The House of Favourite Newspapers

The angel of darkness – 32

0

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabaki kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake. Wanakubaliana wamdanganye mfanyabiashara huyo kwamba wawili hao ni ndugu wa damu wakati ukweli ni kwamba wawili hao ni wapenzi.

Wawili hao wanahamia kwenye jumba la kifahari la Msuya na mapenzi kati ya Arianna na Msuya yanaanza kukolea, jambo linalosababisha Diego awe kwenye wakati mgumu sana kihisia kutokana na wivu uliokuwa ukimsumbua kila kukicha.

Asubuhi moja, Diego na Arianna wananusurika kufumwa na Msuya, hata hivyo, baadaye anapoondoka, kunatokea mvutano mkali kati ya Arianna na Diego, jambo linalosababisha kijana huyo ampige na kumjeruhi vibaya. Anamuomba Arianna amfichie siri, jambo ambalo msichana huyo analikubali.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Umepatwa na nini mpenzi wangu?” alisema Msuya huku akiwa haamini alichokuwa anakiona. Kutokana na jinsi msichana huyo alivyokuwa amevimba, Msuya hakutaka kupoteza muda, akambeba juujuu mpaka kwenye maegesho ya magari, akamuingiza na kuondoka kwa kasi bila kumuaga mtu yeyote.

Akamkimbiza mpaka hospitali aliyokuwa akitibiwa yeye na familia yake ambapo jambo la kwanza ilikuwa ni Arianna kutundikiwa dripu kisha daktari akaanza kumfanyia vipimo kubaini sehemu alizokuwa ameumia.
“Kwani amepatwa na nini?”

“Wanasema ghafla alisikia kizunguzungu na kudondoka chini, akapoteza fahamu,” alisema Msuya, daktari akamtazama usoni akiwa ni kama haamini alichokuwa anakisikia, akatazama tena faili lake lililokuwa na vipimo vya majibu, akawa ni kama anayejiuliza maswali yaliyokosa majibu.

“Mbona inaonesha kama amefanyiwa shambulio? Kama angeanguka tu asingeumia kiasi hiki,” alihoji daktari huyo, Msuya akakosa cha kujibu kwa sababu alichokuwa anakijua yeye ni kwamba Arianna alidondoka. Daktari akaendelea kumchunguza kwa umakini kisha akatingisha kichwa kuonesha kutokubaliana na maelezo aliyokuwa anapewa.

“Ni kwa sababu ya heshima yako tu mzee, vinginevyo ilitakiwa kwanza mpitie polisi akapewe fomu maalum ya matibabu (PF-3) ndiyo tuje kumtibu,” alisema daktari aliyekuwa akimfanyia vipimo Arianna, Msuya akaendelea kukosa cha kujibu.

Harakaharaka Arianna alianza kutibiwa matibabu ya kina ikiwa ni pamoja na kumchunguza kwa undani kubaini alikuwa amejeruhiwa kiasi gani. Saa kadhaa baadaye, hali yake ilianza kutengemaa, akafumbua macho na kuanza kuzungumza.
“Arianna, unajisikiaje mpenzi wangu.”

“Najisikia vizuri baba, hapa ni wapi na nimefikaje?”
“Upo hospitali Arianna, pole sana.”
“Ahsante, nilianguka vibaya asubuhi na kuumia,” alisema Arianna huku akigeukia upande wa pili. Hakutaka macho yake yakutane na ya Msuya kwa sababu alijua anaweza kugundua kwamba anamdanganya.

“Pole sana, utakuwa sawa usijali, cha msingi tayari upo kwenye mikono ya madaktari, naamini utatibiwa na kupona,” alisema Msuya huku na yeye akijitahidi kujionesha kwamba ameamini kile kilichoelezwa na Arianna.

Msichana huyo aliendelea kupatiwa matibabu, usiku huo akalala hospitalini kwa sababu madaktari walikuwa wakihitaji kumchunguza zaidi ili kuona maendeleo yake. Usiku huo Msuya hakurudi kabisa nyumbani kwake, muda wote alikuwa amekaa pembeni mwa kitanda cha Arianna.

Mpaka kunapambazuka, hakuwa amepata hata lepe la usingizi kutokana na kutumia muda wote kumuangalia Arianna. Asubuhi ilibidi arudi nyumbani kwenda kubadilisha nguo kisha akaenda kazini kutoa taarifa kwamba alikuwa akiuguliwa.

Baada ya takribani dakika ishirini alikuwa tayari amesharejea tena hospitalini baada ya kuwa ameshatoka nyumbani alikoenda kuwahimiza wafanyakazi wake kuhakikisha wanamuandalia mgonjwa kifungua kinywa haraka na kumpelekea hospitalini kisha akarudi hospitalini.

“Vipi unaendeleaje mke wangu?”
“Naendelea vizuri kabisa, namshukuru Mungu na nakushukuru kwa kunihudumia vizuri,” alisema Arianna kwa sauti ya kudeka. Japokuwa alikuwa ameumizwa vibaya na Diego, mapenzi mazito aliyooneshwa na Msuya yalimfanya ajihisi kuwa na ahueni kubwa ndani ya moyo wake.

Hakuna kitu kilichomfurahisha kama kugundua kwamba kumbe kuna mtu pembeni yake ambaye yupo tayari kufanya chochote ilimradi amuone akiwa salama. Kutokana na huduma bora alizopatiwa tangu alipofikishwa hospitalini hapo, madaktari waliridhishwa na maendeleo yake na kuamua kumruhusu.

“Haya majeraha mengine yatakuwa yanapona taratibu na hizi alama kufutika,” alisema daktari, akakabidhiwa kwa Msuya na mipango ya kumrejesha nyumbani ikaanza mara moja. Kwa muda wote aliokuwa hospitalini, Diego hakwenda kumuona Arianna hata mara moja, jambo lililomshangaza kila mmoja ndani ya nyumba hiyo.

Ni mpaka waliporejea nyumbani ndipo Diego alipoenda kumjulia hali Arianna huku akitoa kisingizio kwamba amekuwa akiharisha kwa usiku mzima ndiyo maana alishindwa kwenda kumuona mgonjwa.

Siku hiyo ilipita huku Msuya akiendelea kumuonesha mapenzi mazito lakini bado ndani ya nafsi yake alikuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua nini hasa kilichotokea mpaka Arianna akawa kwenye hali hiyo. Hata hivyo, aliamua kutumia akili za kiutu uzima, akasubiri mpaka Arianna apone kabisa.

Wiki moja baadaye, tayari alikuwa amepona kabisa na yale makovu yalikuwa yameanza kufutika.
“Arianna!”
“Abee mume wangu mtarajiwa.”

“Siku ya harusi yetu imekaribia sana, zimebaki wiki chache tu utakuwa mke wangu halali.”
“Ni kweli Msuya.”

“Lakini mbona naona kama kuna mambo mengi unayonificha kuhusu maisha yako?”
“Kwa nini umeniuliza swali hilo Msuya?”
“Unaweza kuniambia ukweli juu ya kilichokutokea mpaka ukaumia kiasi kile?”
“Jamani mume wangu, si nilishakwambia kwamba nilianguka ghafla?”
“Unasema kweli?”

“Nasema kweli mpenzi wangu.”
“Hebu nitazame,” alisema Msuya lakini Arianna hakuthubutu kunyanyua uso wake kumtazama. Akajiinamia huku akichezea kucha zake.
“Arianna!” aliita Msuya huku akimuinua Arianna, macho yao yakagongana, wakabaki wametazamana huku Arianna akianza kulengwalengwa na machozi.

Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

Leave A Reply