The House of Favourite Newspapers

Tamasha la Pasaka Latarajiwa Kuwa Na Ubora Wa Hali Ya Juu Mwaka Huu

0

Dar er Salaam: 1 Aprili 2023. Kuelekea Tamasha kubwa la Pasaka linalotarajiwa kufanyika katika Viwanja vya Leaders Club vilivyopo Kinondoni jijini Dar, Aprili 9 mwaka huu tamasha linatarajiwa kuwa na ubora wa hali ya juu ikiwa ni pamoja na maombi ya kuliombea taifa  la Tanzania ambapo watu wote wanakaribishwa kuhudhuria.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Msama Promotion Waandaaji wa tamasha hilo, Alex Msama amesema tamasha hilo litakuwa na ubora wa hali ya juu kulinganisha na matamasha mengine yaliyowahi kupita kwa sababu ya kuwa kimya kwa kipindi kirefu.

Msama amesema katika tamasha hilo waimbaji wake wote wako kwenye maandalizi na kuongeza kuwa kutakuwa na maombi maalumu ya kumuombea Rais wetu. Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka miwili  kwa kufanya kazi kubwa ya kuliongoza taifa.

Msama aliendelea kusema;

“Mgeni rasmi tulitegemea angekuwa ni Mama yetu Dk. Samia Suluhu Hassan lakini kutokana na majukumu ya kuliongoza taifa Waziri wetu wa Habari, Nnape Nnauye ndiye atakayemuawakilisha na kutakuwa na maombi ya kumshukuru Mungu kwa miaka miwili ambayo Rais wetu huyo ametuongoza vyema na kwa mafanikio makubwa.

 

Waziri wa Habari, Nnape Nnauye

“Naendelea kusisitiza kuwa hakuna kiingilio itakuwa ni bure na usalama wa hali ya juu kwa watu na mali zao na kuwaomba wananchi kuja kufurika kwenye tamasha hilo ili wajionee burudani hiyo itakayoacha gumzo.

“Katika kipindi hiki cha Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan tumeona mambo mengi yanaenda vizuri sana hivyo nasi tumeamua kuandaa tamasha hili kubwa na la aina yake ndio maana kutakuwa na wasanii wakubwa ambao wanafanya vizuri katika muziki wa injili.

Baadhi ya wasanii hao kutoka nje ya nchi ni pamoja na Masi Masilia kutoka Congo Faustine Munishi kutoka Kenya, Tumaini Akilimali kutoka Kenya, Joshua Ngoma kutoka Rwanda, Nicole Ngabo kutoka Congo.

Na kutoka hapa nchini miongoni mwa watakaokuwepo ni Upendo Nkone, Abwene Mwasongwe na wengine wengi.” Alimaliza kusema Msama.

Leave A Reply