The House of Favourite Newspapers

Usipige Bwana…Tuma Meseji!-19

0

ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA:
“Neema,” Nancy aliita kwa sauti ya mshtuko huku akisimama kwa jaziba…
“Niambie shoga yangu, nilifuata gauni langu kule mbele,” alisema Neema akienda kukaa kwenye lile kochi kubwa lisilokuwa na mtu…
TAMBAA NAYO…

“Hivi unajiridhishaje kumwamini mwanamke mwenzako kama huyu kwa shemeji Bony? Angalia wanakaa pamoja kama hivi,” alihoji Nancy huku akionekana kukerwa na kitendo cha wawili hao kukaa pamoja.

Bony alijua akisema lolote yataibuka mengi, aliingilia kati kwa hekima ya ubindamu…
“Shemeji Nancy, kama kero yako ni hiyo ya sisi kukaa pamoja wala usijali, mimi nakaa hapa sasa,” alisema Bony na kwenda kukaa kwenye kochi lingine…
“Haitoshi shemeji Bony…mimi nakulaumu wewe Neema. Huyu si wa kumpa nafasi ya ukaribu na mumeo. Si yeye tu hata kama ni mimi naishi hapa kwako lakini si wa kunipa nafasi ya ujirani kiasi kikubwa…

“Sisi wanawake siku zote zunapenda sana vilivyokwishapendwa na wengine. Si rahisi kukuta mwanamke anaanzisha upendo wake. Ila akikuta uliokwishaanzishwa na yeye anaingia hapo.”
Ulipita ukimya kidogo, Neema alikuwa akimwangalia sana Aisha kama kumsoma anachukuliaje madai ya mgeni wao Nancy. Lakini alimshangaa kumwona  anaiweka midomo yake kwa sura ya kejeli badala ya masikitiko kwamba anasingizwa jambo ambalo yeye halipo kichwani…
“Pokea maneno yangu Neema kama tahadhari katika ndoa yako..ohooo!”
Aisha alikuja kubadilika mbele, akasimama na kumwambia Nancy…
“Kama wewe ukipewa nafasi ya kuzoeana na mashemeji zako unapitiliza, mimi siko hivyo,” kisha akaondoka.
Neema aliingiwa na mawazo kibao kwani alikumbuka maneno ya awali ya Nancy baada ya kufika tu hapo kwamba alimwambia anamuamini vipi mumewe na Aisha…
“Nancy,” aliita Neema kwa sauti yake ya upole…

“Niambie shoga yangu…”
“Umezungumza nimekuelewa, lakini tatizo liko wapi? Kwa nini umemuwazia hivyo Aisha? Je, kuna dalili zozote umeziona? Lakini pia nilikuuliza au niliwauliza wote mnafahamiana? Hamkujibu lakini mpo kama mnayefahamiana hivi…kuna nini katikati yenu?”
“Neema katikati ya mimi na huyo nani sijui, Asha…”
“Aisha,” alirekebisha Neema…
“Ee Aisha, simjui hanijui. Ila mimi nakulaumu wewe Neema. Mtu hawezi kuja nyumbani kwangu akawa huru na mume wangu…
“Kwanza mimi nilishangaa sana kusikia na wewe unawaita mume na mke, nikajua ndiyo mazoea yenu…hii si sawasawa Neema. Mume anauma sana….kama anavyouma mke pia. Sidhani kama huyo mumewe aliyekwenda huko wapi sijui…”
“Ulaya,” neema akamsaidia…

“Ee…angekuwepo hapa kama angefurahia kumwona Bony na mkewe wamekaa beneti hivi mimi sidhani na siamini.”
“Nancy nimekusoma shoga yangu, niachie mimi sasa,” alisema Neema…

“Unisome kabisa,” alisema Nancy huku akimwangalia Bony kwa jicho la ‘nimekunyoosha.’
Baada ya hapo mazungumzo yaliendelea. Ilifika mahali, Neema akahisi Aisha hayuko sawa, ikabidi amfuate chumbani…
“Jamani ngojeni nimwone bibiye aliyeondoka kwa hasira, nadhani hayuko sawa,” alisema akienda.

Nyuma, Nancy alipohakikisha Neema amezama, alimwangalia Bony, akaachia tabasamu, akasema…
“Lazima nikuchomoe kwa huyu malaya wako Asha sijui Aisha. Haiwezekeni afaidi vizuri kiulaini wakati sisi wengine tumevitolea macho kwa miaka mingi. Yeye ni nani kwanza…”
“Sawa baby, lakini sasa huna sababu za kumchana hivi…si ajabu ulitaka kusema ya kule baa Mbezi,” alisema Bony…
“Wala ya kule sitayasema hata siku moja. Mimi nayasema ya kutetea masilahi yangu tu, nimemaliza.”
***
“Mke mwenzangu…yaani unaumia kichwa kwa ajili ya yule nung’ayembe kweli Aisha..?”
“Noo Neema…unajua amesema maneno mabaya sana kwangu…”
“Hayo maneno ameyasema kwa nani kama si kwangu na kwa Bony ambao wote tunakufahamu. Angewaambia majirani sawa. Hawezi kutenganisha ukaribu wetu.  Mimi mwenyewe asiponipigiaga simu yeye huwa simtafuti…

“Umemwona alivyokuja kama anakwenda disko! Wewe mwanamke anayejiheshimu anaweza kuvaa vile kwenda nyumbani kwa mtu tena mchana? Angekuja usiku sawa…”
“Mimi mwenyewe nilitaka kukutumia meseji nikwambie mna ahadi ya kwenda muziki? Maana lile gauni nalo mwenzangu…loo!”
***
Kule sebuleni, Nancy alipoona Neema anachelewa kurudi na yeye anataka kuondoka, alisimama kumfuata chumbani kwa Aisha…
“Wala hatuna ahadi yoyote ile,” alikanusha Neema…
Je, unajua nini kilitokea? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Ijumaa, Ijumaa ijayo.

Leave A Reply