The House of Favourite Newspapers

The World You Left Behind 34

0

Hatimaye mazishi ya Waziri Magesa yanakamilika na dunia nzima kuamini kuwa mtu huyo alikufa kweli, bila kujua ukweli halisi uliokuwa umejificha nyuma ya pazia. Viongozi mbalimbali wa serikali wanahudhuria, wakiwemo mabalozi walioziwakilisha nchi zao.

Huzuni kubwa inatanda miongoni mwa wananchi kutokana na historia nzuri na yakutukuka aliyokuwa amejijengea Magesa kutokana na utendaji kazi wake, ikiwemo uzalendo wa kweli wa kupinga vitendo vya kifisadi. Hali iliyomfanya kuwa na maadui wengi ndani ya serikali iliyokuwa imejaa uovu kwa urasimu wa watendaji wake wakiwemo mawaziri.

Upande wa pili mwanamke mrembo, Grace aliyeokoa maisha ya Magesa kwa kumuepusha na kifo katika ajali iliyokuwa imepangwa, akitumia mbinu ya kijasusi ikiwemo kununua maiti na kuivisha nguo za Waziri Magesa na kuiweka kwenye usukani wa gari la waziri huyo, aina ya Range Rover Evoque (New Model), lenye mfumo wa kujiendesha peke yake kwa teknolojia maalum.

Anafanikiwa kumuondoa nchini Tanzania, ambapo kwa pamoja wanafika nchini Kenya, katika mji wa Mombasa, Mtaa wa Kizingo, ndani ya jumba la kifahari alilokuwa akiishi Grace.

Ni huko ndiko Magesa anaamua kumdadisi kwa undani Grace ili kujua ni nani haswa hadi aweze kumuokoa na kifo kwa njia ya kitaalam kwani kwa macho ya kawaida, ikiwemo urembo wake, haikuwa rahisi kuamini kama mwanamke wa aina yake angeweza kufanyia wema huo.

Je, nini kitafuata?

SONGA NAYO…

SWALI alilokuwa ameulizwa na Magesa lilimpa wakati mgumu sana Grace, ni kweli alikuwa anampenda kupindukia na ndiyo maana aliweza kujitolea kwa hali na mali kuokoa maisha yake, lakini kamwe hakuwa tayari kumueleza undani wa maisha yake.

“Mbona umekaa kimya, niambie tafadhali,” alizidi kusisitiza Magesa huku akimkazia macho Grace aliyekuwa amejiinamia huku akiminya vidole vyake vya mkononi.

“Please, Magesa hebu achana na maswali mengi yasiyokuwa na msingi, muhimu hapa ni kuangalia maisha yaendeje baada ya kujinasua na mikono ya maaadui,” alisema Grace, maneno ambayo yalimuingia sawasawa Magesa na kubaki amejiinamia na kuanza kutafakari mambo mbalimbali.

Maisha yalizidi kusonga ndani ya jumba hilo, Grace akimpa kila faraja ambayo Magesa alihitaji kuhakikisha anasahau kila kitu kilichotokea, jambo ambalo linafanikiwa kwa kiasi kwani urembo wa Grace ulitosha kabisa kuwa tulizo bora la Magesa katika ulimwengu mpya ambao alilazimika kuishi ili kulinda uhai wake.

Mara kwa mara, alikuwa akijiwa na mawazo juu ya maisha yake ya nyuma, zaidi aliikumbuka sana familia yake, wakiwemo watoto na mke wake Vivian ingawa kwa siku za mwisho walikuwa na ugomvi mkubwa. Ni dunia ambayo tayari alikuwa ameachana nayo.

“Unawaza nini Magesa, niliwahi kukueleza unatakiwa kusahau kabisa maisha yako ya nyuma, si rahisi tena kurejea maisha yako ya zamani katika ulimwengu wa kawaida, hiyo ni dunia uliyoiacha nyuma.”

“Sawa Grace, lakini naikumbuka sana familia yangu, hususan wanangu ambao niliishi nao vizuri.”

“Huna jinsi tena Magesa, huna jinsi baba yangu.”

Yalikuwa ni mazungumzo kati ya wawili hao, wakiwa sebuleni katika mapumziko huku wakipata chakula cha mchana.

Siku zikazidi kukatika, huku Magesa akijitahidi kusahau kila kitu, ingawa mara kwa mara alikuwa akitamani kukutana na watu wake wa karibu wakiwemo baadhi ya viongozi mbalimbali aliokuwa akifanya nao kazi. Mara kadhaa moyo ulimuuma sana kila alipokuwa akitazama taarifa za habari zikionesha matukio yaliyokuwa yakiendelea nchini Tanzania.

Wakati mwingine baadhi ya viongozi kutoka nchini Tanzania walikuwa wakifanya ziara nchini Kenya katika mji wa Mombasa lakini hakuwa na uwezo wa kuonana nao, aliishia kuumia moyoni na kuzidi kumuomba Mungu atende muujiza siku moja arejee kwenye ulimwengu aliouzoea na kuungana tena na familia yake.

Wakiwa sebuleni, ghafla simu ya Grace iliita na kuipokea kwa haraka sana na kuanza kuzungumza huku akimtazama Magesa kwa macho ya kuibia. Kilichozua maswali mengi kichwani mwa Magesa, ni kitendo cha Grace kuzungumza kwa unyenyekevu wa hali ya juu huku akishindwa kuambulia chochote kwani Grace alikuwa akizungumza kwa mafumbo hali iliyozidi kumuweka katika wakati mgumu sana Magesa.

“Dah, nimepata safari ya dharura Magesa,” alisema Grace na kumshika Magesa mkono kwa staili ya kupapasa taratibu.

“Kwa hiyo?”

“Sina jinsi zaidi ya kusafiri.”

“Ni safari ya kwenda wapi?”

“Jerusalem, Israel.”

“Kufanya nini tena huko?”

“Acha maswali mengi Magesa, ipo siku utajua kila kitu.”

“Sasa mimi nitaenda wapi?”

“Inabidi ubaki hapahapa.”

“Mmh, hadi lini?”

“Nitakujulisha.”

“Sawa.”

Baada ya mazungumzo hayo, haraka sana Grace aliingia chumbani na kumuacha Magesa sebuleni, ambapo alianza kukusanya vitu muhimu na kuviweka kwenye mabegi tofauti.

Kesho yake Grace alisafiri huku akimsisitiza Magesa kutothubutu kutoka nje ya nyumba hiyo, aliweka sawa mambo yote muhimu ikiwemo chakula cha kutosha na huduma zingine.

Siku mbili baada ya Grace kusafiri, ghafla Magesa alipata wazo la kukagua baadhi ya vitu ndani ya nyumba hiyo ili kuweza kujua Grace alikuwa mtu wa aina gani.

Alipekua kila kitu ikiwemo baadhi ya mabegi ambapo katika hali ambayo hakuitarajia alikutana na nyaraka nyeti za nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania zikiwa na siri nzito za kiserikali. Pia alishangaa kuona hati mbalimbali za kusafiria zenye utambulisho wa majina tofauti ya Grace hali ambayo ilizidi kumchanganya.

Kubwa zaidi na lililozidi kumuweka njia panda Magesa, ni baada ya kufunua mahali na kukutana na rundo la silaha mbalimbali za kisasa, zikiwa zimefichwa mahali ambapo haikuwa rahisi mtu kuziona.

Magesa alichanganyikiwa sana, akiwa ameshika nyaraka hizo alisogea hadi kitandani na kuendelea kuzisoma moja baada ya nyingine. Magesa alipigwa butwaa alipokuwa akisoma waraka wa mwisho.

Je, nini kitafuata? Usikose kufuatilia Siku ya Ijumaa kwenye Gazeti la Uwazi Mizengwe.

Leave A Reply