The House of Favourite Newspapers

The angel of darkness – 41

0

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake na sasa maandalizi ya ndoa yao yamepamba moto. Wanakubaliana wamdanganye mfanyabiashara huyo kwamba wawili hao ni ndugu wa damu wakati ukweli ni kwamba ni wapenzi.

Wanahamia kwenye jumba la kifahari la Msuya na hatimaye, Arianna na Msuya wanafunga ndoa ya kifahari. Baadaye Arianna anagundua kwamba amenasa ujauzito na anapopiga hesabu, anagundua kuwa mhusika wa ujauzito huo si mumewe Msuya bali ni Diego, jambo linalomchanganya sana.

Anajikuta akizidi kuharibikiwa kimaisha na sasa ameanza kuchanganya bangi na Cocaine kwa lengo la kupunguza msongo wa mawazo, jambo linalosababisha mabadiliko makubwa kwenye tabia yake.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Baada ya kufokewa na Arianna, harakaharaka mfanyakazi huyo alitoka huku akipatwa na mshangao mkubwa, hakuelewa amepatwa na nini mpaka awe mkali kiasi hicho. Hata alipoenda kumsimulia mfanyakazi mwenzake kilichotokea, wote walibaki wamepigwa na butwaa, hawakuelewa ni kwa sababu gani Arianna alikuwa mkali kiasi hicho, wakahisi hayupo sawa lakini atarudi kwenye hali yake ya kawaida akishatulia.

Mabadiliko ya ghafla ya tabia hayakuwashangaza wafanyakazi hao na Diego pekee bali hata Msuya mwenyewe kwa sababu kuna muda Arianna alikuwa akishindwa kujizuia na kumjibu kwa ukali mumewe, jambo ambalo hakuwahi kuwa analifanya hata mara moja tangu amfahamu.

“Umepatwa na nini mke wangu? Mbona umekuwa mshari kiasi hicho?”
“Unaniudhi! Kwa hiyo unataka ukinikasirisha nikuchekee,” alisema Arianna baada ya kutokea hali ya kutoelewana kati yake na mumewe na kusababisha amfokee mumewe huyo, jambo ambalo hakuwahi kulifanya hata mara moja tangu wafahamiane.

Hata hivyo, Msuya alipiga moyo konde akiamini kwamba huenda hali ya ujauzito ndiyo iliyosababisha awe hivyo, akaamua kumvumilia huku akijitahidi kuwa mpole na kumnyenyekea kadiri ya uwezo wake wote.

Siku zilizidi kusonga mbele huku Arianna akizidi kubadilika kitabia kila kukicha. Madawa ya kulevya aliyokuwa akitumkia kwa kuchanganya bangi na Cocaine, yalimfanya aanze kuwa na tabia tofauti kabisa. Hakuwa Arianna yule wa wiki kadhaa zilizopita.

Kutokana na mapenzi mazito aliyokuwa nayo kwa mkewe, Msuya aliwatahadharisha wafanyakazi wake pamoja na Diego kujiepusha na kumkasirisha Arianna na inapotokea hivyo, wamsamehe kwa sababu alikuwa akisumbuliwa na ujauzito.

“Mh! Huu ujauzito gani mwenzangu. Kama kuzaa sote tumeshawahi kuzaa lakini mbona tulipokuwa na mimba hatukuwa hivi? Au wewe mwenzangu ulikuwa hivi?” mmoja kati ya wale wafanyakazi alimuuliza mwenzake, muda mfupi baada ya bosi wao kuwapa maagizo kuhusu Arianna.

“Mh! Mimi wala sina cha kusema mwenzangu, yangu macho,” alijibu mfanyakazi huyo huku akiendelea na majukumu yake ya kawaida. Hakuna aliyekuwa na majibu ya kilichosababisha Arianna akawa na hali hiyo.

Kama Msuya alivyokuwa amezungumza na mkewe Arianna, shule zilipofunga alienda kuwachukua wanaye na kuwaleta pale nyumbani kwake, akawatambulisha kwa mama yao mpya ambapo watoto hao walionekana kumpenda kutokana na jinsi alivyokuwa mrembo na alivyowapokea kwa furaha.

Maisha yakaendelea kusonga mbele lakini tofauti na awali, nyumba hiyo ilichangamka zaidi kutokana na uwepo wa watoto hao. Siku za mwanzo Arianna alijitahidi ‘kuekti’ kama anawapenda sana watoto hao lakini kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga mbele huku akiendelea kutumia dozi hatari ya madawa ya kulevya, alianza kuwanyanyasa watoto hao ikiwa ni pamoja na kuwafokea kwa ukali mara kwa mara hata pale wanapofanya kosa dogo.

Tangu enzi za uhai wa mama yao, watoto hao walizoea kudekezwa na kulelewa kama mayai, haikuwa kawaida ya mama yao mzazi kuwafokea au kuwatukana kama alivyokuwa akifanya Arianna, jambo lililosababisha wakose kabisa amani ya kuendelea kuishi nyumbani hapo.

Hata hivyo, kwa jinsi Arianna alivyokuwa akiwatishia, hakuna aliyethubutu kufumbua mdomo wake na kumwambia baba yao juu ya jinsi walivyokuwa wakinyanyasika. Hata wale wafanyakazi wa ndani wa Msuya, japokuwa walikuwa wakishuhudia jinsi watoto wa bosi wao walivyokuwa wakinyanyaswa na mama yao wa kambo, hakuna aliyethubutu kumwambia chochote Msuya.

“Arianna!”
“Mbona siku hizi umebadilika sana mpenzi wangu?”
“Nimebadilika nimekuwa mweusi au?”

“Hapana, umebadilika kabisa kitabia. Hata mimi ambaye ndiye niliyechangia kwa kiasi kikubwa ukaolewa na Msuya lakini sasa hivi unaniona kama sina maana kwako si ndiyo?”

“Usinichanganye bwana! Kama unaona mimi nafaidi olewa wewe na Msuya.”
“Unasemaje Arianna?” Diego alikasirishwa mno na kashfa alizokuwa anapewa na Arianna, jazba zikampanda baada ya kauli hiyo na kujikuta amemrukia Arianna na kumkaba shingoni, akamsukuma mpaka ukutani huku macho yakiwa yamemtoka pima kwa sababu ya hasira.

“Usinione nimekunyamazia ukafikiri nakuogopa. Naweza kukufanyia kitu kibaya ambacho hutakuja kukisahau halafu nikamwambia na huyo mumeo kwamba mimi siyo kaka yako bali mpenzi wako, usitake kuniona mi mshamba umeskia wewe!” alisema Diego huku akitweta kwa hasira.

Kwa jinsi alivyokuwa amekasirika, Arianna alijua endapo ataendelea kubishana naye anaweza kumfanyia kitu kibaya kama alivyoahidi, ikabidi awe mpole na kuufyata mkia.
“Sasa kwa sababu nimekupa uhuru lakini unashindwa kuutumia, sasa hivi ni zamu yako kunisikiliza ninachokisema, unanielewa?” alifoka Diego na kumuachia Arianna, akawa anajishika pale shingoni alipokuwa amekabwa na Diego.

“Unaona hii!” alisema Diego huku akitoa simu yake na kufungua sehemu ya video, akamuonesha video ya utupu aliyoirekodi wakati wakivunja amri ya sita chumbani kwa Arianna.

Kwa mshtuko alioupata, almanusra Arianna adondoke chini, akageuka huku na kule kutazama kama hakuna mtu aliyekuwa anawatazama. Akanywea na kumsogelea Diego, safari hii akionesha utii.

“Ukinizingua namtumia mumeo hata sasa hivi tukose wote.”
“No! Usifanye hivyo Diego, nipo chini ya miguu yako. Niko tayari kufanya chochote utakachotaka.”

“Ninachotaka mimi unakijua. Nataka tutoroke hapa kwa Msuya, twende mbali tukailee pamoja hiyo mimba kwa sababu mimi ndiye baba wa mtoto. Tumuibie Msuya fedha za kutosha na vitu vingine ambavyo vitatusaidia kuanza maisha huko tuendako.
“Tukiendelea kukaa hapa, siku ukijifungua Msuya atagundua ukweli na tutapoteza kila kitu, hebu amka usingizini,” alisema Diego kwa sauti ya chini lakini kwa msisitizo mkubwa.

Arianna alishusha pumzi ndefu na kumtazama Diego usoni, macho yao yakagongana.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave A Reply