The House of Favourite Newspapers

Sugu: Mhe. Rais Ninakuunga Mkono Mpaka Mwisho! – Video

MBUNGE wa Mbeya Mjini (CHADEMA), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’,  amesema yapo baadhi ya mambo ambayo viongozi wa upinzani humuunga mkono Rais John Magufuli lakini huwa haambiwi na badala yake huambiwa yale ya kupinga pekee na kusema yuko tayari kutumika katika kuondoa mapungufu ya kisiasa yaliyopo katika Mkoa wa Mbeya na hata kitaifa.

 

Sugu amesema hayo hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Ruanda, Nzovwe, jijini Mbeya leo Aprili 26, 2019 na kusema suala la vitambulisho vya machinga alivyovitoa rais analiunga mkono kwa asilimia 100 huku akibainisha kuwa yapo mambo mengine wanayomuunga mkono. 

 

“Mheshimiwa naibu Spika (Tulia Ackson) alizungumza na kusema yeye na wamachinga wenzake, ila hata mimi ni mmachinga,  niliuza mitumba katika Soko la Mwanjelwa baada ya kumaliza kidato cha nne, kabla ya sijaingia kwenye muziki na nilikuwa naona shida zile.

 

“Nilifurahi baada ya kusikia kuwa wamachinga wasibughudhiwe kwa sababu ndiyo mfumo wao wa ufanyaji biashara, hata Jengo la Machinga Complex limeshindwa kwa sababu ni ngumu kuwaweka wamachinga pamoja na badala yake wao ni watu wa kuzunguka tu,” na kusisitiza kwamba hawampingi rais katika kila kitu bali wanaowajibika kumwambia wanamficha ukweli huo.

 

Amesema wafanyabiashara wa jiji la Mbeya pia wamekuwa wakilalamikia kodi na tozo nyingi huku Mamlaka ya Mapato wakishindwa kuweka utaratibu rafiki wa ukusanyaji kodi.

 

“Siyo kila mtu anaweza kuwa na utaalamu wa kodi, badala yake wawape elimu ili walipe kodi kwa hiari bila kushurutishwa,” alisema na kuongeza kwamba  Sh70 bilioni zinahitajika ili kumaliza tatizo la maji katika Jiji la Mbeya ambapo chanzo chake  ni Mto Kiwila.

 

MSIKIE SUGU AKIZUNGUMA HAPA

Comments are closed.