The House of Favourite Newspapers

The Angel of Darkness (Malaika wa Giza) -22

0

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna. Arianna anaokotwa na vikosi vya uokoaji na kurejeshwa Tanzania ambako awali anakabidhiwa kwa mdogo wa marehemu baba yake, Hans ambaye anapewa jukumu la kusimamia mirathi na kumlea mtoto huyo.

Brianna anaokotwa na mwanamke mwendawazimu, Mashango na kwenda kuanza naye maisha kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare. Japokuwa mwanamke huyo alikuwa amechanganyikiwa akili, lakini anamlea vizuri mtoto huyo na kadiri muda unavyozidi kusonga mbele, ndivyo anavyozidi kuwa mkubwa huku mwanamke huyo naye akipona maradhi ya akili yaliyokuwa yanamsumbua.

Siku zinazidi kusonga mbele na kwa bahati mbaya zaidi, Mashango, mwanamke aliyekuwa akimlea Brianna kwa mapenzi makubwa, anagongwa na gari na kupoteza maisha, jambo linalomuathiri sana Brianna. Baadaye anajitokeza msamaria mwema, Wailima Njoroge ambaye anaamua kumchukua mtoto huyo na kuishi naye pamoja na familia yake.

Upande wa Arianna, maisha yanaanza kumuendea kombo ambapo Hans anatumia vibaya mali alizoachiwa Arianna na baadaye anatorokea kusikojulikana na familia yake. Arianna anaendelea kukua lakini kwa sababu ya kukosa uangalizi wa karibu, anajikuta akiingia kwenye vitendo viovu, ikiwemo matumizi ya madawa ya kulevya.

Baada ya Arianna kuuza nyumba anakwenda Arusha akiwa na teja mwenzake, Diego. Wanapofika huko, kwa bahati mbaya wanakamatwa na polisi hivyo kujikuta wakimaliza fedha zote mahakamani kwenye kutoa hongo. Baadaye, wakiwa kwenye maisha ya msoto, Arianna anakutana na mzee tajiri ambaye anatokea kumpenda. Diego anamwambia huo ni muda wa kumchuna fedha tu. Arianna anakubali.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Hakukuwa na sababu ya kumwacha mzee huyo aondoke mikononi mwake, kwa kuwa alikwishajilengesha na kwa muonekano wa nje tu alionekana kuwa na pesa, akaamua kukubaliana naye lakini lengo kubwa likiwa ni kumchuna fedha zake ili waweze kununua madawa ya kulevya kwani kwa kipindi hicho wote walikuwa wamepigika.
Diego hakutaka kutulia, kila alipoambiwa kwamba mzee aliyekutana naye Arianna ana uwezo mkubwa kifedha, aliendelea kumsumbua msichana huyo kuonana na mzee huyo tena kwa sharti moja kwamba hata naye awepo ili aweze kumuona na ajue amuingie vipi.

“Ila si umesema ni mshefa fulani hivi?” aliuliza Diego.
“Ndiyo! Ana pesa, kwanza hilo gari lake, ni noma, kama la Jay-Z,” alisema Arianna.
“Basi kama ndiyo hivyo, panga naye mishemishe halafu tuone tunamseti vipi, ni lazima tupige mpunga au unaogopa?” alisema Diego na kuuliza.

“Siogopi na ndiyo maana nimeamua kumseti, cha msingi ni kuonana naye tu.”
Siku waliyopanga kuonana ikafika, siku hiyo Arianna alijiandaa vilivyo, alijua kwamba alikuwa teja hivyo akajitahidi hata kupendeza ilimradi tu mzee huyo asiweze kugundua kama alikuwa mtumiaji mzuri wa madawa ya kulevya.
Alijitahidi kujiremba, alichana nywele zake vizuri, nguo zake ambazo alikuwa amekwishaziandaa, akazivaa kisha kujipamba kwa kujipaka wanja na vipodozi vingine, alipomaliza, akatoka na kuelekea katika baa iliyokuwa karibu na mtaa aliokuwa akiishi.

“Alisema baa ipi?”
“Sakina Pub.”
“Basi sawa. Sasa tukifika huko, nitambulishe kama bro wako, si unajua jembe likiwepo kila kitu kitakuwa mukide,” alisema Diego kwa maneno ya mitaani.
“Haina kwere….”

Walipofika hapo baa, wakatafuta sehemu iliyokuwa imejifichaficha na kutulia huko. Walikuwa mahali hapo wakimsubiria mzee huyo ambaye baada ya dakika thelathini, akafika na gari lingine la kifahari lililowafanya watu wote waliokuwa hapo baa kuyapeleka macho yao kule lilipopakiwa gari lile.

“Ndiye yeye! Huyo hapo,” alisema Arianna wakati mlango wa gari ulipofunguliwa na mzee huyo kuteremka.
Mzee yule akaingia hapo baa, hakuyatuliza macho yake, alikuwa akiangalia huku na kule kama mtu aliyekuwa akimtafuta mtu fulani. Arianna akasimama na kuanza kumfuata mzee yule kule alipokuwa.
“Ooh! My beautiful….” (Ooh! Mrembo wangu…) alisema mzee Msuya, hapohapo akamkumbatia Arianna.
“Karibu sana mpenzi…”

“Asante. Samahani kwa kuchelewa.”
“Usijali.”
Wakaelekea kule kulipokuwa na meza. Walipofika huko, mzee Msuya akabaki akimshangaa Diego. Kwa kumwangalia ilikuwa vigumu kugundua kama mtu huyo alikuwa teja, uvaaji wake tu, ulionesha kama mtu makini asiyekuwa na tatizo lolote lile.

“Huyu ni kaka yangu, anaitwa Diego. Baada ya wazazi wetu kufariki dunia, nimebaki na yeye tu, ndiye kila kitu kwangu, mama, baba na familia yangu,” alisema Arianna maneno ambayo hayakupingwa na mzee Msuya.
Vinywaji na vyakula vikaagizwa, muda mwingi mzee Msuya alibaki akimwangalia Arianna, alionekana msichana mrembo mno ambaye alistahili kuwa na mtu mwenye pesa kama alivyokuwa.

Kila alipomwangalia, moyo wake ulizidi kumpenda, alihisi kwamba tangu Mungu alipoanza kuumba, utaalam wake wote katika uumbaji aliumalizia kwa msichana huyo. Alishindwa kuvumilia, japokuwa aliambiwa kwamba Diego alikuwa kaka yake, Arianna lakini akajikuta akianza kumchombeza kwa maneno matamu hapohapo.

“Umependeza sana Arianna, u mwanamke ambaye sikudhani anaweza kuwemo katika dunia hii. Una mvuto sana, macho mazuri, uso wa kuvutia, umbo la kimisi, kwa kifupi, umenoga kila kona,” alisema mzee Msuya huku akimwangalia Arianna usoni.

“Kweli?”
“Kweli! Nimewahi kuwaona wanawake wengi, ila kwako, wewe ni mwanamke ambaye naamini Mungu alitulia sana siku ya kukuumba,” alisema mzee huyo.

Maneno matamu aliyoambiwa yakamfanya Arianna kujisikia wa thamani, Diego aliyekuwa pembeni alibaki akimwangalia mzee huyo, alichokuwa akikifikiria ni pesa, hakutaka kusikiliza maneno ya kimapenzi aliyokuwa akiambiwa Arianna, kwake, kila alipomwangalia mzee huyo, aliziona pesa tu, hivyo alihakikisha piga ua lazima mzee aingie katika ‘taimingi’ zao.

“Naomba utupishe kidogo kaka…” alisema Arianna, alimwambia Diego.
“Hakuna noma.”Walipoachwa wawili, mzee Msuya aliendelea kumwambia Arianna jinsi alivyokuwa akimpenda, maneno ya mzee huyo yalionesha ni jinsi gani alimhitaji Arianna kwa gharama zozote zile.
Msichana huyo hakuwa na mapenzi kwa mzee huyo ila kitu alichokiangalia kilikuwa ni fedha tu.
Walipigika, walikosa fedha za kununulia madaya ya kulevya hivyo kuwa na mzee huyo kuliwapa uhakika kwamba kila kitu kingekwenda poa.

“Sawa.
Nimekuelewa, nipo tayari kuwa nawe,” alisema Arianna.
“Na kama nitataka ukaishi nami nyumbani kwangu?”
“Kwako?”
“Ndiyo!”
“Na mkeo je?”

“Sina mke, alifariki dunia kwa ajali ya gari nchini Marekani miaka mingi iliyopita,” alisema mzee huyo, Arianna hakuwa na tatizo, akakubaliana na mzee huyo kwenda kuishi naye ila kwa sharti moja, kwamba naye Diego alitakiwa kuishi naye awe mfanyakazi wa ndani, kwa hilo, wala halikuwa tatizo, mzee Msuya akakubaliana naye pasipo kujua kama watu hao walikuwa na mipango yao vichwani.

Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

Leave A Reply