loading...

Toa comment