The House of Favourite Newspapers

Sugu Alivyogoma Kusoma Hotuba ya Upinzani Bungeni

Msemaji wa Kambi rasmi ya upinzani Bungeni katika Wizara ya Habari Joseph Mbilinyi (Sugu) amegoma kuendelea kusoma hotuba yake Bungeni kwa madai kuwa zaidi ya 80% ya maneno yameondolewa katika hotuba yake kuhusu bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/20.

 

Sugu amelazimika kuchukua uamuzi huo leo Alhamisi Aprili 18, bungeni jijini Dodoma, baada ya Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson kumtaka asisome baadhi ya maeneo yaliyoko katika hotuba yake. Kwa mujibu wa Dk. Tulia, hotuba aliyotaka kusoma Sugu ilikuwa na mambo yaliyoondolewa baada ya kuonekana yanakiuka kanuni za kudumu za Bunge.

 

Kabla ya Sugu kuchukua uamuzi huo, alianza kusoma hotuba kupitia katika kitabu alichokuwa nacho lakini baada ya muda mfupi tangu alipoanza kusoma, Dk Tulia alimtaka asiisome bali asome kupitia kitabu kipya cha hotuba yake ambacho wabunge wote walikuwa wamegawiwa.

 

Kutokana na maelekezo hayo,Sugu alisema hawezi kufanya hivyo kwani kitabu kipya hakina maoni ya kambi yake na hivyo kulazimika kuondoka mbele ya Bunge na kurudi katika kiti chake. Baada ya kusema hayo Naibu Spika aliruhusu mjadala wa bajeti hiyo uanze huku akisema hotuba ya Sugu isiingizwe katika kumbukumbu za Bunge kwa kuwa Sugu hakusema kama anataka iingizwe katika kumbukumbu hiyo.

SPIKA ALIVYOULIZA – “Kwanini MIREMBE Imejengwa DODOMA?”

Comments are closed.