The House of Favourite Newspapers

Timu za Manchester Zimerejea Nafasi Zao

0
Wachezaji wa Manchester Utd wakishangilia.

 

TIMU za jiji la Manchester zimeendelea kutawala kwenye Ligi Kuu England mwanzoni tu mwa msimu huu.

Hii ni kasi ya ajabu tofauti na hali ilivyokuwa msimu uliopita ambapo timu hizo zote zilishindwa kufanya vizuri.

Manchester United msimu uliopita walimaliza msimu wakiwa nafasi ya tano, lakini wakapata nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Europa.

Huku Manchester City wenyewe wakimaliza kwenye nafasi ya tatu, lakini walitakiwa kusubiri hadi mchezo wa mwisho kujua kama wana tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu au la.

Hii imewafanya wote wawili waamke na sasa kila timu inaonyesha kiwango cha juu kuhakikisha kuwa matatizo ya msimu uliopita hayawezi kujirudia tena msimu huu.

Makocha wa timu zote mbili ni wazoefu na wabishi kwenye soka duniani, wakiwa walikutana kwenye Ligi Kuu ya Hispania, Jose Mourinho akiwa na Mabingwa wa Dunia Real Madrid, na Guardiola akiwa na Barcelona ambazo ni timu pinzani nchini Hispania, lakini sasa wamekutana tena wakiwa na timu pinzani nchini England.

Wote ni wazoefu wa kutwaa makombe na ukitaka kuzungumzia mafanikio kwenye soka duniani basi utafanya kosa kama hutawataja wawili hawa.

Wachezaji wa Manchester City.

Guardiola amefanikiwa kwa kiwango kikubwa akiwa ametwaa makombe yote makubwa ngazi ya klabu, huku Mourinho naye akiwa na mafanikio makubwa sana kwenye ngazi hiyo lakini kabati lake likiwa na makombe yote makubwa.

Kwa sasa timu zao wote ndiyo zipo kileleni kwenye Ligi Kuu England, Manchester City wapo juu wakiwa na pointi 13 baada ya kucheza michezo mitano.

Katika michezo hiyo timu zote mbili zimelingana kwenye kila kitu, United wanashika nafasi ya pili nao wakiwa na pointi 13, sawa na City.

Lakini kuonyesha kuwa makocha hao kwa sasa wanataka kutikisa kwenye Ligi Kuu England kama walivyofanya wakiwa pamoja kule Hispania, wamelingana pia kwenye mabao ya kufunga ambapo wote wamefunga mabao 16.

 

Mbali na kufunga mabao sawa ndani ya michezo hiyo mitano, wanaume hao wamefungwa pia mabao mawili kila mmoja, huku wakiwa wametoka sare moja na wakiwa hawajapoteza mchezo wowote.

Hali hii inaonyesha kuwa huu utakuwa msimu muhimu kwa timu hizo mbili ambazo zipo kwenye jiji la Manchester, ambazo zilikuwa zikitawala ulimwengu wa soka kwa miaka kadhaa iliyopita na baadaye zikaanza kupotea.

Tofauti na msimu uliopita Manchester United walikuwa wakimtegemea staa wao, Zlatan Ibrahimovic kwenye chati ya ufungaji ambapo alimaliza msimu akiwa amefunga mabao 17 kwenye ligi.

Kwa sasa wamekuwa tofauti wanamtegemea Mbelgiji, Romelu Lukaku, ambaye kwenye michezo mitano tu ameshapachika mabao matano wavuni, ajabu ni kwamba msimu uliopita City walikuwa wakimtegemea Sergio Kun Aguero ambaye alimaliza akiwa amepachika mabao 20 kwenye ligi, lakini kwa sasa ndani ya michezo mitano naye amelingana na Lukaku kwa kila mmoja kupachika mabao matano kwenye ligi hiyo wakiwa wanatawala kileleni Lukaku akiwa juu.

Hii ni picha halisi kuwa baada ya michezo mitano tu United na City wanalingana kwenye kila takwimu muhimu kwenye ligi hiyo.

Vita ya timu hizi inaonyesha kuwa zenyewe zipo mbali sana na timu nyingine kwenye ligi hiyo, kwani wakati wenyewe wakiwa na pointi 13 timu inayofuata kwenye nafasi ya tatu ina pointi 10, ikiwa ina tofauti ya mabao nane dhidi ya timu hizo vinara.

Inawezakana huu ukawa mwanzo mpya mwa timu hizo za jiji la Manchester kurejea tena kwenye kasi yao na kuwaacha kwenye mataa wagumu wa London ambao kupitia kwa timu yao ya Chelsea walitwaa ubingwa wa England msimu uliopita.

Leave A Reply