The House of Favourite Newspapers

TFF, TPLB Sogezeni Macho Yenu Championship Makosa ya Waamuzi, Mechi Zimebaki Sita

0
Wachezaji wa timu ya DTB.

MWENDO wa Ligi Daraja la Kwanza umeongeza mvuto kwa kiasi kikubwa wakati ligi hiyo ikiwa inakwenda ukingoni.

 

Vinara ni DTB wakiwa na pointi 55 na inavyoonekana kama watashinda mechi zao mbili zilizobaki na kujikusanyia pointi sita, watakuwa na asilimia 95 ya kuwa tayari wamepanda hadi Ligi Kuu Bara.

 

Pointi 61 zinaonekana kuwa uhakika wa kuingiza miguu yote katika Ligi Kuu Bara hata kama watakuwa na mechi kama nne hivi ambazo pia wana nafasi ya kushinda angalau mbili au tatu.

 

Wakati DTB wanaonekana kuwa na uhakika zaidi, juzi wamepoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Ndanda ya Mtwara ambayo haina uhakika wa kubeba ubingwa na inapambana kuokoa ‘roho’ yake. Hii ni sehemu ya kuonyesha ligi hiyo kuwa ni ngumu kwelikweli.

 

Utamu ulivyo ni yule anayeonekana kibonde ana uwezo wa kumzuia anayewania ubingwa. Hii ni sehemu ya kuonyesha kuwa ushindani utakuwa hadi mwisho wa ligi hiyo.

Msimamo wa Championship League baada ya mchezo uliochezwa wa Aprili 10, 2022.

Achana na lile kundi la pili, kwani DTB kama amechukua sehemu kubwa kuonekana itakuwa ni timu ya kwanza kupanda daraja na itaacha nafasi moja ambayo itagombewa na timu angalau nne ambazo ni Ihefu, Kitayosce, JKT Tanzania na Kengold.

 

Ingawa Ihefu na Kitayose ndizo zinazopewa nafasi zaidi katika nafasi hizo mbili lakini bado inategemea watazicheza vipi karata zao za mwisho ili ugali wao usipokwe na JKT Tanzania au Kengold kama watazicheza karata zao vizuri.

 

Hakuna ubishi kuwa Ligi Daraja la Kwanza kama Championship imebadilika na kupanda kiwango kwa kiasi kikubwa. Wamiliki wa timu hizo 16 wanapaswa kupewa pongezi kubwa kutokana na kupambana hadi mwisho licha ya gharama kubwa.

 

Baadhi ya timu zimesajili wachezaji wakubwa waliowahi kuzichezea timu kubwa za Tanzania kama Yanga na Simba lakini timu kubwa za DRC kama TP Mazembe na AS Vita ambao hapo nyumbani wakija nchini ilikuwa ni lazima wajiunge na timu kubwa za Ligi Kuu Bara.

 

Safari hii wanaonekana wakipambana Championship, jambo ambalo linaifanya ligi hiyo kuwa moja ya ligi kubwa zaidi katika Bara la Afrika kama utazungumzia ligi za daraja la kwanza katika nchi haza za Ukanda wa Chini ya Jangwa la Sahara. Ninaamini ukiachana na ile ya Afrika Kusini, basi Tanzania inaweza kuwa inafuatia.

 

Kwa kifupi ni hatua kubwa sana ya mafanikio ambayo inapaswa kuendelea kusimamiwa vyema na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB).

 

Wakati huu wa lala salama lazima kuwe na macho ‘makubwa zaidi’ kwa kuwa lazima ushindani unapoongezeka na fikra kwa wanaoshindana huchukua wigo mpana zaidi.

 

Wako watataka kushindana uwanjani lakini wako watataka kufanya ujanjaujanja. Jambo ambalo shirikisho na bodi kupitia kamati ya waamuzi lazima watupe macho yao.

 

Mara nyingi TFF na TPLB, wanajitahidi kwa asilimia kubwa sana. Lakini makosa ya waamuzi yamekuwa yakiwaangukia wao hata kama kosa ni la mtu mmojammoja au kama inatokea udhaifu kutoka katika kamati ya waamuzi.

 

Ndio maana, nawakumbusha kuwa wakati huu ni mwafaka kuinua shingo na kutupa macho kwa karibu katika mechi hizo sita kwa kila timu zilizobaki. Maana kama hakutakuwa na uangalizi wa karibu, mechi hizo chache zilizobaki ndizo zinaweza kubadilisha kila kitu.

 

Wapenda mpira wa Tanzania wanavutiwa zaidi na makosa kuliko mazuri yanayofanywa hata yakiwa mengi. Hivyo wasipewe hiyo nafasi na badala yake usimamizi uongezeke ili kuhakikisha ubora uliochipukia wa ligi hiyo, iwe hadi mwisho na msimu ujao mambo yaboreshwe zaidi hadi ligi hiyo ikiwezekana iwe namba moja Afrika kwa daraja la kwanza, inawezekana.

MAKALA NA SALEH ALLY (METODO)

WABUNGE WANAJENGA HOJA NZITO KWA SERIKALI, BUNGE LA 12, MKUTANO WA 7, KIKAO CHA 5…

Leave A Reply