The House of Favourite Newspapers

Tatizo la Kutokwa na Uchafu Ukeni (Vaginosis)

0

LEO tutazungumzia tatizo linalowasumbua wanawake wengi, tatizo la kutokwa na uchafu unaotoa harufu mbaya sehemu za siri. Kitaalamu hali ya mwanamke kutokwa na majimaji (vaginal fluids) yenye rangi nyeupe au ya njano, ni hali ya kawaida na wala siyo tatizo endapo majimaji hayo siyo mazito sana na wala hayatoi harufu mbaya. Lakini endapo majimaji yanayotoka yapo katika hali ya ute mzito wenye rangi nyeupe au kahawia, yanatoa harufu kali na yanawasha, basi hiyo ni ishara ya ugonjwa uitwao Vaginosis. Majimaji au ute unaoteleza kutoka sehemu za siri ni njia inayowezesha viungo vya uzazi vya mwanamke kujisafisha na kuutoa uchafu wa seli zilizokufa na mabaki ya damu ya hedhi nje ya mwili.

 

Pia huvikinga viungo vya uzazi dhidi ya maambukizi ya bakteria au fangasi wanaosababisha magonjwa. Kwa kawaida huwa hayatoi harufu na huwa na rangi nyeupe au ya njano. Pia huwa na asidi ya Lactic ambayo huzuia kuzaliana kwa vijidudu vya maradhi na huzalishwa kwenye tezi za Bartholin (Bartholin’s glands) zilizopo kwenye shingo ya mlango wa uzazi (Cervix). Kwa kawaida, mwanamke hutoa kiasi cha gramu 2 za seli zilizokufa kutoka kwenye mji wa uzazi na gramu 3 za ute mwepesi kila siku. Kiwango hiki huweza kuongezeka au kupungua kutegemeana na mzunguko wa hedhi. Kuna wakati ute huwa mwepesi na unaovutika (kama ute wa yai la kuku) na kuna wakati huwa mzito kiasi na wenye rangi ya njano. Ute huu ni wa kawaida na huwatoka wanawake wote hususan baada ya kuvunja ungo.
SABABU ZA KUTOKWA NA UCHAFU NA HARUFU MBAYA

 

Kuna sababu nyingi ambazo husababisha mwanamke kutoa ute au majimaji yasiyo ya kawaida kutoka kwenye sehemu zake za siri. Maambukizi ya bakteria wanaosababisha
magonjwa kama Trichomoniasis, Candidiasis, Gonorhear au uambukizo wa bakteria Candida albicans, Vaginosis Bacteria n.k husababisha mwanamke kutokwa na uchafu unaoambatana na harufu mbaya. Pia mabaki ya vitambaa, tishu au pedi ambazo hazikutolewa wakati wa hedhi huweza kusababisha tatizo hili. Usafi wa sehemu za siri usipozingatiwa hususan mwanamke anapokuwa kwenye siku zake za hedhi, huweza kuwa mazalia mazuri ya bakteria wanaosababisha harufu mbaya.
DALILI ZA UGONJWA WA VAGINOSIS

Mwanamke mwenye tatizo la Vaginosis huwa na dalili kubwa ya kutokwa na ute na majimaji yasiyo ya kawaida (uchafu) kutoka sehemu za siri. Uchafu huu huwa unatoa harufu kali kama shombo ya samaki au kitu kilichooza na huambatana na maumivu makali ya tumbo chini ya kitovu.
– Wakati mwingine uchafu wenye rangi kama ya kijani hutoka. – Kuwashwa na kuchomachoma sehemu za siri, mgonjwa asipopatiwa tiba haraka husababisha vidonda sehemu za siri. – Mwanamke anapoona anatokwa na ute uliochanganyikana na damu hata kama hayupo kwenye siku zake, hii ni dalili nyingine ya Vaginosis. – Maumivu makali wakati wa tendo pia ni dalili za ugonjwa huu.
MATIBABU

Tatizo hili hutibika hospitalini baada ya vipimo vya kitaalamu kuchukuliwa na daktari au nesi mwenye uzoefu wa kutosha juu ya magonjwa ya wanawake. Dawa za kupaka (Ointment/ Cream) na dawa za kumeza (Pills) huweza kumaliza tatizo hili. Kumbuka: Ni makosa kutumia dawa bila kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa daktari au nesi

Leave A Reply