The House of Favourite Newspapers

Sitasahau Nilivyokumbana na Jini Mwanaume-16

0

ILIPOISHIA WIKIENDA
Teksi ikaondoka. Hata sikujua ilikuwa inaelekea wapi. Mwili ulinifumka jasho ghafla. Nikajikuta ninatota kama ninayemwagiwa maji.

“Leo naenda kuuawa jamani!” nikawa najiambia kimoyomoyo.
“Kwa nini nimekubali kuingia kwenye hii teksi? Huyu jini ananipeleka wapi sasa?” nikawa najiuliza bila kupata jibu.

Teksi iliendelea kuyoyoma kuelekea mahali nisikokujua.
SASA ENDELEA…

Maneno ya jini huyu aliyoniambia kwamba anaweza kuyaharibu maisha yangu yakawa yananijia akilini mwangu.
Maneno hayo aliniambia jana yake wakati aliponipigia simu usiku nikiwa bandarini nikitokea Zanzibar.
“Mimi naweza kuyaharibu maisha yako mara moja!” jini huyo aliniambia kwa kitisho.

Lakini kwa jinsi maneno hayo yalivyokuwa yakijirudia kichwani mwangu wakati nikiwa ndani ya ile teksi, nilihisi kama vile alikuwa akiniambia wakati ule nikiwa naye ingawa sauti yake haikuwa ikisikika.

Kwa kweli mwili ulinisisimka, nikaogopa sana. Nikainua uso wangu na kumtazama yule Mzungu mara moja tu. Alikuwa akitazama mbele huku akionekana kuwa kwenye mawazo.

Bila shaka alikuwa akiniwazia mimi atakavyokwenda kunishughulikia huko tunakokwenda.
Wakati mawazo yangu yakitangatanga, ghafla simu yangu ikaita. Nikatazama kwenye skirini. Nikaona namba ya dada yangu. Nikaipokea simu haraka.

“Umeonana na huyo mganga?” dada akaniuliza.

Mama yangu wee! Dada ananiuliza kuhusu mganga wakati jini mwenyewe niko naye hapa!
“Sijaonana naye, nimekutana na yule Mzungu amenipakia kwenye teksi.”
“Mzungu gani tena huyo?” Dada akashtuka.

Nikamtazama yule jini usoni, nikaona na yeye alikuwa akinitazama.
Nikavunga. “Si yulee…”
“Yule jini?” dada akaniuliza.

“Ndiyo.”
“Mmekutana wapi?”
“Hukuhuku.”
Nilijua kuwa yule jini alikuwa anasikiliza yale maongezi nikaongea haraka.
“Anasema ananileta nyumbani.”
“Makubwa! Atakuleta nyumbani kweli huyo?”
“Nimpe simu uongee naye?”
“Mh! Haya mpe.”
“Mr Smith ongea na dada,” nikamwambia na kumpa ile simu.
Mzungu huyo akatikisa kichwa.
“Hapana. Siwezi kuongea na mtu,” akaniambia huku macho yake yakitazama mbele.
“Amekataa,” nikamwambia dada.

“Mwambie akuteremshe urudi nyumbani.”
“Mr Smith unaambiwa uniteremshe,” nikamwambia Smith.
Mzungu huyo aliyeonekana kukasirika hakunijibu chochote.

“Mteremshe mdogo wangu arudi nyumbani,” nikamsikia dada akifoka kwenye simu.
Ile sauti aliisikia yule Mzungu lakini alinyamaza kimya.

“Hataki dada, sijui ananipeleka wapi?” nikasema kwenye simu lakini nilijisemea peke yangu kwani simu hiyo ilikata mawasiliano ghafla.

Wakati naitazama ile simu kwa mshangao, yule Mzungu naye alikuwa akinitazama mimi kama aliyekuwa akinisuta kwa macho yake kutokana na kukatika kwa yale mawasiliano. Ilionesha wazi kuwa mawasiliano hayo aliyakata yeye.
Nikadhani dada angepiga tena lakini hakupiga labda alijaribu lakini aliona sipatikani.
Ghafla teksi ikasimama mbele ya hoteli moja.

“Tushuke hapa kwanza tuzungumze, teksi itatusubiri,” Mzungu akaniambia huku akifungua mlango.
Na mimi nikafungua mlango. Tukashuka. “Huyu amenileta hapa hoteli kwa ajili gani?” nikajiuliza.

Mbele ya hoteli kulikuwa na uwanja ambao uliwekwa viti. Mzungu huyo akaniambia:
“Tukae hapa.”
Ilikuwa vyema aliniambia tukae pale. Kama angeniambia anataka kuchukua chumba nisingekubaliana naye.
Tukakaa pale kwenye viti. Mhudumu alipotufuata, Mzungu huyo akaniuliza:
“Unataka nini?”
Nikatikisa kichwa.
“Sitaki kitu.”
“Kunywa japo soda,” akaniambia kisha akaniagizia soda, yeye mwenyewe akaagiza pombe kali.
“Nataka nikwambie kwamba hutaweza kuishi na mwanaume mwingine zaidi yangu,” akaniambia mara tu mhudumu huyo alipoondoka.

“Kama mimi nimeshakupenda wewe huwezi kunikwepa. Mimi nina uwezo wa kukufuata wewe mahali popote ulipo hata kama utakuwa Ulaya. Na usidhani kama kuna mganga hapa Afrika ataweza kuniondoa mimi. Usijidanganye kabisa,” Mzungu huyo aliendelea kuniambia.

Mzungu huyo aliendelea kuniambia maneno mengi ya kunitisha na kutaka nikubali kuwa naye. Mimi nilikuwa nimenyamaza kimya nikimsikiliza.

Kumbe pale simu ilipokata mawasiliano dada alijaribu kunipigia tena lakini hakunipata, akampigia yule mganga na kumueleza kuwa nilitekwa na yule jini wakati nakwenda kwake.

Mganga akataharuki. Baada ya kuzungumza na mashetani yake akamwambia dada ameshapajua mahali nilipo hivyo atakodi teksi kunifuta. Mganga akachukua vifaa vyake akaenda kukodi teksi.

Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda siku ya Jumatatu.

SOCIAL MEDIA ZETU:

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

 

Leave A Reply