The House of Favourite Newspapers

SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (5)

0

SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (5)

ILIPOISHIA JANA…

 

Mganga alikimbia kama swala, niliona rubega yake ikipepea, nilikimbia kuelekea alikoelekea mganga, lakini kasi ya mganga ilikuwa kali na sikuweza kumpata, alikunja kona zake na mi’ nikakunja zangu. Mwisho kila mtu alimpoteza mwenzake, nikabaki nikikimbia peke yangu.

 

ENDELEA KUISOMA…

 

Niligeuka nyuma kuhakiki kama nilikuwa salama. Mtu wa ajabu aliendelea kunikimbiza na alianza kunikaribia. Nilijawa na hofu, tumaini pekee la kuiona kesho lilibaki katika miguu yangu.

 

Nilifika katika nyumba ambayo ilikuwa wazi. Niliingia humo bila hodi kisha nikaufunga mlango kwa nguvu. Waliokuwamo, wakapiga kelele za hofu. “Mwiziiiiih! Tunakufaaaa…”

 

Sikuyajali makelele yao, nilingoja kuona kama mtu yule wa ajabu angeweza kunifuata katika ficho langu la ghafla. Hakuingia, hapo nikahisi usalama.

 

Watoto wawili wa kike na bibi mmoja wa makamo waliendelea kupiga kelele za kuhitaji msaada. Akili yangu haikufanya kazi kwa kiwango kilichotakiwa. sikuweza kuwatuliza. Niliwatazama wakazidi kuogopa kwa kuhofu nilikuwa mwizi katili.

 

Kilio kile nilichokisindikiza kwa macho kilimwamsha mwanamme pekee aliyeishi pale. Aliuliza kwa hasira, “kuna nini huko!” majibu yalikuwa, “Mwizi! Mwizi! Mwizi!”

 

Mzee akiwa kavaa msuli na baraghashia kichwani, alitoka na  panga la familia. Aliponiona akanirukia, nikakwepa nikijitetea: “Mzee mimi si mtu mbaya, nisikilize nina matatizo mjukuu wako!”

 

Mzee alikuwa mhenga mwema. Alisikia utetezi wangu. Akanitazama usoni kunipima uungwana, hata macho yetu yalipokutana, akanisihi nikakae katika mkeka. Ni katika mkeka huu ndipo alikaa yule bibi mwoga na wajukuu wawili wenye hofu! Wote watatu waliponiona, wakanyanyuka taratibu kisha wakapotelea chumbani kama sisimizi wadogo waingiao katika shimo baada ya saa kadhaa za kuishangaa dunia!

 

Nilibaki na mzee, hata hivyo nilikuwa na hofu isivyo kawaida. Mwenyeji wangu ambaye niliingia katika makazi yake bila hodi, aligundua.

 

“Sakina leta vipande vinne vya mihogo. Vitatu vyangu, kimoja cha mgeni,” mzee aliagiza.

 

Vipande vinne vya mihogo vikiwa katika sahani chakavu, vililetwa. Sakina hakunitazama usoni. Aliniogopa!

 

Mzee alivikamata vipande vyote vitatu. Nilishangazwa na kitendo kile, nikamuona akitabasamu huku akisema, “Kila mwanadamu ana asili ya ubinafsi. Haiwezekani mihogo nilime mimi kisha tule sawa. Tafuna huo mmoja, usiposhiba kunywa maji mengi!”

 

Maneno ya mzee hayakuwa kichekesho, lakini yalitosha kuitwa mzaha uliolenga kuniweka sawa kiakili. Alisema maneno yale akitabasamu. Akili yangu iliyochemshwa kwa mawazo, hofu na woga, ikaanza kupoa.

Itaendelea kesho…

Leave A Reply