The House of Favourite Newspapers

Binti Mkulima Ashtua Bongo!

KWENYE mitandao ya kijamii Bongo, kuna binti maarufu aitwaye Nicole Joyce Mbaga (26) ambaye anadaiwa kuwa mkulima anayeishi ‘kama malaika’ kutokana na kufuru za kipesa anazozifanya. Gazeti la Ijumaa lina habari yake.

 

DOLA NA MAGARI YA KIFAHARI

Mbali na kuonekana na ‘mavibunda’ ya dola za nchi mbalimbali hasa za Kimarekani, pia anaonekana akibadilisha magari ya kifahari, kuvaa nguo, mikufu na kubeba mikoba ya bei mbaya yenye majina makubwa duniani.

 

AIBUA MASWALI MAGUMU

Katika hali kama hiyo huku wengine wakilia njaa, Nicole mwenye umbo namba nane na ‘mzigo mkubwa nyuma’, ameibua maswali magumu miongoni mwa wafuasi wake mitandaoni.

Miongoni mwa maswali yanayoulizwa ni pamoja na mwanadada huyo anapata wapi jeuri hiyo katika kipindi hiki ambacho watu wanaamini ni kigumu kipesa?

 

IJUMAA LAZAMA MTAANI

Hapo ndipo Gazeti la Ijumaa lilipolazimika kuzama mtaani na kwenye vyanzo vyake kujua huyu Nicole hasa ni nani?

Katika nusanusa zake, Ijumaa limeibuka na wasifu wa Nicole ambaye ni mwenyeji wa mkoa wa Iringa.

 

GUMZO MJINI

Nicole kwa sasa ni gumzo mjini kutokana na bata anazokula kwenye hoteli za kifahari maeneo mbalimbali ndani na nje ya Bongo huku akitamba kwamba ana uwezo wa kwenda kula bata ndefu kwenye nchi yoyote anayoitaka hapa duniani.

Wanaomjua wanadai kuwa Nicole ni Mpare kwa kabila na alizaliwa mwaka 1993 huko Iringa nchini Tanzania.

Alikulia mkoani Iringa na Mbeya kabla ya kuhamia jijini Dar kimasomo na baadaye nchini Malaysia kwa elimu ya chuo kikuu.

MKULIMA WA MATIKITI

Pia wanasema Nicole amekuwa akijinasibu kuwa kazi inayompa jeuri ya kufanya kufuru zote hapa duniani ni kilimo cha matikiti anachokifanya katika Vijiji vya Kiwele na Pawaga mkoani Iringa.

“Kuna watu hawaamini kama kilimo anachofanya Nicole cha matikiti kuwa hakiwezi kuwatoa kimaisha, lakini habari ndiyo hiyo,” alisema Kase, mmoja wa watu wanaomjua Nicole na kuongeza;

“Watu wengi wanajua si Mbongo, lakini mimi namjua, ni mwenyeji wa Iringa.”

 

MADAI NA ESSIEN WA CHELSEA

‘Infomesheni’ nyingine zilizopatikana kuhusu Nicole ni kuwepo kwa madai mazito (hatujayathibitisha) kuwa aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na staa wa soka duniani kutoka nchini Ghana, Michael Essien.

Essien amechezea timu kubwa duniani kama Bastia, Lyon, Chelsea, Real Madrid, Milan, Panathinaikos, Persib Bandung na sasa anakipiga katika timu ya Sabail ya nchini Azerbaijan katikati ya Bara la Ulaya na Asia.

 

Inasemekana wakati anatoka na Nicole, Essien alikuwa akikipiga kwenye timu ya Chelsea ya Uingereza.

Ilidaiwa kuwa, akiwa na jamaa huyo, ndipo Nicole alipopata shavu kubwa la matangazo ya Kampuni ya Nike kabla ya uhusiano wa kimapenzi kufikia ukingoni na kurejea Bongo kisha kuwekeza kwenye kilimo.

 

AACHA KAZI YA BENKI AKALIME

Pia inaelezwa kwamba, Nicole ni msomi wa masuala ya benki ambaye baada ya kumaliza masomo aliajiriwa benki, lakini aliamua kuacha kazi hiyo na kugeukia kwenye kilimo kwa maelezo kuwa kinalipa zaidi kuliko kazi ya kuajiriwa.

 

AKATAA KUWA VIDEO QUEEN

Inasemekana kwamba, kutokana na urembo na umbo lake matata, Nicole amekuwa akifuatwa na kuombwa auze sura (awe video queen) kwenye video za muziki, kuigiza filamu au umodo, lakini amekuwa akidai kuwa hazilipi.

 

PASIPOTI YA KIDIPLOMASIA

Kwenye ukurasa wake wa Instagram, Nicole alitupia picha akionesha pasipoti zake za kusafiria ikiwepo ya kidiplomasia na kuibua gumzo kama lote kwani pasi hizo hutumiwa na watu wa diplomasia na viongozi wakubwa.

 

MAGARI MAKALI

Nicole ambaye amekuwa akitupia picha akilindwa ile mbaya na askari mwenye bunduki, amekuwa akionekana na magari tofauti kama Range Rover Sport, BMW, Benz, Porsche 911 na mengineyo makalimakali.

 

AJIACHIA DUBAI

Nicole amekuwa akitupia picha kibao akila bata sehemu mbalimbali ikiwemo The Dubai Mall huko Dubai kwenye Falme za Kiarabu akipiga shisha na pombe za bei mbaya.

 

ASEMA HAJIUZI

Katika mahojiano na runinga moja ya mtandaoni, Nicole anasema kwamba mambo hayo yote anaweza kuyafanya kutokana na pesa nyingi anazotengeneza kupitia kilimo na si kweli kwamba anajiuza kwani hakuna mwanaume mwenye uwezo wa kumnunua kutokana na kiasi kikubwa cha pesa alizonazo.

“Hawana pesa za kunilipa,” alisema Nicole anayezungumza Kiswahili kilichonyooka na kuweka sawa kwamba kwa sasa yupo ‘singo’.

 

Stori: Waandishi Wetu, Dar

Comments are closed.