The angel of darkness

Shambulizi kubwa la kigaidi linatokea kwenye kituo kikubwa cha biashara nchini Kenya, Kikuyu Mall na kusababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Wakenya, Watanzania na watu wengine kutoka mataifa mbalimbali.

Miongoni mwa wahanga wa tukio hilo la kikatili, wamo Watanzania, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam, mkewe, Asia Mustafa na watoto wao mapacha waliokuwa bado wachanga, Arianna na Brianna.

Kwa bahati mbaya, Ndaki na mkewe wanapoteza maisha katika tukio hilo, maiti zao na za Watanzania wengine zinasafirishwa mpaka nchini Tanzania ambako hatimaye wanazikwa.

Pacha wa kwanza, Arianna anapatikana na kurejeshwa nchini Tanzania ambako anakabidhiwa kwa ndugu zake. Bado haifahamiki pacha mwingine, Brianna yuko wapi na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Upande wa pili, mwanamke mwenye upungufu wa akili, Mashango anamuokota mtoto mchanga kwenye shambulizi hilo la kigaidi na kutokomea naye kwenye dampo, mahali yalipo makazi yake. Baadaye anahamia kwenye kitongoji cha watu maskini, Mathare, pembezoni kidogo mwa Jiji la Nairobi, mahali anakoweka makazi yake. Maisha yanazidi kusonga mbele huku mtoto huyo japokuwa alikuwa mdogo, akimpa changamoto kubwa za kimaisha Mashango.

Taratibu maisha ya Mashango yanaanza kubadilika kutokana na uwepo wa mtoto huyo, anaanza kufanya biashara ya mbogamboga na matunda na kuishi maisha ya kawaida kama binadamu wengine. Upande wa pili, Hans na mkewe wanatumia vibaya mali za marehemu na sasa wanajiandaa kutoroka kuukimbia mkono wa sheria.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Baada ya hali ya hewa kuvurugika kwa dakika kadhaa kwenye Shule ya Msingi Mathare kutokana na uwepo wa Mashango na mtoto Brianna, hatimaye wanafunzi waliokuwa wakishangilia kutokana na kumuona mwanamke huyo ambaye alikuwa akifahamika mno na watoto kutokana na ukichaa wake, hali ilitulia.

“Mama! Kwa nini wanakuimba na kukuita kichaa?” Brianna alimuuliza Mashango swali lililosababisha ashindwe kuzificha hisia zake, machozi yakawa yanamlengalenga. Alishindwa cha kumjibu zaidi ya kumshika mkono na kuanza kutembea naye kuelekea kwenye ofisi za mwalimu mkuu.

“Karibuni,” mwanaume wa makamo, aliyekuwa amevalia miwani na kuishusha kidogo kwenye pua yake, alizungumza kwa sauti nzito wakati Mashango na Brianna wakiingia kwenye ofisi yake.

“Nikusaidie nini mama,” alisema mwalimu huyo huku akikaa vizuri kwenye kiti chake na kuivua miwani yake. Sura ya Mashango haikuwa ngeni kwake lakini alishangaa siku hiyo alikuwa tofauti na alivyomzoea. Hakuwa Mashango yule aliyemzoea, aliyekuwa akivaa ‘malapulapu’ na kubeba makopo kichwani.

Alikuwa amebadilika mno, hali iliyomfanya hata yeye amtazame mara mbilimbili.

“Nimemleta mwanangu kuja kuanza shule,” alisema Mashango, hali iliyozidi kumduwaza yule mwalimu mkuu, akamkodolea macho Brianna akiwa haamini kama kweli yule ni mtoto wake.

“Huyu ni mwanao?”

“Ndiyo mwalimu,” alijibu Mashango kwa kujiamini, mwalimu akakosa kingine cha kumuuliza zaidi ya kuvua miwani yake na kuifuta vumbi kisha akaivaa tena.

“Unaitwa nani?” mwalimu huyo alimuuliza Brianna huku akiwa ameachia tabasamu hafifu.

“Naitwa Brianna Mashango.”

“Kweli unataka kuanza shule au mama amekulazimisha?”

“Napenda sana kusoma mwalimu,” alijibu Brianna kwa lafudhi ya kitoto lakini akionesha kujiamini sana na kuwa na uwezo mkubwa wa kujieleza. Mwalimu huyo akawachukua mpaka ndani kabisa ya ofisi yake ambapo alimuuliza maswali kadhaa Mashango kuhusu uhusiano wake na mtoto huyo na mtu ambaye angekuwa akimsimamia.

Mashango aliendelea kushikilia msimamo wake kwamba huyo ni mwanaye wa kumzaa, yeye ndiye msimamizi wake wa kila kitu na kwamba angebeba dhamana ya kumlipia mahitaji yote muhimu, ikiwemo karo ya shule na kutoa tahadhari kwa mwalimu huyo kwamba asije akatokea mtu mwingine yeyote na kudai kwamba huyo ni mwanaye.

Baada ya mazungumzo ya dakika kadhaa, hatimaye Brianna aliandikishwa rasmi kuanza masomo, Mashango akamlipia michango mbalimbali iliyokuwa ikihitajika kwani alikuwa na fedha za kutosha alizozipata kutokana na biashara yake ya kuuza mbogamboga na matunda akisaidiana na mwanaye huyo.

Taratibu zote zilipokamilika, waliondoka shuleni hapo kwa makubaliano ya mtoto huyo kuanza shule siku iliyokuwa inafuata. Furaha aliyokuwa nayo mtoto Brianna ilishindwa kujificha kabisa, akawa anarukaruka kwa furaha huku akibembea kwenye mkono wa Mashango wakati wakitoka eneo hilo la shule.

Wakaingia mitaani kuendelea na biashara kama kawaida yao ambapo faida iliyopatikana siku hiyo, ilitumika kwa ajili ya kumnunulia Brianna sare za shule, viatu pamoja na daftari.

Hatimaye kesho yake Brianna akaanza rasmi masomo, Mashango alishindwa kujizuia kulia wakati akimpeleka mwanaye shuleni, usingeweza kuamini kwamba huyo ndiyo mtoto aliyelelewa na mwanamke mwendawazimu. Alikuwa amevaa sare mpya ya shule, alikuwa na viatu vipya pamoja na vifaa vyote muhimu kwa ajili ya masomo.

“Nakutakia masomo mema mwanangu, kuwa makini watu wabaya wasije wakakuiba,” alisema Mashango huku akilia baada ya kumfikisha mwanaye shuleni, akamkumbatia kwa nguvu na kumbusu kwenye paji lake la uso, Brianna naye akafanya hivyohivyo, wakaagana huku Mashango akiendelea kulia.

Siku ya kwanza kwa Brianna shuleni ilikuwa ngumu sana lakini alijitahidi kuendana na mazingira kwa kadiri ya uwezo wake. Wanafunzi wenzake walikuwa wakimtania na kumzodoa sana kwamba mama yake ni kichaa lakini mwenyewe hakuwa akijali, kilichompeleka shuleni ilikuwa ni kusoma na nguvu zake zote alizielekeza kwenye masomo.

***

Hans na mke wake, waliendelea kupanga mikakati ya namna ya kutoroka kukwepa mkono wa sheria baada ya kukiuka masharti ya usimamizi wa mirathi. Hiyo ndiyo njia pekee waliyoona inafaa kwa wakati huo kwani endapo wangefanya masihara, ni kweli jela ilikuwa ikimuita Hans.

Mipango ya maandalizi iliendelea kimyakimya na ilipofika saa sita za usiku, Hans akiwa ameshakusanya fedha nyingi kutokana na kuuza mali nyingi za marehemu pamoja na kukombeleza fedha zilizokuwa zimesalia benki, walisubiri mpaka majirani wote wamelala kisha wakatoroka.

Waliwachukua watoto wao wote kinyemela na kumuacha mtoto Arianna akiwa amelala peke yake, akiwa hajui hili wala lile. Kwa kutumia gari la marehemu aina ya Toyota Lexus, Hans, mkewe na familia yake walitokomea kusikojulikana bila kumuaga mtu yeyote.

Arianna alipokuja kushtuka kesho yake asubuhi, alishangaa kujikuta amelala peke yake, tofauti na siku zote ambapo alikuwa akilala na ndugu zake, watoto wa Hans. Akakurupuka kitandani na kuanza kuita lakini hakuitikiwa, akatoka na kwenda mpaka kwenye chumba walichokuwa wanalala walezi wake hao lakini pia hakukuta mtu.

Kingine kilichomshtua mtoto huyo, ni kwamba vitu vingi sebuleni havikuwepo, vikiwemo vifaa mbalimbali vya umeme vilivyoachwa na wazazi wake. Hakuelewa nini kimetokea, kutokana na umri wake mdogo, alichoweza kufanya ilikuwa ni kuanza kulia tu.

Gari la shule lilipokuja kumchukua, Arianna hakuwa amejiandaa kwa chochote, hali iliyomshtua mwalimu wao aliyekuwa akiwapitia majumbani kuwakusanya, ikabidi ashuke na kwenda kuangalia nini kilichomtokea mtoto huyo mpaka asiwe amejiandaa mpaka muda huo huku akionekana kulia.

Mwalimu huyo ndiye aliyegundua hali isiyo ya kawaida nyumbani hapo, akamsaidia mtoto huyo kujiandaa, akafunga milango yote ya nyuma kisha akamchukua na kwenda naye shuleni ambako alieleza hali halisi aliyoikuta nyumbani kwao kwa mkuu wa shule.

Harakaharaka taratibu za kuwatafuta ndugu zake ikaanza ambapo si Hans wala mkewe waliokuwa wakipatikana kupitia simu zao. Baada ya kuwakosa, ilibidi watafutwe ndugu zake wengine ambapo walifanikiwa kuwapata, haraka wakaitwa shuleni na kwenda kuulizwa juu ya kilichotokea. Hakuna aliyeonesha kuwa na majibu.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

Loading...

Toa comment