STEVE NYERERE AKALIWA KOONI ISHU YA DIMPOZ

Steven Mengere ‘Steve Nyerere’

DAR ES SALAAM: Baada ya hivi karibuni video yake kusambaa mitandaoni akisikika akisema kwamba hana uhakika kama msanii wa Bongo Fleva, Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ atarejea na kuimba vizuri kama zamani kwa kuwa hali yake kiafya si nzuri, mwigizaji Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ amejikuta akikaliwa kooni baada ya mashabiki wa Dimpoz kumjia juu na kumtaka atengue kauli yake kwani haikuwa nzuri.  Kauli hiyo ya Steve aliyoitoa kwa Dimpoz ambaye alikuwa amelazwa nchini Ujerumani akisumbuliwa na tatizo la uvimbe kwenye koo, iliibua mtafaruku wa aina yake ambapo kila mtu aliitafsiri kivyake kutokana na jinsi alivyoielewa.

Kuna baadhi ya mashabiki walimtukana Steve na kumwambia kwamba hakupaswa kuitoa kwani hakuna linaloshindikana chini ya jua. Wengine walimwambia kwamba kutoa kauli hiyo ni sawa na kumkufuru Mungu kwani yeye pekee ndiye mwenye uwezo wa kusema binadamu hataweza kufanya jambo fulani.

“Unaanzaje kusema hataweza wewe ni nani? Watu wengine bwana wanakuwa na kiherehere sana, atubu na asipofanya hivyo tutamtembezea kichapo popote atakapokuwa,” aliandika mmoja wa wadau mtandaoni. Gazeti la Ijumaa lilifanya jitihada za kumtafuta Steve ili alizungumzie suala hilo, ambapo baada ya kupatikana alisema alichokizungumza ni kwamba, Dimpoz atachukua muda kurejea katika gemu tofauti na jinsi watu walivyomtafsiri kwamba hataweza kuimba kamwe.

“Narudia kauli yangu nilisema hivi, atachukua muda kurudi katika gemu, kwa sababu hakuna mtu ambaye hajamuonea huruma Dimpoz wakati anaumwa, wote tulihuzunika, kwanza ni kijana mdogo amepita katika misukosuko mikubwa sana ya kimaradhi kwa hiyo sisi wote kama vijana tulimuonea huruma, ilitupasa sisi kama wasanii wenzake tuungane naye katika kipindi kile alichokuwa anapitia, lakini tunaamini kabisa kwamba itamchukua muda kurudi kwenye gemu na ndiyo kauli niliyosema mimi.

“Ni sawasawa na kocha akuambie kwamba itakuchukua muda kurudi kucheza mpira, kwa hiyo hayo maneno yanayosambaa huko mitandaoni sijui Steve kafanya hivi, sijui kafanya vile hayaniumizi kichwa hata kidogo, sina mamlaka ya kusema kwamba hataimba milele, mimi ni nani?” Alihoji Steve.

Steve alipoulizwa kuhusu mashabiki wa Dimpoz (Timu Dimpoz) ambao wamemtaka kuomba radhi na asipofanya hivyo watamtembezea kichapo popote atakapokuwa, aliwapuuza watu hao.

“Kwanza niseme hawawezi kufanya kitu kama hicho, hatuongozwi na matimu. Tunaongozwa na sheria na Katiba ya nchi, hakuna mamlaka inayoruhusu mwananchi kumtisha mwananchi mwenzake, wajaribu waone, lakini mwisho tu nisema, nisinukuliwe vitu ambavyo sijaongea, narudia tena kusema Dimpoz ni mdogo wangu, ni ndugu yangu ni rafiki yangu ni msanii mwenzangu, tusiziingize chuki, kisa hii mitandao,” alisema.

Dimpoz alirejea nchini hivi karibuni baada ya kufanyiwa upasuaji wa koo kwa takriban mara tatu kwa nyakati tofauti ambapo safari hii yake imeonekana kuimarika na tayari ameachia wimbo wake mpya uitwao Ni Wewe wenye ujumbe wa kumshukuru Mungu.

 

STORI:MEMORISE RICHARD, IJUMAA

Loading...

Toa comment