The House of Favourite Newspapers

Tanzia: Naibu Waziri wa Kikwete Afariki Dunia

0

MBUNGE  wa zamani wa Mpwapwa mkoani Dodoma nchini Tanzania, Gregory Teu, amefariki dunia usiku wa kuamkia jana baada ya kujisikia vibaya akiwa kikaoni.

 

Akizungumza jana Jumatatu Januari 25, 2021, msemaji wa ukoo wa Teu Stanley Mbijili amesema Teu alikuwa kwenye kikao cha bodi ya Kampuni ya Maendeleo ya Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro (KADCO) ambacho yeye ni mwenyekiti wake.

 

Mbijili amesema Teu alifariki saa 9.00 alfajiri usiku wa kuamkia jana wakati akiendelea na matibabu katika hospitali ambayo bado haijafahamika. “Tunajua kuwa marehemu alienda Arusha kwenye kikao cha Bodi kwa sababu yeye alikuwa ni Mwenyekiti wa bodi hiyo ila hatujajua alikufa katika hospitali gani,” amesema.

 

Amesema utaratibu wa kusafirisha mwili wake utafanyika Januari 27 (kesho kutwa ) kutoka Arusha kwenda Wilayani Mpwapwa na kwamba mazishi yatafanyika Jumatano (Januari 28) katika makuburi yaliopo katika viwanja vya Kanisa la Watakatifu Wote Vighawe.

 

Amesema kuwa Teu alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu na sukari mara kwa mara. Teu aliwahi kuwa Mbunge wa jimbo la Mpwapwa (CCM) kati ya mwaka 2010 hadi 2015 na kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na baadaye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara.

 

Pia Teu aliwahi kuwa Naibu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kabla ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa Mpwapwa katika uchaguzi mkuu mwaka 2010. Aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi hiyo Oktoba 17 mwaka 2017 baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa mwenyekiti wa bodi hiyo, Balozi Hassan Kibelloh.

Leave A Reply