The House of Favourite Newspapers

Straika mpya ampa jeuri Zahera

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mkongoman, Mwinyi Zahera, amesema kuwa wale wanaoponda ushindi kiduchu wa mabao inaoupata timu yake, watanyamazishwa na straika mpya atakayetua katika usajili wa dirisha dogo.

Dirisha dogo la usajili msimu huu linatarajiwa kufunguliwa Novemba 15, mwaka huu na Mkongoman huyo tayari ametaja nafasi anazotaka kuziongeza ni beki, kiungo, winga na mshambuliaji mmoja pekee.

 

Yanga hadi hivi sasa imefunga mabao 17 huku wapinzani wao Simba wanaoshika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, wakipachika 23 huku Azam FC wanaoongoza ligi wakiwa na mabao 15.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Zahera alisema kuwa katika mechi yeye anachoangalia ni pointi tatu kwa ushindi wowote bila ya kuangalia idadi kubwa ya mabao kama wanayopata watani wake Simba katika michezo yake ya ligi ambayo hayampi hofu.

 

Zahera alisema, straika huyo anayetokea Ghana, atafuta kiu ya mabao ya mashabiki wa Yanga kama wakifikia muafaka mzuri katika kusaini mkataba wa kukubali kutua Yanga katika dirisha dogo.

Aliongeza kuwa, mshambuliaji huyo ni chaguo lake yeye mwenyewe na kabla ya kumsajili atafanya majaribio kwa ajili ya viongozi kumuangalia ili awathibitishie kiwango chake.

“Nimeiona Simba ikipata ushindi wa mabao kumi katika michezo miwili mfululizo waliyoicheza, niwapongeze katika hilo, lakini niwaambie kuwa mimi siangalii ushindi wa mabao zaidi ninachoangalia ni pointi tatu.

 

“Nafahamu wadau wa soka wanaponda ushindi mdogo tunaoendelea kuupata katika michezo yetu, lakini niseme kuwa hayo yote yatanyamazishwa na usajili wangu wa dirisha dogo ambalo nimepanga kumleta mshambuliaji kutoka Ghana ambaye ninaamini anaimudu ligi ya hapa nchini, hivyo atafunga mabao mengi.

“Pia, nitamleta winga kutoka DR Congo ambaye yeye atahusika vizuri katika kumtengenezea mipira ya kufunga mshambuliaji huyo atakayecheza pacha na Makambo (Heritier),” alitamba Zahera.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Comments are closed.