The House of Favourite Newspapers

The Angle of Darkness (malaika wa giza)-68

0

Watoto wawili mapacha, Arianna na Brianna wanatenganishwa wakiwa bado wadogo kufuatia tukio baya la kigaidi linalotokea wakiwa mapumzikoni na wazazi wao nchini Kenya, kwenye kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi.

Katika tukio hilo, baba wa watoto hao, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa wanapigwa risasi na magaidi hao na kupoteza maisha, wakiwaacha watoto wao wakiwa bado wachanga.
Kila mmoja anapitia maisha tofauti kabisa, Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anaokotwa na mwanamke mwendawazimu, Mashango ambaye anaishi naye kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Arianna anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kuamua kumuoa. Baadaye, Arianna ananasa ujauzito wa Diego na wanapanga njama za kutoroka.

Msichana huyo anafanikiwa kutorokea nchini Kenya, jambo linalomfanya Msuya atangaze dau nono.
Hatimaye, pacha wa Arianna, Brianna aliyekulia kwenye mitaa ya watu maskini Mathare, Nairobi nchini  Kenya anapatikana na kuchukua nafasi ya Arianna  lakini anaonesha tofauti kubwa ya kitabia, jambo linalomshangaza kila mtu.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Tofauti na madawa aliyozoea kutumia tangu akiwa nchini Tanzania, Cocaine aliyouziwa Arianna kwenye mji huo wa Mandera unaosifika kwa matukio mengi ya kihalifu, ilikuwa tofauti kabisa.

Muda mfupi baadaye, alianza kuhisi hali ya tofauti, kichwa kikawa kinamgonga kwa nguvu huku damu zikianza kumtoka mdomoni na puani. Ukichanganya na jinsi madawa hayo yalivyokuwa yamemlewesha, Arianna alikosa cha kufanya zaidi ya kujikongoja mpaka bafuni, akafungulia maji na kuingia kwenye sinki la kuogea, damu zikawa zinaendelea kumtoka kwa wingi huku maji yakijaa kwenye sinki hilo.

“Whats wrong upstairs, it seems there is water leakage in one of our rooms, call the plumber,” (Kuna nini kimetoka huko ghorofani? Inaonekana kuna maji yanavuja kwenye moja ya vyumba vyetu, hebu muite fundi bomba), meneja wa Hoteli ya Kornesh alimwambia dada aliyekuwa mapokezi.

Harakaharaka meneja huyo akapanda ngazi kuelekea vyumba vya ghorofani kuangalia tatizo ni nini kwani maji yalikuwa yakiendelea kuvuja kwa wingi.

“Ooh! My God! Somebody help! Help!” (Ooh! Mungu wangu! Jamani msaada! Msaada) alisema meneja huyo baada ya kufika kwenye mlango wa chumba alichokuwa amepanga Arianna na kukuta maji mengi yaliyochanganyikana na damu yakitoka kwa wingi chini ya mlango. Kwa kuwa alikuwa na funguo za akiba, harakaharaka alifungua huku akiendelea kupiga kelele za kuomba msaada.

Muda mfupi baadaye, wapangaji wa vyumba vingine pamoja na wahudumu wa hoteli hiyo walikuwa wamewasili eneo hilo, wakaingia ndani na kumkuta Arianna akiwa amelala kwenye sinki, maji yakiendelea kumwagika kwa wingi huku na yeye damu zikimtoka kila sehemu na kuchanganyikana na maji hayo.

Harakaharaka walimtoa Arianna kwenye sinki hilo akiwa hajitambui kisha wakafunga maji yaliyokuwa yanaendelea kutiririka kwa kasi, taratibu za kumuwahisha Arianna hospitalini zikaanza kwani alikuwa na hali mbaya sana, damu nyingi zikiendelea kumtoka puani, mdomoni na masikioni.

Meneja wa hoteli hiyo ndiye aliyekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanaokoa maisha ya mteja wao, wakamtoa mpaka nje ambapo tayari gari lilikuwa limeandaliwa, wakamuingiza na safari ya kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Mandera ikaanza kwa kasi kubwa.

Huku nyuma, fundi bomba kwa kushirikiana na wafanyakazi wawili wa hoteli ile, waliendelea kuhangaika kukausha maji yaliyokuwa yanaendelea kumwagika na baada ya kufanikiwa kuyadhibiti, kazi ya kufanya usafi chumbani humo ilianza.
“Fartooma, come and see this!” (Fartooma, njoo uone!) mfanyakazi wa hoteli hiyo aliyekuwa anajulikana kwa jina la Ashkir alimuita mwenzake wakati wakiendelea kufanya usafi chumbani humo baada ya kuona kitu kilichomshtua.

Yalikuwa ni mabaki ya dawa za kulevya pamoja na bomba la sindano alivyotumia Arianna kujidunga. Wote wawili walibaki wamepigwa na butwaa lakini wakaambizana kutogusa chochote lakini bosi wao akija wampe taarifa.

“How comes a beautiful lady like her is addicted in this deadly drugs?” (Inakuwaje msichana mzuri kama yeye atopee kwenye matumizi ya madawa haya yanayoweza kumuua?)
“No one knows! May Allah spare her life so that she learn to be obedient to Him.” (Hakuna anayejua! Mungu amnusuru maisha yake ili ajue namna ya kumtii) alisema Fartooma, wakaendelea kufanya usafi ndani ya chumba hicho huku wakiendelea kuulizana maswali yaliyokosa majibu. Mwonekano wa Arianna ulikuwa hauendani kabisa na tabia hatarishi aliyokuwa nayo.
***
Maisha ndani ya nyumba ya Msuya yalizidi kuwa mazuri huku amani na upendo vikizidi kutawala. Uwepo wa Brianna ulibadilisha kila kitu, hata zile sheria ngumu zilizokuwepo ndani ya nyumba hiyo, zote zikaondolewa. Wafanyakazi nao walizidisha bidii katika kumsaidia Brianna kuilea familia hiyo.

Kwa jinsi walivyokuwa wanaishi kwa upendo, ilikuwa vigumu sana kugundua kwamba walikuwa ni wafanyakazi, ungeweza kudhani nao walikuwa ndugu wa damu wa familia hiyo.

Hali ilikuwa hiovyohivyo kwa watoto wa Msuya. Kwa jinsi Brianna alivyokuwa anaishi nao vizuri, usingeweza kuamini kwamba siyo wanaye wa kuwazaa. Nao wakazidi kumzoea na kumpenda, hali iliyomfurahisha sana Msuya.

Kutokana na jinsi Brianna alivyokuwa anazidi kuchangamka kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele, Msuya hakuona tena umuhimu wa kumtafuta mtaalamu wa saikolojia kwa ajili ya kumsaidia mkewe kwani ilionekana ameweza kukabiliana na hali aliyokuwa nayo bila msaada wa mtu yeyote.

Hata hivyo, bado kuna mambo hayakuwa yakienda kama ilivyokuwa zamani ingawa hata hivyo hayakuwa makubwa. Ukaribu uliokuwepo kati ya mkewe na Diego, safari hii ulipungua sana, jambo ambalo hata hivyo lilikuwa likimfurahisha Msuya na kumfanya azidi kumpenda na kumuamini mkewe.

Tatizo pekee lilikuwa limesalia ambalo lilikuwa likimsumbua sana Msuya ndani ya kichwa chake, lilikuwa ni kitendo cha mkewe kuendelea kukataa kukutana naye kimwili. Hata baada ya wiki kadhaa kupita, bado Msuya alikuwa akiishia kumkumbatia tu mkewe lakini alipotaka haki yake, alikuwa akimkatalia kwa kisingizio kwamba bado tumbo linamuuma baada ya ujauzito wake kuharibika.

Msuya aliendelea kuvumilia lakini mwisho uvumilivu ukamshinda, kwa kuwa alikuwa mtu mzima anayefahamu mbinu mbalimbali za namna ya kumzidi akili mwanamke, aliamua kumuandalia mtego ambao aliamini hawezi kuukwepa.
“Nataka kesho tutoke mke wangu, nimeandaa ‘dinner’ hotelini kwa ajili ya kuboresha ndoa yetu,” alisema Msuya, Brianna akakubali bila kipingamizi. Msuya alikodi watu maalum kwa ajili ya kuandaa chumba atakachokitumia usiku huo yeye na mkewe.

Kitanda kikubwa na cha kifahari kilitandikwa mashuka nadhifu meupe kisha maua waridi mengi yakatandazwa kuanzia kitandani, kwenye zulia mpaka kwenye mlango wa kuingia ndani ya chumba hicho. Taa zote zilizimwa na badala yake mishumaa ya rangi nyekundu iliyokuwa ikitoa harufu nzuri iliandaliwa na kukifanya chumba kiwe na mvuto wa aina yake.
Mezani kulikuwa na chupa mbili za mvinyo aliokuwa anapenda kuutumia Msuya pamoja na matunda mengine ambayo hayapatikani kwa urahisi nchini Tanzania yakiwemo ‘raspberry’ na mengineyo.

Baada ya maandalizi kukamilika, Brianna akiwa amevaa gauni maalum alilonunuliwa na mumewe kwa ajili ya siku hiyo, huku Msuya akiwa amevalia suti nadhifu, waliaga nyumbani na kuelekea hotelini.

Walipofika hotelini, kwa kuwa tayari wahudumu walikuwa wanajua kuhusu ujio wa Msuya na mkewe, walipokelewa kama wafalme na kupelekwa mpaka kwenye bustani nzuri ambako nako kulipambwa vizuri kama kule chumbani. Wakakaa na kupata chakula cha usiku huku wakipiga stori za hapa na pale. Kwa jinsi Msuya alivyokuwa akimjali mkewe usiku huio, Brianna alijikuta akizidi kumpenda maradufu.

Baadaye wakatoka na kuelekea chumbani, kila kitu kilikuwa ‘sapraizi’ kwa Brianna, akawa anajihisi huenda yupo kwenye ndoto tamu ya kimapenzi. Waliingia na kwenda mpaka kitandani huku Msuya akimdekeza kama mtoto mdogo.
“Najua hujawahi kunywa pombe lakini leo nataka unywe huu mvinyo japo glasi moja tu, mwenyewe utafurahi,” alisema Msuya na kumbusu mkewe, kwa jinsi alivyokuwa na furaha, Brianna hakupinga, Msuya akafungua chupa moja na kumimina kwenye glasi mbili, wakaanza kunywa huku akimtazama mkewe kwa macho yaliyojaa matamanio.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply