The House of Favourite Newspapers

Tanga: Kijana Akatwa Jembe Shingoni, Auawa

0

MTU mmoja aliyekuwa akifanya kibarua cha kulima, Fadhili Rashidi (35), ameuawa kwa kukatwa na jembe shingoni.

 

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana katika kitongoji cha Mgombezi, kijiji cha Mafere, kata ya Mkuzi wilayani Muheza ambako alikuwa anaishi.

 

Ofisa mtendaji wa kata ya Mkuzi, wilayani Muheza, Japhet Hayule, alisema mtuhumiwa wa mauaji hayo ni Joseph Lukas, ambaye alikuwa akiishi nyumba moja na marehemu, wote wakiwa wanafanya vibarua vya kulima.

 

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mgombezi, Athumani Hamisi, alisema vibarua hao, mtuhumiwa na (marehemu) walipita nyumbani kwake saa saba usiku wakiwa wameongozana wakienda wanakoishi huku wakiwa wamelewa, lakini walikuwa wakigombana kwa kudaiana Sh. 20,000.

 

Aliongeza kwamba asubuhi walipata taarifa juu ya tukio hilo na yeye alitoa taarifa kwa mtendaji wa kijiji, Victoria Masanja, ambaye naye alitoa taarifa kwa mtendaji wa kata ya Mkuzi, Japhet Hayule.

 

Kufuatia tukio hilo jeshi la polisi wilayani Muheza linawashikilia watu watatu kutoka eneo hilo kwa uchunguzi zaidi ambao ni Lukas, Abdallah Shabani na Shabani Athumani.

 

Kaimu mkuu wa upelelezi wa polisi wilayani  humo, aliyeomba jina lake lisitajwe, aliwataka wananchi kutofumbia macho matukio kama hayo na kwamba wakiwaona watu hawaeleweki wanajihusisha katika matumizi ya dawa za kulevya ikiwamo mirungi, bangi na pombe haramu ya gongo watoe taarifa kwa viongozi wao kwa kuwa hiyo ndiyo inaleta watu kufanya mauaji.

 

Alisema jshi hilo litaanza msako katika vijiji vyote wilayani humo kwa ajili kukamata madawa ya kulevya ikiwamo bangi, mirungi, pombe ya gongo huku akiwataka maofisa watendaji kuwafichua vijana wanajihusisha na vitendo hivyo wakamatwe.

 

Mwenyekiti wa kijiji cha Mafere, kata ya Mkuzi wilayani humo,  Haji Athumani, alisema vijana ndiyo wako mstari wa mbele kwa kutumia madawa ya kulevya.

Leave A Reply