The House of Favourite Newspapers

Straika Simba: Ajibu, Chirwa Wasaliti

Obrey Chirwa

BAADA ya nyota saba wa Yanga wakiwemo Ibrahim Ajibu na Obrey Chirwa juzi hawakuondoka na timu hiyo kwenda Algeria, straika wa zamani wa Simba na Yanga, Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’, amesema wachezaji hao na wenzao ni wasaliti.

 

Nyota hao ‘waligoma’ lakini kwa aina yake wakitoa udhuru kila mtu kwa mtindo wake lakini nyuma ya pazia ikielezwa wanagoma wakishinikiza walipwe malimbikizo ya mishahara yao.

Ibrahim Ajibu (katikati).

Yanga juzi iliondoka kwenda Algeria ambako kesho Jumapili itacheza na USM Alger mechi ya Kundi D ya Kombe la Shirikisho Afrika.

 

Wachezaji ambao hawajaondoka na timu ni Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Obrey Chirwa, Papy Kabamba Tshishimbi, Ibrahin Ajibu, Thabani Kamusoko na Beno Kakolanya.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Mogella alisema kuwa wachezaji hao ni wasaliti kwani walipaswa kutanguliza maslahi ya nchi halafu mambo mengine yangefuata baadaye.

 

“Klabu zinapaswa kuwa makini kutimiza mahitaji ya wachezaji hao kama walikubaliana jambo fulani liwe hivi basi watekeleze na si vinginevyo kama haya yanayotokea kwa Yanga.

 

“Lakini wachezaji wa Yanga nao ni wasaliti sababu walitakiwa kutanguliza mbele maslahi ya klabu kwanza ukiangalia wachezaji ambao hawajaondoka na timu ni wale ambao ni tegemeo,” alisema Mogella.

 

Naye straika wa zamani wa Yanga, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ alisema: “Wachezaji wa sasa wanatakiwa kubadilika sababu wamekuwa wakitanguliza maslahi mbele kuliko kazi kama ilivyokuwa zamani.”

 

JULIO NAYE ATEMA CHECHE

Kocha wa Dodoma FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amesema licha ya Yanga kutokuwa na nyota wake kama Ajibu na Chirwa, timu hiyo inaweza kuifunga USM Alger kesho Jumapili.

 

Julio alisema Yanga wanaweza kushinda mechi hiyo lakini wachezaji waliogoma kwenda Algeria ni lazima waadhibiwe.

 

“Naamini kama vijana walioondoka na timu wakijituma Yanga itashinda kwani hata kama wangeenda wachezaji wa Ndanda (FC) wangeshinda kama wana nia, wapambane tu watashinda.

 

“Kama Yanga ikifungwa huko Algeria kwa upuuzi wa wachezaji hawa waliogoma basi wote wafukuzwe na wapewe adhabu kwani hawafai na ni wasaliti kwani Yanga inawakilisha nchi,” alisema Julio.

 

“Fedha zinatafutwa utapata utatumia zitaisha sasa umesusa na tukitolewa kama nchi itakuwa ni kwa sababu ya ujinga wao waliogoma,” alisema Julio.

Comments are closed.