The House of Favourite Newspapers

TANZANIA NA CHINA ZATILIANA SAINI KUANZA UJENZI WA CHUO CHA VETA KAGERA

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leornald Akwilapo pamoja na Mwakilishi wa Uchumi na Biashara nchini Tanzania Yuan Lin wakitia saini  mkataba wa makubaliano wa ujenzi wa chuo cha VETA.
...Dk. Leornald Akwilapo pamoja na Yuan Lin wakibadilisha hati za mkataba wa makubaliano wa ujenzi wa chuo cha VETA mkoani Kagera.

 

Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetiliana saini ya makubaliano na Serikali ya Jamuhuri ya watu wa China kuanza kwa ujenzi wa Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ambacho kinatarajiwa kukamilika mwaka 2020.

 

Makubakiano hayo yametiwa saini na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leornald Akwilapo na Mwakilishi wa Uchumi na Biashara nchini Tanzania Yuan Lin Jijini Dar es Salaam ambapo Dk. Akwilapo amesema Chuo hicho mpaka kukamilika kitagharimu zaidi ya shilingi bilioni 22.

 

Dk. Akwilapo amesema Chuo hicho kitakachojengwa mkoani Kagera kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 400  kozi za muda mrefu na 1000 wa kozi za muda mfupi ambapo miundombinu itakayojengwa katika chuo hicho ni pamoja na Madarasa, Karakana za Kufundishia, Majengo ya Utawala, mabweni  na Viwanja vya michezo.

 

“Chuo hiki ni kikubwa kwani kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 400 wa kozi za muda mrefu na wanafunzi 1000 wa kozi za muda mfupi, pia kitakuwa na mabweni yenye uwezo wa kulaza wanafunzi wavulana 200 na wasichana 100” amesisitiza Dk. Akwilapo.

 

Aidha, Dk. Akwilapo amesisitiza wakandarasi  wanaopewa mikataba ya ujenzi na wizara yake kuhakikisha wanatekeleza makubaliana ya mikataba hiyo kwa wakati  na kwamba serikali haitasita kuvunja mikataba yote inayositasita na kuwachukulia hatua za kisheria.

 

Akizungumza wakati wa utiaji saini Mkurugenzi Mkuu wa VETA Pancras Bujulu amesema Chuo hicho kinachojengwa mkoani Kagera kitasaidia kuongeza udahili wa wanafunzi katika fani mbalimbali za VETA kutokana na ukweli kwamba mkoa huo ni mkubwa na ulikuwa na chuo cha VETA Rwamishenye ambacho kilikuwa kidogo.

 

Naye Mwakilishi wa China anayeshughulikia masuala ya Uchumi na Biashara nchini Tanzania Yuan Lin amesema Serikali za Tanzania na China zimekuwa marafiki kwa muda mrefu na ndio maana imeona umuhimu wa kusaidia ujenzi wa chuo hicho ikiwa ni hatua ya kuunga mkono wa ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini.

 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

 

WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

 

Comments are closed.