The House of Favourite Newspapers

Ticha J; Waziri Anayezidi Kutusua Kisiasa, ni Mtoto wa Mamalishe

0

JUMAA Hamidu Aweso ni mojawapo ya mawaziri vijana zaidi katika Baraza la Mawaziri lililotangazwa hivi karibuni na Rais John Magufuli. Aweso ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, anafahamika pia kwa jina la Ticha J, au mwalimu J.

 

Hilo ndilo jina alilopewa na wanafunzi wake wa Shule ya Sekondari Kisarawe ambako alifundisha wa muda mfupi kabla ya kuhamishia nguvu kwenye siasa na kufanikiwa kutusua katika jimbo la Pangani kwa vipindi viwili mfululizo.

 

Ukimtazama kwa haraka, waweza kudhani kuwa kufanikiwa kisiasa ni jambo rahisi. Hata hivyo, yeye binafsi katika mahojiano mbalimbali aliwahi kueleza ugumu aliokutana nao katika harakati zake kisiasa jambo ambalo linazidi kumpa ukomavu katika nafasi hizo za uongozi.

 

Ndoto ya Aweso ilianza kutimia baada ya  kwenda likizo nyumbani kwao mwaka 2012 na kukuta uchaguzi wa wajumbe wa kamati kuu ya halmashauri kuu ya CCM (NEC) Pangani.

 

“Nikaenda kwenye kopo la mama anakoweka fedha nikachukua Sh 10,000 kwa ajili ya fomu kugombea nafasi ya mjumbe wa NEC, lakini wakaniambia mimi mdogo sana sitaweza nafasi hiyo lakini nilikomaa mpaka jina langu likapita.”

 

KIONGOZI MWENYE MAONO

Katika moja ya mazungumzo yake, Aweso alisema moja ya sababu ya kusaka nafasi za uongozi, ni baada ya kumshuhudia mama mjamzito akijifungua kando ya nyumba yao baada ya mama huyo kukosa usafiri wa kivuko cha Pangani kuelekea hospitali.

 

Kwa kuwa mama huyo alipoteza maisha, huku mtoto akipona, alimuahidi mama yake ambaye ni mama lishe kuwa lazima atasoma na kuja kuwa kiongozi ambaye atawaondolea wananchi wa Pangani adha hiyo ya usafiri na kuiboresha sekta ya afya.

 

Kutokana na maono yake kiongozi, Aweso alifanikiwa kuvuka vihunzi ndani ya CCM na fitina zote za uchaguzi mwaka 2015, licha ya kutishiwa kuwa atapooza (kiharusi) iwapo ataendelea na harakati za kugombea ubunge.

 

Baada ya kumbwaga aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Salehe Pamba ndani ya CCM na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Hesabu za Serikali (PAC), Amina Mwidau katika kinyang’anyiro cha ubunge, ni dhahiri kuwa nyota yake kisiasa imezidi kunga’a.

MOTISHA KWA VIJANA

Aweso ambaye mama yake ni maarufu huko Pangani kwa shughuli za mamalishe, ameendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wanaoingia katika siasa hasa kutokana na utendaji wake kuzidi kumvutia Rais John Magufuli.

 

Kwa kuwa Rais Magufuli ni mmoja wa viongozi wasiopenda uzembe, pia alitoa nafasi kubwa kwa vijana ambapo mwaka 2017 alimteua Aweso kuwa Naibu Waziri wa Maji na umwagiliaji na sasa amemteua kuwa waziri kamili wa wizara hiyo.

 

HAJASAHAU ALIPOTOKA

Katika moja ya tafakuri yake, Aweso aliandika hivi katika ukaunti yake ya Instagram; “Weekend ya leo nimeitumia kufanya tafakuri ya ujenzi wa Taifa nikagundua silaha moja wapo ni sekta ya Elimu na hasa Watu muhimu sana katika nchi hii ni waalimu.

 

“Nimekumbuka nilipotoka nikiwa mwalimu Kisarawe namna ambavyo leo nayaona matunda ya baadhi ya wanafunzi wangu, nilifundisha kwa moyo sana na kuwafanya wanafunzi wangu wa Somo la kemia (Chemistry) na Physics kuibuka vinara katika mitihani yao ikiwemo kuongoza katka masomo haya kiwilaya.

 

“Hisia zimenipeleka mbali nilivopanda mbegu ilio bora kwa wanafunzi na moaka leo nikipita maeneno ya Kisarawe jamii nzima inaweza kuzizima kwa furaha na zitasikika sauti zikiita “Mwalimu J”. .(Teacher J)

 

“Ni kwa namna nilivojitoa kama Mwalimu bora, kutumia muda wa ziada kufundisha tuition na kila niwezalo kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi. Nazikumbuka tuition zangu za shillingi mia mia zilivokua zainajaza vijana kuja kupata maarifa ya masomo ya Chemistry Na Physics.

 

“Nakiri kuwa ile ndio ilikua kazi yangu ya kwanza kunifanya kushika pesa nyingi katika maisha yangu nilipopewa mshahara wa laki 400,000 kama mshahara mwaka 2008.

 

“Niliheshimu na kuitendea haki kazi ile. Katika kila hatua tunayopitia katika maisha tuitendee haki kweli na kuacha alama. Mwisho naamini elimu ndio ukombozi wa kweli wa mtanzania na hasa hii imepelekea kuibeba ajenda hii kama kipaumbele kwa Jimbo la Pangani.”

 

WACHAMBUZI: NI ZAO LA MARAIS VIJANA WA KESHO

Baadhi ya wachambuzi pamoja na wadadisi kadhaa waliokaribu na Aweso, wanamtazama waziri huyo, kama kiaja asiyesita kufanya maamuzi.

 

 Kauli za wachambuzi hao akiwamo Samson Mwigamba wanasema hatua za hivi karibuni alizochukua waziri huyo zinaendana na kasi ya Rais Magufuli.

 

“Hata alipokuwa Naibu Waziri, tumemshuhudia mara kadhaa akichukua hatua dhidi ya wabadhirifu na wazembe. Lakini mipango yake ya kumtua mama ndoo kichwa inatakiwa kutekelezwa kwa vitendo kwa sababu bado tatizo la maji ni kubwa,” alisema.

 

Mwigamba aliongeza kuwa anamuona Aweso kuwa ni mwakilishi sahihi wa vijana;  “kwa sababu tulishasema vijana ni taifa la leo sio la kesho. Vitabu vitakatifu vinasema wazee wataota ndoto, vijana wataona njozi, sasa vijana wanaiangalia kesho lakini wazee wanazungumzia uzoefu. Kwa hiyo tunahitaji wazee kutupatia muongozo na vijana kutekeleza sasa.

 

“Awamu zilizopita tuliona kama vijana wanaachwa, waliokuwa wakipewa nafasi waliboronga, lakini tunashuruku kuona watu kama akina Jumaa Aweso, Anthony Mavunde, Husein Bashe na Innocent Bashungwa wakifanya vizuri,” anasema.

 

 Anasema vijana hao wamemfanya Rais Magufuli azidi kuwamini na sasa amewa nafasi ya uwaziri kwa awamu nyingi.

“Kwa hiyo utendaji kazi wao kama wataendelea vizuri, unaweza kusababisha kwa mara ya kwanza tukapa rais kijana, kwamba rais mwenye umri kuanzia miaka 40 na 50,” alisema.

CHANGAMOTO NDANI YA WIZARA

Katika mojawapo ya changamoto kubwa kitaifa, ni upatikanaji wa maji. Wiraza aliyopewa Aweso ni kipimo toshelevu kwake katika kufikia lengo namba sita la Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2015-2030. Lengo hilo linaweka msisitizo wa upatikanaji wa huduma za maji safi na salama na usafi wa mazingira kwa wote.

 

Lengo la wizara hiyo ni  kuwapatia wananchi vijijini huduma ya maji katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao ili kufikia asilimia 85 kwa wananchi wanaopata huduma ya maji safi na salama. Vivyo, hivyo kwa maeneo ya mijini lengo ni kufikia asilimia 90.

 

JUMAA AWESO NI NANI

Jumaa Aweso amezaliwa Machi 22, 1985. Ni kijana wakitanzania ambaye pia ni mwanachama wa CCM tangu mwaka 2012. Aweso ambaye sasa ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji pia ni mbunge wa Pangani  mkoani Tanga.

 

Aweso ni mtoto wa pili kati ya watoto sita. Amehitimu Shahada ya Kemia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 2013. Shule ya Sekondari amesoma Pugu na kidato cha tano na sita nimesoma Shule ya Sekondari Bagamoyo. Alianza elimu ya msingi mwaka 1994 na kuhitimu mwaka 2000 huko Mwambao.

NA GABRIEL MUSHI

Leave A Reply