The House of Favourite Newspapers

TFF Yamrudisha Morrison Yanga

0

BAADA ya sekeseke la siku kadhaa kuhusu mshambuliaji wa Yanga, Bernard Morrison kutofautiana na klabu yake, habari ni kuwa mambo sasa yanaelekea kuwa mazuri baada ya kutakiwa kurejea kwenye majukumu yake.

 

Juzi Jumatano nyota huyo Mghana aliitwa na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) ikidaiwa ni kuhusu masuala yake ya kimkataba na Yanga, baada ya kikao kizito, inaelezwa kuwa mabosi wa shirikisho hilo walimtaka mchezaji huyo kurejea kwa mwajiri wake na kuendelea na kazi kama kawaida.

 

Morrison amekuwa katika mvutano wa kimkataba na Yanga ambapo kulikuwa na taarifa kuwa mwenyewe anasema hakusaini mkataba wa nyongeza kuendelea kuitumikia Yanga kwa miaka miwili zaidi wakati klabu yake inaeleza kuwa alisaini.

 

Morrison mwenyewe alipoulizwa juu ya kinachoendelea baada ya kikao cha juzi, alisema: “Nimetakiwa kurejea kazini, na hapa ninajiandaa kwa ajili ya kwenda mazoezini.”

STORI :KHADIJA MNGWAI NA MUSA MATEJA

Alitoa kauli hiyo jana mchana ambapo hakuwa tayari kufafanua nini ambacho kilizungumzwa kati yake na mabosi wa TFF, ambao inadaiwa walimuita baada ya mchezaji huyo kutoa kauli ya akiungana na wenzake kuanzia katika kuwasili kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria uliopo Ubungo jijini Dar es Salaam, jana.

 

Championi Ijumaa ambalo lilikuwepo sehemu ya tukio lilishuhudia Morrison akishuka katika basi la timu, ikimaanisha kuwa alikuwa na wenzake kuanzia kambini, akaenda uwanjani na moja kwa moja kuanza mazoezi kama vile hakuna kilichotokea.

 

Naye Kocha Mkuu wa Yanga, Mbelgiji, Luc Eymael, awali alipoulizwa kuhusu mchezaji huyo, alisema ameshazungumza naye na kumpa masharti kadhaa muhimu ikiwa ni kumalizana na uongozi kwanza.

 

Taarifa kutoka ndani ya kambi ya Yanga iliyopo Hoteli ya Regency jijini Dar zinasema kuwa, Eymael amempa masharti mchezaji huyo ya kurejea kikosini hapo mara baada ya kumalizana na viongozi wake.

 

“Kocha Eymael anakikubali kiwango cha Morrison lakini amemtoa kambini kwa sasa kutokana na kile kinachoendelea kati yake na uongozi wake, hivyo amemtaka amalizane na uongozi wake ndipo amrejeshe kikosini.

 

“Iwapo mchezaji huyo atamalizana na uongozi wake kocha yeye hana shida yeyote, ataendelea kufanya kazi naye,” alisema mtoa taarifa.

 

Hiyo inamaanisha kuwa Morrisona sasa atakuwa tayari kuivaaa Simba katika nusu fainali ya Kombe la FA, Julai 12, mwaka huu kama akocha ataamua kumtumia.

NINJA AREJEA YANGA

Wakati huohuo katika mazoezi ya jana, beki wa zamani wa timu hiyo, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ alikuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kilichofanya mazoezi chini ya Luc kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria.

Ninja amekuwa hana timu tangu arejee nchini akitokea Marekani ambapo alikuwa akiichezea LA Galaxy ya Marekani kwa mkopo akitokea Klabu ya Ligi Daraja la Tatu ya Jamhuri ya Czech, MFK Vyškov.

 

Alishiriki katika mazoezi hayo vizuri kuanzia mwanzo hadi mwisho ambapo alikuwa amevaa jezi ya Yanga.Mtu wa karibu na uongozi wa klabu hiyo aliliambia gazeti hili kuwa Ninja yumo kwenye mipango ya Yanga kwa ajili ya msimu ujao.“Kama mambo yataenda vizuri tunaamini kuanzia msimu ujao tutakuwa naye kwenye kikosi chake,” alisema mtoa taarifa.

Leave A Reply