The House of Favourite Newspapers

Usipige Bwana…Tuma Meseji!-15

0

ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA:
Sasa siku hiyo kutokea Nancy ndiyo anaomba hisia zake zitambulike, Bony alihisi amepata muujiza ambao hakuwahi kuufikiria.
Mara simu yake iliita, alipiga Neema.
SASA ENDELEA MWENYEWE…

Bony aliipokea simu ya Neema huku akitetemeka, hakujua nini kitatokea kwenye mazungumzo. Akili yake ilimwambia, Neema anataka kumuuliza aliko, akajipanga kujibu uongo wenye kufanana na ukweli…
“Baby, ukija niletee pakti ya maziwa ya mtindi,” alisema Neema…
“Haya baby…baridi au moto?”
“Baridi bwana baby.”
“Sawa sweetheart.”
Baada ya kukata simu tu, Bony aliendelea kumfikiria Nancy…
“Yaani Nancy ninayemjua mimi, uzuri wake wote ule, kumtamani kote kule tangu siku nyingi, leo hii anasema mwenyewe?! Ama kweli unaweza ukalala ukaamka na bahati ya mtende kuota jangwani kwenye jua kali.
“Au ana mpango f’lani maalum sasa ndiyo anataka kuutumia ili anipate?” aliwaza sana Bony, wakati mwingine akijisikia raha, wakati mwingine akihisi kukosa amani, wakati mwingine akitaka kucheka kama siyo kutabasamu.
Kule alikokaa, Nancy kumbe alitarajia kuwa, baada ya Aisha kupita na kumbetulia midomo, Bony angekwenda kwenye meza yake, akaona kimya!
Aliinua kichwa kidogo lakini hakuweza kumwona Bony alipokaa, akamwita mhudumu…
“Anti, naomba hivi vinywaji vipeleke kwa anko mmoja amekaa hapo kona, juu amevaa t-shirt ina mchanganyiko wa rangi ya bluu na nyekundu. Mweupe hivi…”
“Yule aliyekuja na yule dada ametoka anatukana?”
“Ametoka anatukana? Dada yupi?” aliuliza Nancy…
“Hakuna dada amepita hapa ameshika mkoba wa njano ya mpauko?”
“Ee…”
“Sasa si ametoka kule nje anatukana matusi ya nguoni…”
“Anamtukana nani?”
“Sijui mwenyewe,” alisema mhudumu akiwa ameshabeba vinywaji hivyo na kuanza kutembea, Nancy alisimama na kumfuata kwa nyuma.

Bony naye alipoona kimya cha Nancy aliamua kubeba kinywaji chake ambapo kilikuwa kwenye kopo na kusimama kumfuata, wakakumbana kwenye kona…
“Eee…sisi tunakuja kwako na wewe unakuja kwetu?” alisema mhudumu huyo huku akiachia tabasamu laini kwa Bony…
“Da! Basi tuwekee kwenye meza ile pale,” alisema Bony akionesha meza tofauti kabisa na ile aliyokaa yeye na ile aliyokaa Nancy. Walikaa hapo…
“Enhe? Niambie shemeji yangu, nasikia mamaa ameonekana akitoka nje ya hii hoteli huku akitukana matusi ya nguoni,” alianza kusema Nancy…
“Nani Aisha?”
“Kumbe anaitwa Aisha?” alisema Nancy.
Bony alihisi amefanya ujinga kumtaja jina Aisha, kwani siku mambo yakivurugika, Nancy si atamwambia  Neema kwamba alimwona na msichana aliyemtambulisha kwa jina la Aisha…
“Yes! Alikuwa akitukana nje kwa sababu gani?”
“Sijui, huyu mhudumu ndiye anajua.”
“Mh!” Aliguna Bony.
Nancy akaamua ghafla kuyachenga mazungumzo hayo…
“Mambo mengine Bony?”
“Poa tu… huonekani kama zamani nyumbani?”
“Mh! Yaani niwe nakuja tu, niwe nakuja tu, faida yenyewe siioni. Afadhali sasa naweza kuja kwa sababu wewe upo. Siyo nakuja kuimwagilia maji ndoa ya mwenzangu kila siku halafu mimi nanyauka,” alisema Nancy huku macho yake yakikimbilia mbali.
Walizungumza sana, mwishowe saa nne usiku, Bony akaomba waondoke. Nancy hakuwa na usafiri, akadandia wa Bony.
Njiani, Bony alianza makeke bila kusubiri, mkono mmoja alishika usukani, mwingine alishika paja la Nancy na kulisuguasugua.

Nancy naye katika ubora wake, aliamua kutoa ushirikiano kwa kuushika mkono wa Bony na kumsaidia yeye kusuguasugua huku akilegeza macho.
Ilifika mahali kwenye barabara hakukuwa na magari, hivyo Bony aliweka gari pembeni na kuanza kula denda. Walikula denda mpaka wakachoka, Bony akatoa gari barabarani na kuendelea na safari mpaka nyumbani kwa Nancy…
“Sasa si unashuka kwanza baby?” Nancy alimwambia Bony…
“Siyo kwamba muda umekwenda sana sweet?”
“Noo! Wala, saa hizi muda umekwenda?”
Bony alikubali, akashuka, akamshika mkono Nancy mpaka ndani kwake huku wakiyumbayumba kwa kileo.
Je, unajua nini kilitokea? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Ijumaa, siku ya Ijumaa.

Leave A Reply