The House of Favourite Newspapers

The Angle of Darkness-65

0

Watoto wawili mapacha, Arianna na Brianna wanatenganishwa wakiwa bado wadogo kufuatia tukio baya la kigaidi linalotokea wakiwa mapumzikoni na wazazi wao nchini Kenya, kwenye kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi.
Katika tukio hilo, baba wa watoto hao, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa wanapigwa risasi na magaidi hao na kupoteza maisha, wakiwaacha watoto wao wakiwa bado wachanga.
Kila mmoja anapitia maisha tofauti kabisa, Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anaokotwa na mwanamke mwendawazimu, Mashango ambaye anaishi naye kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.
Arianna anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kuamua kumuoa. Baadaye, Arianna ananasa ujauzito wa Diego na wanapanga njama za kutoroka.
Msichana huyo anafanikiwa kutorokea nchini Kenya, jambo linalomfanya Msuya atangaze dau nono.
Hatimaye, pacha wa Arianna, Brianna anapatikana na kila mtu anaamini kwamba ndiyo Arianna na Diego anashiriki kuandaa mpango wa kumuaminisha Msuya kwamba huyo ndiye Arianna na tayari amefika nyumbani kwa Msuya lakini matendo yake yanazua maswali mengi kwa mumewe.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Kwa muda wote huo, Msuya alikuwa makini kuendelea kumfuatilia mkewe kila alichokuwa anakifanya. Akabaki na mshangao mkubwa kwani huyo hakuwa Arianna anayemjua yeye, akawa anajiuliza moyo wa uchapakazi na usafi wa kiwango hicho ameupata wapi? Hakuwa na majibu zaidi ya kuzidi kumpenda.
Kingine kilichomfanya aendelee kubaki njia panda, msichana huyo hakuwa anazungumzia chochote kuhusu ujauzito wake. Hata ile hali ya kudeka, kutapika na kulalamika kuwa anajisikia vibaya haikuwepo tena.
“Ina maana ujauzito upo au haupo? Na kwa nini anaonekana kufanya mambo tofauti kabisa na kawaida yake?” alijiuliza Msuya bila kupata majibu. Alichoamua kukifanya, ilikuwa ni kumpeleka hospitali bila mwenyewe kujua ili akampime na kujua kama ujauzito upo au ndiyo umeshaharibika.
“Kesho kuna mahali nataka unisindikize, sawa mke wangu?” Msuya alimwambia msichana huyo wakati akimalizia kufanya usafi ndani ya jumba hilo la kifahari.

“Sawa hakuna shida,” alisema Brianna huku akijaribu kuyakwepa macho ya Msuya. Baada ya kumaliza kufanya usafi, alienda bafuni kuoga na kurudi kupumzika kwani haikuwa kazi nyepesi.
“Badilisha basi nguo mke wangu, huoni kama hizo zimelowana?” alisema Msuya huku akiinuka na kwenda kabatini, akamchagulia gauni zuri na kumtolea, akampa ili abadilishe.
Kama ilivyokuwa usiku wa siku iliyopita, Brianna aliingia bafuni na kujifungia mlango ndiyo akabadilisha nguo, akawa anajitazama kwenye kioo kikubwa kilichokuwa bafuni. Lilikuwa gauni zuri sana ambalo hakuwahi kuvaa tangu azaliwe, akawa anajigeuza huku na kule huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.
“Inaonekana mke wake alikuwa anafaidi sana,” alijisema Brianna huku akiendelea kujitazama kwenye kioo. Baadaye alitoka na kurudi pale kitandani. Msuya alishindwa kuficha mshtuko alioupata alipomtazama msichana huyo.
“Whaooo! Unazidi kuwa mzuri mke wangu, utafikiri siyo wewe?” alisema Msuya huku akiinuka na kutaka kumkumbatia, akaachia tabasamu hafifu lakini hakutaka kukumbatiwa, akajitoa kwenye mikono ya Msuya na kukaa pembeni.
“Leo utapenda upikiwe nini mke wangu! Nataka kukuona ukifurahi,” alihoji Msuya kwa sauti ya chini iliyokosa uchangamfu, hakuna kitu kilichokuwa kinamkosesha raha kama kitendo cha mkewe kukataa asimkumbatie wala asimsogelee mwilini.

Hata hivyo, aliendelea kujipa moyo kwamba matatizo aliyokumbana nayo ndiyo yaliyomfanya awe na hali hiyo, akawa na imani kubwa kwamba atakuwa sawa baada ya muda si mrefu.
“Hujanijibu mke wangu, unataka leo wakupikie nini?”
“Chakula chochote tu,” alisema Brianna, jambo ambalo pia halikuwa kawaida kwa Arianna. Mara kwa mara alikuwa akipenda kutoa maelezo ya nini anachotaka kula. Hakuwa na simile katika suala hilo na pale wafanyakazi wa nyumba hiyo walipokuwa wakienda tofauti na maelekezo yake, alikuwa akiwajia juu na kuwafokea kama watoto wadogo.
“Basi sawa mke wangu, nakuona kama unahitaji muda wa kukaa peke yako, ngoja nikuache kidogo, ukinihitaji nipo hapo nje bustanini napunga upepo,” alisema Msuya, msichana huyo akatingisha kichwa kama ishara ya kumkubalia kisha Msuya akatoka.
Brianna alishusha pumzi ndefu kwani ni kweli alikuwa akihitaji muda wa kukaa peke yake na kuyazoea mazingira mapya. Kila kitu kilikuwa kigeni kwake, akawa na kazi ya ziada ya kuvunga ili asionekane mgeni kwani ingekuwa rahisi kwa Msuya kumshtukia kwamba hakuwa mkewe.

Msuya alipotoka, Brianna alianza kukichunguza vizuri chumba hicho, moyoni akawa anashangaa jinsi maisha yalivyokuwa tofauti, kwamba wakati familia ya Njoroge ikiishi kifukara, kuna watu walikuwa wakiishi kama wapo peponi.
Hakukaa sana chumbani humo, akatoka na kuelekea jikoni ambako wafanyakazi walikuwa wakiendelea kuandaa kifungua kinywa. Walipomuona tu, wote walikosa amani kwani Arianna alikuwa na kawaida ya kuwafokea na kuwanyanyasa mara kwa mara, wakajua lazima ataanza manenomaneno.
Hata hivyo, haikuwa kama walivyotegemea, msichana huyo aliomba wasaidiane kuandaa kifungua kinywa, akaanza kufanya kazi ndogondogo zikiwemo kusafisha vyombo vilivyotumika na kuweka kila kitu sehemu yake. Wakawa wanatazamana kwani haikuwa kawaida ya bosi wao.

Baada ya kifungua kinywa kuwa tayari, alisaidiana nao kuandaa meza, akaongozana na mfanyakazi mmoja mpaka kwenye chumba walichokuwa wanalala watoto wa Msuya kwa ajili ya kuwaamsha ili wajumuike pamoja.
Watoto hao nao hawakuwa wakimpenda mama yao mlezi kwani alikuwa na kawaida ya kuwafokea hata pale wanapokosea kidogo. Walipoona ameingia chumbani kwao, harakaharaka walikurupuka kitandani na kuingia bafuni kuoga.
“Kwa nini wanakimbikimbia halafu wanaonesha kama wanaogopa kitu?”
“Wanakuogopa, wanahisi utawafokea kwa sababu wamechelewa kuamka,” alijibu mfanyakazi huyo na kumfanya Brianna ajisikie vibaya sana ndani ya moyo wake. Tayari alishaanza kupata picha jinsi Arianna alivyokuwa akiishi ndani ya familia hiyo.

Akajiapiza ndani ya moyo wake kwamba atarekebisha kila kitu ambacho msichana huyo alikiharibu. Ilibidi aingie bafuni na kuanza kuongea kwa upole na watoto hao akiwasihi wasimuogope kwa sababu hatawafokea tena wala kuwapiga, akawasaidia kuwaogesha kisha wakatoka ambapo mfanyakazi tayari alishawachagulia nguo za kuvaa.
Wakatoka sebuleni na kwenda mezani ambako tayari Msuya alikuwa amekaa akiwa na Diego. Kitendo cha kumuona mkewe anatoka chumbani kwa wanaye, tena akiwa amemshika mmoja kwa upendo, kilimshangaza zaidi Msuya, alitambua fika kwamba mkewe hakuwa akiwapenda wanaye lakini alikuwa akijipa moyo kwamba huenda ni kwa sababu ya ujauzito aliokuwa nao, akabaki amepigwa na butwaa na kumtazama mkewe kwa macho yaliyojaa mshangao.

Diego aligeukia pembeni kwani alikuwa anajua kila kitu kinachoendelea, akaanzisha mazungumzo tofauti kabisa ili kupoteza mada ambapo hata hivyo, Brianna hakuwa mzungumzaji kama alivyokuwa Arianna. Wakaanza kupata kifungua kinywa huku mazungumzo ya hapa na pale yakiendelea.
Walipomaliza, Brianna kwa kushirikiana na wale wafanyakazi, walitoa vyombo na kusafisha meza, wakaelekea jikoni ambako pia walisaidiana kusafisha vyombo na kuweka kila kitu mahali pake, watu wote ndani ya nyumba hiyo wakabaki wamepigwa na butwaa.

Hawakuelewa ‘Arianna’ amekumbwa na nini mpaka abadilike kiasi hicho kitabia na kuwa mpole, mnyenyekevu, mstaarabu na mtu anayestahili kweli kuwa mama wa familia. Diego hakutaka kukaa sana sebuleni hapo, akatoka na kurudi chumbani kwake, Msuya akaendelea kukaa pale sebuleni na wanaye ambao nao walianza kumuuliza kwa nini mama yao anawaonesha mapenzi makubwa kiasi hicho.
Je, nini kitafuatia? Usikose  Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply