The House of Favourite Newspapers

Tanzania Mwenyeji Shindano La Binti Afrika 2024 Warembo Toka Nchi Za Afrika Kuchuana

0
Mkurugenzi Mtendaji wa KL International Agency, Alphonce Mkama (katikati) akizungumza kwenye mkutano na wanahabari uliofanyika Hoteli ya Kingazi Resort iliyopo Kijichi Mgeni Nani. Kulia ni Mkurugenzi wa hoteli hiyo, Nelson Mahenge na kushoto ni binti wa mfano wa shindano hilo, Irene Luhwago.  

Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa shindano la Binti Afrika linalotarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini ambapo imeelezwa kuwa lengo kuu la shindano hilo ni kukuza lugha ya Kiswahili na kuutangaza Utu wa Mwafrika.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mkurugenzi Mtendaji wa KL International Agency, Alphonce Mkama, amesema shindano hilo linakuja kukuza lugha ya Kiswahili, kutangaza Utu wa Mwafrika lakini pia ni shindano ambalo linakuja kuwaambia mabinti zetu urembo si kujikondesha inachotakiwa ni kuwa na miili yao ya asilia.

Mkurugenzi Mtendaji wa KL International Agency, Alphonce Mkama (kushoto) na Mkurugenzi wa Hoteli Kingazi Resort, Nelson Mahenge wakibadilisha mikataba baada ya kutiliana saini kushirikiana katika kufanikisha shindano hilo.

“Katika kuungana na Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha lugha ya kiswahili inakuwa zaidi na sisi kupitia Binti Afrika tunakwenda kutangaza lugha ya kiswahili na hapa Hoteli ya Kingazi Resort jijini Dar es Salaam ndipo washiriki wataweka kambi na kufanya mazoezi mbalimbali ikiwemo kutembea kwa mikogo na mengineyo.

“Shindano hili linahitaji mabinti wenye maumbo makubwa na wenye nywele za asili na wenye ngozi ya asili wasiojichubua na ambapo mabinti kutoka nchi zaidi ya 30 barani Afrika wanatarajia kuja kuchuana siku hiyo hapa Hoteli ya Kingazi Resort ambapo wiki ijayo kutakuwa na tukio la kuwatambulisha mawakala wa shindano hilo katika nchi zinazoshiriki.

“Kambi itachukua miezi minne ili kutoa fursa kwa wageni kufundishwa lugha ya kiswahili kupitia wakufunzi mbalimbali kutoa vyuo vyetu vikuu, Bakita na Bakiza kuja kukutana na washiriki wetu kuja kuwafunza maneno mazuri ya kuvutia ya lugha ya Kiswahili.

Nae Mkurugenzi wa Hoteli Kingazi Resort, Nelson Mahenge linapotarajiwa kufanyika shindano hilo amesema wamejiandaa kupokea ugeni mkubwa kutoka nchi mbalimbali za Afrika na kuahidi kutoa huduma bora zaidi katika kipindi chote cha shindano hilo.

“Sisi tunapatikana maeneo ya Kijichi, Mgeni Nani na tunawakaribisha wageni wote na tupo tayari kuwapokea, hapa tuna kila kitu ikiwemo malazi, chakula na vinywaji hivyo ukifika huduma zote zinapatikana hapa, nawaombea kila la heri washiriki wote ambao watakwenda kushiriki katika mashindano hayo, alimaliza kusema, “Mahenge.

Leave A Reply