The House of Favourite Newspapers

The Angels of Darkness – 59

1

Watoto wawili mapacha, Arianna na Brianna wanatenganishwa wakiwa bado wadogo kufuatia tukio baya la kigaidi linalotokea wakiwa mapumzikoni na wazazi wao nchini Kenya, kwenye kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi.

Katika tukio hilo, baba wa watoto hao, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa wanapigwa risasi na magaidi hao na kupoteza maisha, wakiwaacha watoto wao wakiwa bado wachanga.

Kila mmoja anapitia maisha tofauti kabisa, Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anaokotwa na mwanamke mwendawazimu, Mashango ambaye anaishi naye kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Baadaye Mashango anafariki dunia baada ya kugongwa na gari na Brianna anachukuliwa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge. Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kuamua kumuoa Arianna na kumchukua pia Diego kwenda kuishi naye kwenye jumba lake la kifahari bila kujua kwamba wawili hao walikuwa wapenzi.

Baadaye Arianna ananasa ujauzito wa Diego na wanapanga njama za kutoroka. Wanatengeneza tukio feki la ujambazi ili ionekane wamevamiwa na Arianna kutekwa na majambazi. Msichana huyo anafanikiwa kutorokea nchini Kenya lakini kazi haiwi nyepesi.

Anaponea chupuchupu kufa katika kituo cha polisi cha Lianai baada ya magaidi kukivamia kituo hicho na kukichoma moto. Anaponea kwenye tundu la sindano na kutorokea Nairobi lakini hakuna anayejua kwamba amenusurika.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Mabaki ya miili ya watu wote walionasa na kuteketea kwa moto kwenye Kituo cha Polisi cha Lianai kilichochomwa moto na magaidi wa Kisomali waliovamia na kuwaokoa wenzao waliokuwa wakishikiliwa, ilitolewa na kupelekwa hospitalini ambapo kazi ya kupima vinasaba (DNA) ili kuwatambua ilianza.

Muda wote Msuya alikuwa akilia huku Diego akitumia muda mwingi kumbembeleza. Kila kitu kilitokea kwa kasi kubwa kiasi cha kumfanya Msuya ahisi kama yupo ndotoni.

Ni saa chache tu zilizopita aliagana na mkewe kwa furaha wakati akimsindikiza uwanja wa ndege, akambusu kila sehemu ya mwili wake na kumtaka akitunze kiumbe kilichokuwa ndani ya tumbo lake lakini sasa kila kitu kilikuwa kimebadilika.

Arianna hakuwepo tena na mbaya zaidi, uwezekano mkubwa ni kwamba huenda alikuwa miongoni mwa watu walioteketea kwenye kituo hicho cha polisi. Msuya alijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu, alihisi kama Mungu alikuwa akimuadhibu kwa kosa ambalo hakuwa akilijua.

Muda wote akawa analia kama mtoto mdogo, wakati mwingine akijihisi kama alikuwa kwenye ndoto ya kutisha na muda mfupi baadaye atazinduka na kujikuta amelala na mkewe lakini haikuwa hivyo.

Askari wa Kenya kwa kushiriana na wa Tanzania wa kitengo maalum cha Crime Scene Investigation (CSI), waliendelea na kazi ya kuifanyia vipimo vya vinasaba miili ya watu wote walioteketea kwenye moto na saa kadhaa baadaye, majibu yalianza kutoka.

Majina ya watu ambao vipimo vya vinasaba vilithibitisha kwamba wamekufa kwenye tukio hilo yalianza kutangazwa na kusababisha ndugu wengi waliokuwa wakisubiri kwa hamu majibu hayo, kuwa kwenye wakati mgumu sana kutokana na huzuni iliyotanda mioyoni mwao.

Majina yaliendelea kutangazwa lakini cha ajabu, jina la Arianna Joseph Ndaki halikuwa miongoni mwao, jambo lililozidi kumchanganya Msuya na Diego.

“Una uhakika kweli Arianna alikuwepo kituoni wakati tukio linatokea?”

“Si unaona jina lake lipo kwenye orodha ya mahabusu waliokuwa kituoni usiku wa tukio? Nina uhakika wa asilimia kubwa, si unaona hata polisi nao wanathibitisha kwamba walikuwa wakimshikilia?”

“Sasa nini kimetokea? Mbona sielewi?”

“Tusubiri, huenda labda mwili wake ni miongoni mwa ile iliyoharibika zaidi kiasi cha kushindwa hata kufanyiwa vipimo vya DNA au aliokolewa na magaidi, chochote kinawezekana, ni suala la kuwa na subira tu,” alisema Diego, Msuya akashusha pumzi ndefu na kujiinamia. Alikuwa anahisi kama amebeba dunia nzima kichwani.

Mpaka giza linaanza kuingia, hakukuwa na taarifa zozote kumhusu Arianna, miili karibu yote ilishatambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao ikiwa kwenye masanduku maalum yaliyotolewa na serikali ya Kenya lakini wa Arianna haukuwepo.

“Sasa tutafanyaje?”

“Mimi nafikiri kama tulivyofanya Tanzania, tufanye hivyohivyo huku Kenya. Tusambaze vipeperushi vyenye jina na sura yake kila mahali, tupeleke matangazo redioni na kwenye runinga na kutangaza dau nono kwa yeyote atakayefanikisha kupatikana kwake.”

“Wazo zuri, naumia sana Diego kwa sababu ya mke wangu, ni bora hata kama amekufa tujue moja ili tukaupumzishe mwili wake kwa heshima zote kuliko hivi, haifahamiki kama yupo hai au amekufa, moyo unauma sana,” alisema Msuya huku akilia, machozi na kamasi vikawa vinamtoka kwa wingi.

Walikubaliana kwamba yeye arudi Tanzania kuendelea kumsaka kipenzi chake na Diego yeye aweke nguvu zote nchini Kenya, akampa fedha nyingi kwa ajili ya kazi hiyo huku akimtaka wawe wanawasiliana mara kwa mara.

Huku akiendelea kulia, Msuya aliwashukuru maafisa wa polisi walioshirikiana naye tangu anafika na kuwaahidi kwamba yeyote atakayefanikisha kupatikana kwa mkewe kipenzi, atampa zawadi kubwa ambayo hatakuja kuisahau maishani mwake.

 Akapanda helikopta na kuondoka kurejea Arusha huku njia nzima akiendelea kulia. Alitamani Mungu aoneshe miujiza mkewe apatikane akiwa hai.

***

Alfajiri na mapema, Arianna aliamka na kuchukua kila kilicho chake, akakabidhi chumba na kutoka kwenye nyumba ya kulala wageni iitwayo Kimathi Lodge iliyopo Kariobangi, Nairobi aliyolala usiku uliopita. Kwa kuwa gesti hiyo haikuwa mbali na kituo cha matatu, alipotoka alienda kituoni na kuungana na abiria wachache waliokuwa kituoni hapo alfajiri hiyo.

Muda mfupi baadaye, alipanda kwenye matatu iliyokuwa inatoka Kariobangi kuelekea katikati ya Jiji la Nairobi, safari ikaanza. Kama alivyopanga tangu usiku uliopita, baada ya kuwasili kwenye stendi kuu ya mabasi, alikata tiketi kwenye basi lililokuwa likielekea Mandera, mji uliopo Kaskazini mwa Kenya, kwenye mpaka kati ya nchi hiyo na Somalia.

Safari hii hakukumbana na ugumu wowote, akaingia kwenye basi na kwenda kukaa kwenye siti ya nyuma kabisa huku muda mwingi akitumia mtandio kujiziba sura. Saa kumi na mbili kamili, safari ya kuelekea Mandera ilianza, Basi ya Nyayo Express likatoka stendi na kuanza kuchanja mbuga kuelekea Kaskazini mwa Kenya.

 Njia nzima Arianna alikuwa akimuomba Mungu wake afike salama kwani hali ilishachafuka na uwezekano wa kukamatwa tena na kujikuta akiishia kwenye mikono ya polisi wa Kenya ulikuwa mkubwa sana.

Basi likawa linachanja mbuga kwa kasi kubwa huku mara kwa mara Arianna akigeuka nyuma kutazama kama hakukuwa na gari la polisi lililokuwa likiwafuatilia.

Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

1 Comment
  1. barnaba says

    gud story nmeipenda

Leave A Reply