The House of Favourite Newspapers

Taasisi za Umma 19 Zapata Hati Zenye Mashaka – Video

0

TAASISI 19 za umma kati ya taasisi 999 zilizofanyiwa ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) katika mwaka mwaka wa fedha 2020/2021 zimepata hati zenye mashaka.

 

Hayo yamesemwa leo Jumatano Machi 30, 2021 na CAG, Charles Kichere wakati akiwasilisha ripoti ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2021 kwa Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu Chamwino.

 

Amesema katika mwaka 2020/21 amefanya kaguzi maalumu 56, kaguzi 37 zikiwa za mamlaka za Serikali za Mitaa, 12 Serikali kuu na sita mashirika ya umma na moja ya mifumo ya Tehama.

 

“Katika mwaka 2020/21 nimetoa jumla ya hati 999 za ukaguzi, kati ya hizo, hati 185 za mamlaka za Serikali za Mitaa, 195 mashirika ya umma, hati 308 serikali kuu, hati 19 vyama vya siasa, hati 292 miradi ya maendeleo,” amesema.

 

Amesema kati ya hati 999 nilizotoa, hati zinazoridhisha ni 970, sawa na asilimia 97.1, hati zenye mashaka ni 19, sawa na asilimia 1.9, hati mbaya ni sita na nilitoa hati 4 za kushindwa kutoa maoni. Amesema hati mbaya na mashaka zimepungua katika ukaguzi huo ikilinganishwa na mwaka jana.

 

Kichere amesema kuna ongezeko la hati safi kutoka asilimia 89 kwa mwaka jana hadi asilimia 98.01 mwaka 2020/2021.

Amezitaja taasisi zilizopata hati zenye mashaka kuwa ni Jiji la zamani la Dar es Salaam, Halmashauri za Wilaya ya Kisarawe (Pwani), Longido (Arusha), Mlele (Rukwa), Musoma (Mara), Sengerema (Mwanza) na Bunda (Mara).

 

Kichere amesema kwa upande wa mashirika ya umma, taasisi zilizopata hati yenye mashaka ni Mamlaka ya Maji na Ustawi wa Mazingira Geita, Muleba, Ngara (Kagera), Tabora, Taasisi ya Mifupa Muhimbili na Mamlaka ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

 

Nyingine ni Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN).

Amesema Shirika la Masoko Kariakoo na Shirika la Reli Tanzania walishindwa kutoa maoni katika ukaguzi huo.

CUF yapata hati yenye mashaka

Kichere amesema vyama vinne vimepata hati mbaya, vitatu hati yenye mashaka na viwili walishindwa kutoa maoni.

Amevitaja vyama hivyo vilivyopata hati mbaya katika ukaguzi huo ni ADC, Chaumma, UMD na TLP huku vyama vya CUF, UDP, SAU vikipata hati zenye mashaka.

Kichere amesema chama cha Demokrasia Makini na AFP walishindwa kutoa maoni katika ukaguzi huo.

Leave A Reply