The House of Favourite Newspapers

Penzi Kabla ya Kifo -4

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA

“Ngoja nimfuate nikazungumze naye.”
“Elizabeth, huoni watu wanavyokuangalia?”
“Hata kama, siogopi chochote kile, acha nimfuate,” alisema Elizabeth.

SONGA NAYO

Hakutaka kuvumilia, moyo wake ulikwishakufa na kuoza kwa mwanaume huyo aliyemuona na kumpenda, akaanza kumsogelea, mapigo ya moyo yaliongezeka, alitaka kumwambia ukweli, hakutaka kuvumilia kuona akiteseka, alichokihitaji kilikuwa mapenzi kutoka kwa mwanaume huyo.

Japokuwa alizunguka kwa wanaume wengi pasipo kupata mtoto, akashindwa kujizuia, alipomwangalia, moyo wake ulimwambia kwamba angeweza kupata mtoto kupitia huyo, hivyo alitaka kuhakikisha anamwambia ukweli kwamba anampenda, hata kama angemkataa, lakini alitaka kumwambia ukweli tu.

Wakati akiendelea kumsogelea huku watu wengi wakimfuata, akiwa amebakiza hatua ishirini kabla hajamfikia, mara mlango wa gari aliloegemea mwanaume yule ukafunguliwa, mwanamke mmoja akateremka, alikuwa mzuri wa sura, alivutia, alimbeba mtoto wake mdogo, akamfuata mwanaume yule na kusimama pembeni yake, akazungumza naye kidogo, wakaingia garini.

Hakukuwa na siku Elizabeth aliyoumia kama siku hiyo, hakujua kama yule mwanamke aliyeteremka kutoka garini alikuwa mke wa yule mwanaume au rafiki yake. Akahisi kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake, akabaki amesimama huku akiliangalia lile gari ambalo liliwashwa na kuondoka mahali hapo.
“Haiwezekani!” alisema Elizabeth, hapohapo akalifuata gari lake, akaufungua mlango na kuingia ndani.
“Vipi Elizabeth!”

“Mwanaume yule anafaa kuwa mume wangu! Sitaki mwanaume mwingine zaidi ya yule,” alisema Elizabeth huku akionekana kuchanganyikiwa, hapohapo akawasha gari na kisha kuanza kulifuata gari lile. Akili yake ilichanganyikiwa mno. Donge kubwa la mapenzi likaung’ang’ania moyo wake.

Aliendesha gari kuelekea Mwenge, walikuwa wakilifuatilia gari lile lililoendeshwa kwa mwendo wa kawaida. Hawakutaka kulipita, waliendelea kulifuatilia mpaka lilipochukua Barabara ya Bagamoyo kuelekea Mbezi Beach.
Kilichomuuma Elizabeth ni uwepo wa mwanamke yule garini mule, hakujua kama alikuwa mkewe au dada yake, moyo wake uliumia mno mpaka yeye mwenyewe kujishangaa.
“Candy!”

“Abeee!”
“Hivi yule mwanamke ni nani?” aliuliza Elizabeth huku akiwa na wivu.
“Sijui! Labda mkewe,” alisema Candy pasipo kujua ni kwa jinsi gani jibu lake lilivyomuumiza Elizabeth.
“Haiwezekani! Hawezi kuwa na mume mzuri kiasi kile, yule anatakiwa kuwa na mwanamke mrembo kama mimi.”
“Ndiyo! Ila utafanya nini kama utagundua kwamba yule ni mkewe?”
“Tutaona, chochote nitaweza kufanya, hata kama kutumia utajiri wangu wote! Nipo radhi, ilimradi nimpate tu,” alisema Elizabeth.

Alimaanisha alichokisema. Kila alipomfikiria mwanaume yule, moyo wake ulimpenda mno, ilikuwa ghafla sana. Waliendelea kulifuatilia gari lile, lilipofika Afrikana, likakata kona kulia. Alichohitaji kujua ni mahali alipoishi mwanaume yule, alikuwa makini barabarani, kila walipopita, kwa kuwa gari lake lilikuwa la kifahari na lilijulikana sehemu nyingi, watu walilipiga picha tu.

Mbele wakakutana na makutano ya barabara, gari halikuchukua barabara nyingine zaidi ya kusonga mbele, lilipofika lilipokuwa likielekea, taa zikaanza kuwaka kuashiria kwamba lilitakiwa kuingia katika jumba la kifahari. Dereva akaanza kupiga honi.

Hicho ndicho alichotaka kuona, alipoona hivyo, akaridhika na hivyo kugeuza gari, kwa sababu alijua mahali alipoishi mwanaume yule, alichokifanya ni kuondoka mahali hapo.

“Tuondoke, nishapafahamu! Nitarudi siku nyingine,” alisema Elizabeth kisha kuondoka mahali hapo.
Siku hiyo ilikuwa ni ya kumfikiria mwanaume yule tu, hakumfahamu lakini alijihisi kuwa na mapenzi mazito juu yake. Kitandani, hakulala kama siku nyingine, alipofumba macho, taswira ya mwanaume yule ilimjia kichwani mwake kitu kilichompa wakati mgumu kupatwa na usingizi.

Alikuja kupatwa na usingizi saa saba usiku, muda wote huo alikuwa akiendelea kumfikiria tu. Alipoamka saa tatu asubuhi, kitu cha kwanza kabisa ni kumpigia simu Candy na kumtaka kufika nyumbani kwake haraka iwezekanavyo.
Je, nini kiliendelea? Fuatilia wiki ijayo.

Leave A Reply