The House of Favourite Newspapers

Tetemeko la Ardhi Laua 20 na Kujeruhi Zaidi ya 300 Pakistan

0

TAKRIBANI watu 20 wakiwemo watoto saba wamefariki dunia na wengine zaidi ya 300 kujeruhiwa, katika tetemeko lililoipiga Pakistan usiku wa kuamkia Alhamisi, majira ya saa tisa za usiku.

 

Kwa mujibu wa taasisi ya US Geological Survey (USGS), tetemeko hilo lenye ukubwa wa 5.9 kwa kipimo cha Ritcher (Richa), imeliathiri zaidi Jimbo la Balochistan lililopo Kusini Magharibi mwa nchi hiyo.

 

Kitovu cha tetemeko hilo kinatajwa kuwa ni katika Mji wa Milimani wa Harnai na kusababisha kubomoka kwa majengo mengi katika mji huo na maeneo ya jirani.

Mkuu wa Wilaya ya Harnai, Sohail Afridi amethibitisha kuwa miongoni mwa waliofariki, ni watoto saba na kuongeza kuwa juhudi za kuwaokoa watu walionasa kwenye vifusi vilivyosababishwa na tetemeko hilo, bado zinaendelea.

 

Ameongeza kuwa majeruhi wa tetemeko hilo, wamekuwa wakikimbizwa hospitali kwa kutumia helikopta za kijeshi tangu usiku na kueleza kuwa jeshi na vikosi vya uokoaji, vimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kunusuru maisha ya watu yaliyokuwa hatarini.

Barabara nyingi za kuingia na kutoka katika mji huo, hazipitiki baada ya vifusi kutoka milimani kuporomoka na kuziba njia huku miundombinu mingine ikiharibiwa vibaya.

 

Mara ya mwisho kwa Jimbo la Balochistan kupigwa na tetemeko kubwa, ilikuwa ni Septemba 2013 ambapo tetemeko lilipiga katika Mji wa Arawan na kusababisha zaidi ya watu 330 kufariki dunia huku wengine 445 wakijeruhiwa.

Leave A Reply