The House of Favourite Newspapers

Tambwe tena akutwa na mkasa

0

AMISSI TAMBWEMshambuliaji wa Yanga, Hamis Tambwe.

Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Hamis Tambwe, amekumbwa na mkasa mwingine baada ya kukabwa koo kwa mara ya pili kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Majimaji Alhamisi Iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Tambwe alikumbwa na mkasa huo tena Januari 17, mwaka jana, wakati timu yake ya Yanga ilipovaana na Ruvu Shooting kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara katika uwanja huohuo.
Beki wa Ruvu Shooting, George Michael ‘Beki Katili’, ndiye alimkaba mshambuliaji huyo raia wa Burundi mwaka jana, lakini ikiwa umepita mwaka mmoja tu mchezaji huyo amekabwa tena na beki wa Majimaji, Sadiq Gawaza kwenye Januari 21, mwaka huu.
Katika mchezo wa Alhamisi iliyopita, Yanga walipata ushindi wa mabao 5-0 huku staa huyo akifunga mabao matatu na kuendelea kukaa kileleni kwenye ligi hiyo ambayo itafikia ukingoni Mei, mwaka huu.
Gazeti bora kabisa la michezo hapa nchini Championi, ndilo lililoibua tukio la kukabwa koo kwa Tambwe mwaka jana na sasa linaibua tena tukio la mchezaji huyo ambaye anaongoza kwa mabao kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na mabao 13.
Tukio hili linakuwa la pili kwa mchezaji huyo ambaye amekuwa bora kwa kipindi chote alichokaa kwenye ligi hii, akiwa ameitumikia timu ya Simba na Yanga kwa vipindi tofauti.
Inaonekana kama vile hii imekuwa kama njia pekee ambayo mabeki nchini wanaona wanaweza kuitumia ili kumdhibiti staa huyo mwenye uwezo wa kufunga mabao kwa kichwa, mguu wa kushoto pamoja na kulia.
Katika tukio la mwaka jana, Tambwe pia alipigwa ngumi, viwiko na kupasuliwa mdomo, pia akavimba jicho la kulia.
Alipokabwa mwaka jana, Tambwe alisema: “Sijawahi kutamka hata siku moja, lakini leo ninatamka kuwa soka la hapa nchini hivi sasa ni vita na siyo burudani tena, haiwezekani mchezaji anacheza soka huku akirusha ngumi, viwiko na mateke uwanjani huku mwamuzi akiangalia tu bila ya kutoa maamuzi yoyote.”

Leave A Reply