TGNP Yawanoa Kinamama Waliotwaa Udiwani
MTANDAO wa Jinsia wa TGNP leo Alhamisi umeanza warsha ya kuwanoa kiungozi kinamama kutoka mikoa mbalimbali waliotwaa udiwani na nyadhifa nyinginezo katika uchaguzi mkuu uliopita.
Warsha hiyo iliyofunguliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi inaendeshwa Makao Makuu ya mtandao huo, Mabibo Jijini Dar, ambapo inatarajiwa kumalizika Jumamosi ijayo.
Akifungua warsha hiyo Lilian amesema itaendeshwa na walimu wabobezi wa masuala ya uongozi lengo ikiwa ni wanawake nao kufikia usawa wa hamsini kwa hamsini na wanaume katika nafasi za uongozi.
Madiwani hao wanatoka katika Halmashauri 24 kutoka mikoa ya Mbeya Mara, Shinyanga, Morogoro, Pwani, Sumbawanga, Kilimanjaro na mingineyo.
Katika warsha hiyo madiwani hao kinamama walijifunza mambo mbalimbali ya kiuongozi na baadhi yao kutoa ushuhuda wa mambo makubwa waliyoyafanya katika maeneo yao.
Miongoni mwa madiwani waliotoa ushuhuda wa jinsi walivyopambana kutetea jamii ni Diwani wa Kata ya Mji Mpya iliyopo Manispaa ya Morogoro, Kiwa Rajab ambaye alipambana na kufanikiwa kubadili matumizi ya eneo lililokuwa likitumiwa na wanywaji wa pombe za kienyeji na kujengwa Zahanati inayotoa huduma mbalimbali ikiwemo kliniki ya wamama na watoto.
Madiwani hao walitoa shuhuda mbalimbali za mambo makubwa waliyoyafanya ambayo hapo awali madiwani waliopita walishindwa kuthubutu kuyafanya.
HABARI/PICHA: RICHARD BUKOS /GPL