Tatizo la mwanaume kukosa mbegu za uzazi (AZOOSPERMIA)

TATIZO la mwanaume kukosa mbegu za uzazi kitaalam huitwa ‘azoospermia’ au ‘medical condition’. Ni tatizo la kitabibu na linafanyiwa uchunguzi na kutibiwa hospitalini tu na siyo sehemu nyingine. Katika hali hii, mwanaume anakuwa hana mbegu hata moja inayoonekana kwenye manii yake. Hali hii inaweza kusababisha ugumba na utasa kwa mwanaume. Katika hali ya ugumba maana yake linaweza kupatiwa ufumbuzi, lakini inapofikia utasa, uwezo wa kuzaa unakuwa haupo kabisa.  Tatizo la mwanaume kukosa mbegu za uzazi ni kubwa na husababisha ndoa kukosa tiba ingawa kwa kiasi kikubwa lawama huelekezwa kwa mwanamke.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, tatizo hili huathiri asilimia moja ya mwanaume, yaani kuwa tasa, kukosa kabisa uwezo wa kuzaa na asilimia ishirini husababisha ugumba kwa wanaume ambapo huweza kutibika baada ya uchunguzi wa kina. Tatizo hili la kukosekana mbegu za uzazi linasababisha mwanaume kushindwa kumpa mimba mwanamke ndani ya mwaka mmoja wa uhusiano na limegawanyika katika makundi matatu;

PRETESTICULAR AZOOSPERMIA

Hapa mwanaume anakuwa na korodani zote kama kawaida, lakini hatoi mbegu za uzazi, anatoa manii tu. Tatizo kubwa linakuwa kwenye mfumo wa uchochezi ambapo homoni zake za kiume hushindwa kuchochea uzalishaji, homoni ya FSH inakuwa chini, kiasi kwamba inaathiri uzalishaji wa mbegu.

Tatizo hili linaweza kusababishwa na tatizo katika ubongo ‘hypopituitarism’ na ‘hyperprolactinemia’ na hata matumizi ya dawa za homoni za kiume bila uchunguzi wa kidaktari vinaweza kuathiri uchocheaji. Chanzo kingine ni wale wanaotumia dawa za kutibu saratani ‘chemotherapy’ ambao huathirika na hali hii. Tatizo hili la uzalishaji kutokuwepo kutokana na matatizo ya homoni pia ni kubwa.

TESTICULAR AZOOSPERMIA

Hapa korodani zinashindwa kuzalisha mbegu kutokana na kasoro. Aidha, korodani moja imesinyaa au zote mbili zimesinyaa, yaani ni ndogo sana au kubwa sana, zote au mojawapo, yaani ilimradi umbile la korodani zako si la kawaida, wengine hawana kabisa korodani moja au zote mbili hazipo. Hili ni tatizo kubwa la uzazi kwa mwanaume.

Mwanaume mwenye tatizo hili homoni zake za uzazi zinakuwa juu sana tofauti yule wa mwanzo kwa sababu ya kutokuwepo kwa mfumo wa mrejesho wa taarifa katoka katika ubongo ‘lack of feedback’ inhibition on FSH. Tatizo hili lipo kubwa kwa asilimia 49 hadi 93 kwa wanaume wenye matatizo ya uzazi ambao hawazalishi mbegu, watakuwa na mojawapo ya kasoro hizo tuizozitaja hapo juu.

Tatizo hili la korodani kushindwa kufanya kazi ya kuzalisha mbegu za uzazi huweza kusababisha mbegu zizalishwe kwa kiasi kidogo sana au zisizalishwe kwa kiasi kidogo sana au zisizalishwe kabisa na zikizalishwa zinakuwa hazijakomaa.

CHANZO CHA TATIZO

Matatizo ya kuzaliwa nayo au ya kijenetiki linachangia zaidi mfano ‘klinefelter syndrome’ korodani kutokushuka tangu utotoni na matatizo katika seli za uzalishaji mbegu ‘sertoli-only-syndrome’, maambukizi katika korodani ‘orchitis’ ambapo huambatana na maumivu ya mara kwa mara ya korodani, upasuaji wa korodani na mionzi, mfano ya X-Ray katika sehemu za siri. Pia ipo hali inayoweza kusababisha mbegu zako za kiume kuuawa au kukosa nguvu hii inayochangia kuzorotesha uzalishaji au kutoa mbegu zisizotemba.

TATIZO LINALOJITOKEZA BAADAYE  (POST TESTICULAR AZOOSPERMIA)

Hapa mwanaume hatoi kabisa mbegu za uzazi, anatoa manii tu, akichunguzwa utaona korodani zinafanya kazi kama kawaida na mbegu hazitoki maana zinakuwa tupu. Tatizo huwapata wanaume kati ya asilimia saba hadi 51. Chanzo kikubwa kitaalam tunaita ‘physical obstruction’ au ‘obstructive azoospermia’ wengi wanaopatwa na tatizo hili ni wale ambao wamefanya uzazi kwa njia ya ‘vasectomy’ uzibaji mwingine unaweza kuwa ni kasoro ya kuzaliwa nayo, mfano kusinyaa kwa njia ya kupitisha mbegu za uzazi kutoka kwenye korodani hadi katika tezi dume ‘agenesis of the vas deferens’ au kuziba kwa njia ya kutolea manii na mbegu kutoka katika tezi dume ‘ejaculatory duct obstruction’ kutokana na maambukizi sugu katika njia ya mkojo.

Matatizo katika utoaji wa manii, mfano ‘retrograde ejaculation’ ambapo tutakuja kulizungumzia kwenye makala zijazo. Katika hali hizi, korodani zinafanya kazi kama kawaida ya kuzalisha mbegu za uzazi, lakini hazitoki.

Matatizo mengine yanayoathiri uzalishaji wa mbegu za kiume hujitokeza tu pasipo kuwepo kwa vyanzo hivyo ila kuna mambo yanayochangia tatizo hili, mfano umri mkubwa na uzito mkubwa wa mwili yaani ubonge, uvutaji sigara na mazingira ya joto kali katika korodani.

UCHUNGUZI

Uchunguzi hufanyika kwa mwanaume kupimwa manii zake hospitalini, kuangalia uwepo wa mbegu za uzazi hasa baada ya kutafuta mtoto au ujauzito kwa kipindi cha mwaka mmoja au zaidi. Mwanaume pia atachunguzwa maumbile yake na hasa korodani zake kwa nje na ndani na kipimo cha ultrasound kitafanyika. Ultrasound pia itachunguza kama ana kasoro katika mirija ya usafirishaji mbegu za uzazi.

Vipimo vingine ni kama tulivyoona hapo awali, vipimo vya damu kuangalia homoni endapo kiwango cha homoni ya LH na FSH vitakuwa chini au kawaida kwa homoni ya testosterone, inaashiria tatizo hili ni lile la mwanzo la korodani kushindwa kufanya kazi kutokana na tatizo la vichochezi kama homoni ya ‘gonadropins’ itakuwa juu, basi tatizo ni katika kundi la pili la korodani yenyewe ‘testicular problems’ endapo korodani inazalisha mbegu nyingi, lakini hazitoki, basi itasaidiwa zitoke ‘testicular sperm extraction’ na kupandikizwa kwa mwanamke.

MATIBABU NA USHAURI

Kama tulivyoona hapo awali, matatizo ya uzazi kwa mwanaume yanakuwa makubwa kuliko hata kwa mwanamke. Katika matatizo ya korodani ya kwanza ‘pretesticular’ ina lile la mwisho ‘post testicular’ yanaweza kutibika, lakini lile la kati ‘testicular’ huwa ni vigumu kutibika. Nakushauri umuone daktari bingwa wa matatizo ya uzazi kwenye hospitali za rufaa za mikoa kwa uchunguzi usio wa kisayansi au kutumia dawa bila ya ushauri wa daktari.


Loading...

Toa comment