The House of Favourite Newspapers

The Angel of Darkness (Malaika wa Giza) -21

1

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna. Arianna anaokotwa na vikosi vya uokoaji na kurejeshwa Tanzania ambako awali anakabidhiwa kwa mdogo wa marehemu baba yake, Hans ambaye anapewa jukumu la kusimamia mirathi na kumlea mtoto huyo.

Brianna anaokotwa na mwanamke mwendawazimu, Mashango na kwenda kuanza naye maisha kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Japokuwa mwanamke huyo alikuwa amechanganyikiwa akili, lakini anamlea vizuri mtoto huyo na kadiri muda unavyozidi kusonga mbele, ndivyo anavyozidi kuwa mkubwa huku mwanamke huyo naye akipona maradhi ya akili yaliyokuwa yanamsumbua.

Siku zinazidi kusonga mbele na kwa bahati mbaya zaidi, Mashango, mwanamke aliyekuwa akimlea Brianna kwa mapenzi makubwa, anagongwa na gari na kupoteza maisha, jambo linalomuathiri sana Brianna. Baadaye anajitokeza msamaria mwema, Wailima Njoroge ambaye anaamua kumchukua mtoto huyo na kuishi naye pamoja na familia yake.

Upande wa Arianna, maisha yanaanza kumuendea kombo ambapo Hans anatumia vibaya mali alizoachiwa Arianna na baadaye anatorokea kusikojulikana na familia yake. Arianna anaendelea kukua lakini kwa sababu ya kukosa uangalizi wa karibu, anajikuta akiingia kwenye vitendo viovu, ikiwemo matumizi ya madawa ya kulevya.

Baadaye Arianna anaamua kuuza nyumba aliyoachiwa na wazazi wake kinyemela na kutorokea Arusha akiwa na Diego. Kijana huyo anaendelea na biashara ya madawa ya kulevya na kwa bahati mbaya, polisi wanafanikiwa kupajua mahali alipokuwa akiishi na Arianna. Wanakwenda kuwakamata na kuwapeleka kituoni.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Kesi iliendelea kunguruma kwa kipindi kirefu na hatimaye, baada ya kuhonga fedha zote, vithibitisho vilibadilishwa na kuwekwa unga wa ngano, ushahidi wa kuwatia hatiani ukakosekana, hatimaye wakaachiliwa huru.

Wakarudi kuanza upya maisha, safari hii wakiwa hawana chochote cha kuanzia. Hali hiyo ilizidi kumchanganya Arianna, majuto yakawa mengi na kusababisha azidi kuongeza dozi ya kutumia madawa ya kulevya. Akazidi kuharibikiwa huku Diego akiendelea kubangaiza kuhakikisha wanapata fedha za kula na kununulia madawa ya kulevya kwa ajili ya matumizi yao.

Maisha yalizidi kuwa magumu kwao na kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele, ndivyo Arianna alivyozidi kudhoofika. Hata hivyo, uzuri wa kipekee wa sura yake uliendelea kujionesha.
“Dada habari yako,” mwanaume wa makamo, akiwa ndani ya gari la kisasa, Jeep Grand Cherokee (New Model) alizungumza kwa upole baada ya kuteremsha kioo cha gari lake, pembeni ya barabara.
“Nzuri.”

“Samahani kwa usumbufu, naomba kuzungumza na wewe japo kwa dakika chache, naitwa Engbelt Msuya, ni mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite, naishi Njiro ila huwa nakuja mara kwa mara kwenye huu mtaa, kuna rafiki yangu anaishi hapo jirani. Sijui mwenzangu unaitwa nani?”

“Arianna,” msichana huyo alijibu kwa kifupi kwani aliona mtu huyo anamchelewesha kwenda kununua madawa ya kulevya mtaa wa pili kutoka pale alipokuwa anaishi. Aliamua kutoka mwenyewe baada ya kuzidiwa na ‘arosto’ huku Diego akiwa hajarejea kwenye mihangaiko yake.

“Samahani, siyo mara ya kwanza kukuona na siku zote nilikuwa natamani sana kupata nafasi ya kuzungumza na wewe, naomba kama hutajali uingie ndani ya gari tuzungumze,” alisema mwanaume huyo lakini Arianna akakataa katakata kwa madai kwamba alikuwa na haraka.

“Basi naomba utakapokuwa na muda unipigie simu, hii ni ‘bussiness card’ yangu,” alisema mwanaume huyo huku akifungua droo kwenye gari lake, akatoa kadi ya mawasiliano na noti kadhaa za shilingi elfu kumikumi, akamkabidhi Arianna ambaye alipokea haraka na kuendelea na safari yake.

Yule mwanaume aliendelea kusimama palepale akiwa ndani ya gari lake, akamsindikiza Arianna kwa macho mpaka alipozamia kwenye vichochoro vya mtaa wa pili.Huo ndiyo ukawa mwanzo wa kuonana na mwanaume huyo, hakujua alikuwa nani, aliogopa kumzoea kwani akili yake ilimwambia kwamba inawezekana mwanaume huyo akawa polisi na alitumwa kwa ajili ya kumpeleleza tu.

Hofu ikamjaa moyoni mwake, hakutaka kumshirikisha suala hilo Diego, kila kitu kiliendelea kuwa siri.
Maisha yaliendelea kumpiga kila siku, alizidi kuwa arosto na wakati mwingine alibaki chumbani huku akijikuna mwili mzima kwani kukaa kwa kipindi kirefu pasipo kutumia dawa kulimuathiri mno.

Aliendelea kuitunza siri ya kukutana na mzee yule mpaka pale alipoona kwamba asingeweza tena kwani kwa jinsi alivyomuona mzee yule, alionekana kuwa na fedha ambaye angeweza kumsaidia katika kununua madawa ya kulevya, hivyo akaamua kumshirikisha Diego.

“Ana mapene?” aliuliza Diego.
“Yapo mengi kachaa wangu, sisi tu tushindwe kutumia,” alijibu Arianna kwa sauti ileile ya teja.
“Kama ndo hivyo haina mbaya, ipo mukide, kama vipi mcheki kwa mafoni basi tujue moja,” alisema Diego.
“Haina mbaya.”

Arianna akachukua simu yake iliyokuwa ya bei ndogo kisha kuanza kuzipiga zile namba alizokuwa amepewa na mzee yule kwenye kadi yake. Simu ilikuwa sikioni na baada ya sekunde chache, simu ile ikaanza kuita, iliita na baada ya muda fulani ikapokelewa na sauti ya mzee huyo kusikika.

“Nazungumza na nani?” ilisikika ikiuliza.
“Arianna hapa! Yule mrembo wa siku ile uliyekutana naye huku kitaa,” alijibu Arianna.
“Oooh! Nimekukumbuka! Tena nilikuwa nakufikiria sana mpenzi! Nafurahi kupata namba yako! Naweza kukuona leo?” aliuliza mzee huyo.
“Leo?”

“Ndiyo! Nataka nikuone sinyorita wangu,” alisema mzee huyo kwa sauti ya kimahaba ambayo aliamini ingemtega Arianna.
“Sawa! Nitakupigia nikwambie wapi,” alisema Arianna akakata simu. Akashusha pumzi ndefu, akamwangalia Diego, akaachia tabasamu pana.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda siku ya Jumatatu.

1 Comment
  1. katalo says

    Inasisimua

Leave A Reply