The House of Favourite Newspapers

TET na TSLTDOWasaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano Kusaidia Wanafunzi Viziwi  Kupata Elimu

0

Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na  Shirika la  Maendeleo ya Tafsiri ya Lugha ya Alama Tanzania (TSLTDO) wamesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano wa Kikazi wenye lengo la  kusaidia wanafunzi Viziwi  kupata elimu kwa kuwa na vifaa bora vya kujifunzia na kufundishia kama walivyo wanafunzi wengine.
Akizungumza  katika hafla hiyo, Mkurugenzi  Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba ameeleza kuwa makubaliano  hayo ya ushirikiano yatalenga  maeneo manne ambapo  baadhi yake ni TET itawakutanisha TSLTDO na Wakuza Mitaala kwa ufafanuzi wa jambo lolote iwapo itahitajika kufanyika hivyo.
Maeneo mengine ni TET kutoa usaidizi wa kitaalamu katika kutathmini usahihi wa ufasiri wa vitabu uliofanywa na TSLTDO kadiri itakavyohitajika pamoja na  kutoa fedha zitakazowezesha kukamilisha zoezi la kutafsiri vitabu vya kiada kwa mujibu wa taratibu na kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha.
“TET, kwa upande wetu tunayo mategemeo makubwa kuwa ushirikiano huu utatupelekea kutekeleza majukumu yetu na utatusaidia kuongeza  wigo kwa kuwafikia kundi lingine la wanafunzi wenye mahitaji maalumu na hivyo kuwawezesha wanafunzi viziwi kupata vifaa bora vya ujifunzaji na ufundishaji bila kikwazo chochote”, amesema Dkt. Komba.
Kwa upande wake, Rais wa TSLTDO, Mch.Sensor  Msimbete ameeleza kuwa ni jambo kubwa mno kwa wanafunzi viziwi sasa kuwa na vitabu ambavyo watakuwa na uelewa navyo.  Pia, ameishukuru Serikali kwa ujumla kupitia TET kwa kukubali kutafsiri vitabu vyote vya kiada kwa wanafunzi viziwi hapa  nchini.
“Hili ni jambo muhimu na kubwa kwetu jamii ya viziwi nchini, kwani sasa kwa wanafunzi wetu ni ukombozi mkubwa kwa wao kuweza kuelewa  zaidi masomo darasani kutokana na kupatikana kwa vitabu vitakavyoandakwa  kwa lugha wanayoielewa” amesema Mch.Msimbete.
Naye ,Mkurugenzi wa Elimu Maalumu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Magreth Matonya amesema kuwa, ni jambo la muhimu na la kihistoria kwa nchi kwani hii ni fursa pekee kwa wanafunzi viziwi sasa kuweza kusoma na kuelewa zaidi kwa kuwa na vitabu vitakavyokuwa na  lugha wanayoilewa.
Leave A Reply