The House of Favourite Newspapers

The angel of darkness – 37

0

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake na sasa maandalizi ya ndoa yao yamepamba moto. Wanakubaliana wamdanganye mfanyabiashara huyo kwamba wawili hao ni ndugu wa damu wakati ukweli ni kwamba ni wapenzi.

Wanahamia kwenye jumba la kifahari la Msuya na hatimaye, Arianna na Msuya wanafunga ndoa ya kifahari na kuacha gumzo kubwa jijini Arusha, wanasafiri mpaka kwenye Visiwa vya Hawaii kula fungate.

Wakiwa kwenye fungate, Arianna anaanza kusumbuliwa na arosto ya madawa ya kulevya na kujikuta akirudia tena matumizi ya madawa hayo. Baadaye inabainika kwamba amenasa ujauzito, hali inayomfurahisha mno Msuya.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti kwa Arianna. Ni kweli naye alikuwa anapenda kupata ujauzito wa Msuya lakini kila alipokuwa akijaribu kuvuta kumbukumbu na kuhesabu, alikuwa na wasiwasi mkubwa kama kweli ujauzito huo ni wa Msuya au ni wa Diego. Akabaki njia panda huku akiendelea kujaribu kukumbuka alikutana kimwili na nani alipokuwa kwenye siku zake za hatari.

Kwa bahati nzuri alikuwa na kawaida ya kutunza kumbukumbu za matukio muhimu kwenye maisha yake, akakumbuka kwamba aliweka alama kwenye ‘diary’ yake siku alipoanza kuziona siku zake katika mzunguko wake wa hedhi, akaanza kutafuta ‘diary’ yake na kupekua mpaka kwenye ukurasa aliokuwa ameandika kumbukumbu.

Bila kupoteza muda, alifungua mpaka kwenye ukurasa huo na kutazama tarehe alipoanza kuziona siku zake, kwa kutumia mbinu alizowahi kufundishwa na mwalimu wake wa sayansi kipindi alipokuwa anasoma, alianza kuhesabu kuanzia siku ya kwanza alipoanza kuziona siku zake kwa lengo la kuzitambua siku zilizokuwa za hatari.

“Mungu wangu,” alisema Arianna baada ya kukumbuka kwamba katika siku zote za hatari, kuanzia siku ya 11 tangu alipoanza kuona siku zake mpaka siku ya 17 ambazo kimsingi ndizo za hatari anazoweza kubeba ujauzito, alikutana kimwili na Diego.

Mbaya zaidi, siku ya 14 ambayo ndiyo ambayo yai hupevuka, alikutana na Diego na katika kumbukumbu zake akakumbuka kwamba baada ya kujidunga madawa ya kulevya, walifanya mapenzi kwa muda mrefu kuliko siku nyingine zote.

“Lazima utakuwa ni ujauzito wa Diego, hata sijui nitauficha wapi uso wangu,” alijisemea Arianna huku akilishika tumbo lake. Huo ulikuwa ni mtihani mwingine mgumu ambao ilikuwa ni lazima aushinde. Kila alipokuwa akimtazama Msuya na jinsi alivyokuwa akimuonesha mapenzi ya dhati, alijihisi kuwa na hatia kubwa ndani ya moyo wake.

“Hustahili Msuya, hustahili kulipwa ubaya mkubwa kiasi hiki,” Arianna aliendelea kuwaza, akashtuka kutoka kwenye dimbwi la mawazo baada ya kusikia mlango ukifunguliwa, harakaharaka akaifunga ‘diary’ yake na kujifanya anatafuta kitu kingine kwenye begi lake.

“Vipi mpenzi wangu, unatafuta nini?”
“Aah! Kuna kitu nilikuwa natafuta lakini siyo muhimu sana,” alisema Arianna huku akiinuka na kumkumbatia Msuya, akambusu kwenye paji lake la uso huku akijitahidi kuficha hisia za kuwa na hatia zilizokuwa zikimuandama.

Msuya aliendelea kufurahia taarifa za ujauzito wa Arianna huku mara kwa mara akimbeba juujuu na kumbusu tumbo. Arianna akawa anailazimisha furaha kwenye uso wake huku moyoni akiwa na mzigo mkubwa ambao hakuwa akijua atautua vipi.

Alipoona mawazo yanazidi kumsumbua, alitafuta upenyo na kumtoroka Msuya kwa dakika chache, akaenda kujifungia chooni na kujidunga madawa ya kulevya, zile hisia za kuwa na hatia zikayeyuka kama donge la mafuta liyeyukavyo kikaangoni. Ili kupoteza ushahidi, aliamua kuoga kabisa, akarudi chumbani na kupitiliza kulala kwa madai kwamba alikuwa anajisikia vibaya sana.

Kwa jinsi Msuya alivyokuwa na furaha kwa mkewe huyo kunasa ujauzito, hakutaka kumsumbua, akamsaidia kumfunika vizuri pale kitandani kisha akatoka na kufunga mlango ili Arianna apate muda wa kupumzika, yeye akaenda ufukweni ambako aliendelea kusherehekea kuhusu ujauzito wa mkewe huyo.

Kutokana na dozi aliyokuwa amejidunga, Arianna alilala kwa muda mrefu bila kuzinduka. Ulipofika muda wa chakula, ilibidi Msuya aende kumuamsha ambapo ilimchukua dakika kadhaa kuamka na kurudi kwenye hali yake ya kawaida.

Kwa kuwa bado madawa hayakuwa yameisha kichwani mwake, Arianna hakukumbuka chochote kuhusu mzigo mkubwa aliokuwa ameubeba ndani ya moyo wake, wakala chakula pamoja na kadiri muda ulivyokuwa unazidi kusonga mbele ndivyo alivyokuwa anazidi kuchangamka.

Siku hiyo ilipita, kesho yake asubuhi Msuya ndiye aliyekuwa wa kwanza kuamka, akaenda kuwasha jakuzi kwani alijua mkewe akiamka hupenda kwenda kukaa humo, baada ya kumaliza alienda kumuamsha Arianna na kumpeleka mpaka bafuni na kuanza kumuogesha kama mtoto mdogo.

“Napenda sana jinsi unavyonidekeza mume wangu,” alisema Arianna na kumbusu mumewe mdomoni.

“Sasa nisipokudekeza wewe nitamdekeza nani mke wangu? Wewe ndiyo furaha ya moyo wangu na lazima nikutunze kama mboni ya jicho langu,” alisema Msuya kwa hisia za hali ya juu, kauli hiyo ikaenda kuuchoma moyo wa Arianna kama mkuki wenye ncha kali. Alitamani siku zirudi nyuma ili arekebishe makosa na kuwa mwaminifu kwa Msuya.

Kila hisia hizo zilipokuwa zikimjia, alikuwa akishindwa kukabiliana nazo, njia pekee akaona ni kuendelea kujidunga madawa kisha kuuchapa usingizi mzito huku akimhadaa Msuya kwamba anajisikia vibaya kutokana na mimba yake changa.

Ilimuwia vigumu sana Msuya kuelewa kilichokuwa kinaendelea nyuma ya pazia kwa sababu kutokana na uzoefu wake wa kuishi na mke, alijua ni hali ya kawaida kwa mwanamke kuwa na hali mbaya katika siku za mwanzo za kunasa ujauzito, akawa anajipa moyo kwamba hali ya Arianna itabadilika na baadaye atarejea kwenye hali yake ya kawaida.

Siku zilizidi kusonga mbele huku wanandoa hao wakiendelea kula fungate lao kwenye hoteli hiyo kubwa ya kifahari. Kadiri muda ulivyokuwa unasonga mbele ndivyo Arianna alivyokuwa anazidi kubadilika.

Ukiachilia mbali hali yake ya kuwa na mimba changa, matumizi ya madawa ya kulevya ambayo kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele ndivyo alivyokuwa anazidi kuongeza dozi kwa lengo la kujisahaulisha kuhusu tatizo kubwa lililokuwa mbele yake, yalianza kumfanya Arianna adhoofike na kupoteza ule mvuto wa asili aliojaaliwa. Bado Msuya aliendelea kujipa moyo kwamba hali hiyo inatokana na ujauzito.

Hatimaye siku thelathini zilimalizika, maandalizi ya kurejea nchini Tanzania yakaanza kufanywa na Msuya kwani muda mwingi Arianna alikuwa akiuchapa usingizi, akiwa amepoteza kabisa mwelekeo kutokana na kutumia madawa kwa siri.

Baada ya kukamilisha taratibu zote hotelini hapo, wanandoa hao walipelekwa na gari maalum la hoteli hiyo mpaka kwenye Uwanja wa Ndege wa Honolulu visiwani humo.
Wakaingia ndani ya ndege kubwa na ya kisasa iliyokuwa na maandishi makubwa ubavuni yaliyosomeka KLM, Msuya akawa anamsaidia Arianna kwa kila kitu, mpaka kupanda ngazi za kuingia ndani ya ndege hiyo.

Dakika kadhaa baadaye, tangazo lilisikika kutoka kwa mhudumu wa ndege akiwataarifu abiria wote kufunga mikanda kwani ndege ilikuwa ikijiandaa kupaa. Msuya akamsaidia Arianna kufunga mkanda kisha akamtegulia siti yake ili aendelee kulala. Safari ya kurejea Tanzania ikaanza huku wakitarajiwa kubadilisha ndege mara mbili njiani, Doha, Qatar na Nairobi, Kenya.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave A Reply